Vatican News
Meli ya Hospitali ya Papa Francisko ni chombo cha huduma ya afya na Neno la Mungu; jibu la kilio cha maskini Ukanda wa Amazonia. Meli ya Hospitali ya Papa Francisko ni chombo cha huduma ya afya na Neno la Mungu; jibu la kilio cha maskini Ukanda wa Amazonia. 

Meli ya Hospitali ya Papa Francisko: Huduma ya Afya & Neno la Mungu Ukanda wa Amazonia

Meli itatoa huduma ya afya na itatumika pia kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu wanaoishi Kando kando ya mto wa Rio, Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo ameunga mkono jitihada hizi za uinjilishaji hatua kwa hatua na umuhimu wake kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Ukanda wa Amazonia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Lengo la Sinodi ya Maaskofu Katoliki Ukanda wa Amazonia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019, na kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani" ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, zitakazokidhi mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linataka kuendeleza mchakato wa utamadunisho kwa kuhakikisha kwamba, tunu msingi za kiinjili zinamwilishwa katika tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Ukanda wa Amazonia pamoja na kuzisafisha zile zinazosigana na kupingana na Injili ya Kristo. Ni Sinodi itakayojikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kama njia ya kuenzi: maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maadhimisho ya Sinodi yanapania pia kuibua mbinu mkakati wa maboresho ya maisha ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia.

Ni katika muktadha wa huduma na maendeleo fungamani ya binadamu, “Meli ya Hospitali ya Papa Francisko” , Jumamosi, tarehe 17 Agosti 2019 imewasili Jimbo kuu la Belèm lililoko Kaskazini mwa Brazil, kwa ajili ya kutoa huduma ya tiba katika maeneo ya Ukanda wa Amazonia, yanayoweza kufikiwa tu kwa kutumia usafiri wa majini. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mchakato wa Injili ya huruma na huduma ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, amemwandikia ujumbe wa pongezi na shukrani, Askofu Bernardo Bahlmann wa Jimbo Obidos, nchini Brazil. Huyu ndiye muasisi wa huduma ya afya kwa njia ya “Meli ya Hospitali ya Papa Francisko” kwa kushirikiana na Wafranciskani wanaotoa huduma ya afya kwenye Hospitali ya Rio de Janeiro, nchini Brazil.  Meli hii pamoja na kutoa huduma ya afya sehemu muhimu sana ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, itatumika pia kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu wanaoishi Kando kando ya mto wa Rio, Ukanda wa Amazonia.

Baba Mtakatifu ameunga mkono jitihada hizi za uinjilishaji hatua kwa hatua na umuhimu wake kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Ukanda wa Amazonia. Hili ni jibu makini kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye amesikiliza na kujibu kilio cha waja wake, na sasa amewatuma wamisionari watakaojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kusimika Ufalme wa Mungu, kwa kuwaganga na kuwatibu wagonjwa pamoja na kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Hiki ni kielelezo cha imani na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Hii ni alama ya Kristo Yesu anayetembea juu ya Bahari ili kutuliza dhoruba ya magonjwa sanjari na kuimarisha imani ya wafuasi wake. Ni meli inayopania kuleta faraja, amani na utulivu wa ndani kwa watu wa Mungu waliokuwa wametelekezwa kwa kukosa huduma ya afya. Huu ndio ushuhuda wa imani ya Kanisa inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wafanyakazi wa afya, watu wa kujitolea, wafadhili pamoja na wale wote watakaofaidika na huduma hii ya furaha ya Injili, kwa kuwakabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, afya ya wagonjwa. Anaiomba familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia, kumkumbuka katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kuendelea kuombea ufanisi katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Ukanda wa Amazonia. Itakumbukwa kwamba, “Meli ya Hospitali ya Papa Francisko” ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013 iliyoadhimishwa Rio de Janeiro, alipogundua kwamba, kutokana na hali mbaya ya miundo mbinu, watu wengi waliokuwa kwenye pembeni mwa Mto Rio, hawakua na fursa ya kupata huduma ya shughuli za kichungaji wala matibabu.

Huu ukawa ni mwanzo wa uundwaji wa “Meli ya Hospitali ya Papa Francisko” kama jibu makini la kimaadili kutokana na nyanyaso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu katika eneo hili. Kampuni ya Shell na Basf S.A zimeshiriki kuchangia katika mchakato wa kuundwa kwa meli hii, kwani Kampun ya Shell iliwahi kusababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira uliopelekea watu 60 kupoteza maisha kutokana na ajali ya moto pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira.

Meli ya Papa Francisko

 

 

20 August 2019, 14:16