Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico. Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico. 

Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Kardinali Sergio Obeso Rivera

Marehemu Kardinali Sergio Obeso Rivera, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86, katika miaka hii, amemtumikia Mungu kama Askofu kwa miaka 48 na katika Daraja takatifu ya Upadre miaka 65, si haba hata kidogo! Ibada ya mazishi yake imefanyika kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico, Jumanne, tarehe 13 Agosti 2019. Papa Francisko amesitishwa na msiba huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea taarifa za kifo cha Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico, aliyefariki dunia, Jumapili, tarehe 11 Agosti 2019 huko Coatepec kwa masikitiko makubwa. Marehemu Kardinali Sergio Obeso Rivera, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86, katika miaka hii, amemtumikia Mungu kama Askofu kwa miaka 48 na katika Daraja takatifu ya Upadre miaka 65, si haba hata kidogo! Ibada ya mazishi yake imefanyika kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico, Jumanne, tarehe 13 Agosti 2019. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi alizomtumia Askofu mkuu Hipòlito Reyes Larios wa Jimbo kuu la Xalapa, anamwelezea Kardinali Rivera kuwa ni kiongozi ambaye amemtumikia Mungu na Kanisa kwa uaminifu, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Mexico. Baada ya huduma yote, hii, sasa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumstahilisha Mtumishi wake mwaminifu taji ya utukufu, maisha na uzima wa milele.

Kardinali Sergio Obeso Rivera, ni kiongozi ambaye amewahudumia watu wa Mungu nchini Mexico katika kipindi tete! Akaliwezesha Kanisa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa haki, amani na maridhiano nchini Mexico na matokeo yake ni “Mkataba wa Amani wa San Andrès”. Ni kiongozi aliyefanikiwa pia kurejesha tena uhusiano mwema kati ya Vatican na Serikali ya Mexico. Itakumbukwa kwamba, alizaliwa tarehe 31 oktoba 1931 huko Xalapa nchini Mexico. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 31 Oktoba 1954 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kwa muda wa miaka 17 alitekeleza dhamana na utume wake wa Kipadre kama Jaalimu wa Falsafa na Taalimungu; Mkurugenzi wa maisha ya kiroho na hatimaye kama Gombera. Kunako mwaka 1971 Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 29 Julai 1971.

Tarehe 18 Januari 1974 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Papantla na Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Xalapa. Akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Xalapa tarehe 12 Machi 1979. Tarehe 18 Novemba 1982 akachaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico kwa vipindi vitatu hadi mwaka 1995. Tarehe 10 Aprili 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akaridhia ombi lake la kung’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa nchini Mexico kunako tarehe 28 Juni 2018 akamteuwa na kumsimika kuwa Kardinali. Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico, apate rehema kwa Mungu na apumzike kwa amani. Kutokana na kifo cha Kardinali Rivera kwa sasa Baraza la Makardinali linaundwa na Makardinali 216, kati yao wenye haki ya kupiga na kupigia kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni 119 na waliosalia 97 hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura!

Papa: Rambi rambi
13 August 2019, 13:59