Tafuta

Vatican News
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 inaongozwa na kauli mbiu: Matumaini, amani na upatanisho. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 inaongozwa na kauli mbiu: Matumaini, amani na upatanisho.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Matumaini, Amani & Upatanisho

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 itamwezesha kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Rais Filipe wa Msumbiji anasema, hija hii inapania kuimarisha imani, matumaini, mapendo na upatanisho wa kitaifa. Kumenoga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 kwa kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Radio Vatican leo inapenda kuzama zaidi katika hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji kuanzia Jumatano tarehe 4 Septemba hadi Ijumaa, tarehe 6 Septemba 2019 atakapohitimisha na kuondoka kuelekea Antananarivo, nchini Madagascar. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuondoka mjini Roma saa 2:00 za asubuhi na kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maputo majira ya saa 12:30 jioni ambako atafanyiwa mapokezi ya kitaifa.

Alhamisi, tarehe 5 Septemba 2019, Baba Mtakatifu atamtembelea Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji pamoja na kufanya naye mazungumzo ya faragha. Baadaye, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanadiplomasia, viongozi wa kisiasa pamoja na vyama vya kiraia. Itakumbukwa kwamba, majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na kuzungumza na vijana kutoka dini na madhehebu mbali mbali nchini Msumbiji, ili kuwaimarisha katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama sehemu pia ya mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya vita na kinzani, zilizoipekenya Msumbuji kwa miaka mingi.

Baada ya chakula cha mchana kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Msumbiji, Baba Mtakatifu Francisko, Alasiri atakutana na kuzungumza na Maaskofu, Mapadre, Watawa, Makatekista, Waseminari pamoja na walezi wao kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji. Na kwa tukio hili, Baba Mtakatifu atakuwa anahitimisha siku yake ya pili nchini Msumbiji. Ijumaa, tarehe 6 Septemba 2019, Baba Mtakatifu asubuhi kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zimpeto, atatembelea Hospitali ya Zimpeto na kusalimiana na wagonjwa. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu atakuwa amemaliza hija yake ya kitume nchini Msumbiji kama hujaji wa matumaini, amani na upatanisho.

Wakati huo huo, Habari kutoka Maputo Msumbiji zinabainisha kwamba, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, tayari amekwisha tembelea na kukagua maeneo yote yatakayotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Msumbiji. Rais Nyusi amedhamiria na anataka kuhakikisha kwamba, Msumbiji inajenga na kudumisha misingi ya haki, amani na umoja wa kitaifa, ndiyo maana hivi karibuni, Chama cha FRELIMO kimewekeana tena sahihi Mkataba wa Amani na Chama cha RENAMO, ambacho kwa sasa kinaongozwa na Bwana Ossufo Momade. Lengo ni kusitisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia; pamoja na kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama wa Msumbiji unaendelea kuimarishwa. Mkataba huu, unaweka matumaini makubwa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Ndiyo maana Rais Nyusi anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji inafanyika kwa wakati muafaka, Msumbiji inapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa ajili ya amani, ustawi na maendeleo ya watoto wake. Serikali ya Msumbiji imetangaza kwamba, tarehe 6 Septemba 2019 itakuwa ni siku ya mapumziko kitaifa, ili kutoa fursa kwa watu wengi kuweza kuhudhuria na kushiriki katika tukio hili la kihistoria, ili kupyaisha tena matumaini, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Msumbiji. Rais Nyusi amewahakikishia waandishi wa habari kwamba, Msumbiji, kumenoga, wako tayari kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuwatembelea, ili aweze kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo!

Papa: Msumbiji

 

23 August 2019, 11:21