Vatican News
Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Tume imeundwa ili kufuatilia kwa karibu zaidi utekelezaji wake katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Tume imeundwa ili kufuatilia kwa karibu zaidi utekelezaji wake katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.  (AFP or licensors)

Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Kamati ya Utekelezaji yaundwa!

Kwa kutambua umuhimu na uzito wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, kumeundwa Kamati ya Utekelezaji wa Hati hii na kati ya wajumbe wake ni pamoja na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar, Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba, binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo.

Ni tafakari ambazo zimezingatia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, tiba ya mwanadamu pamoja na maboresho makubwa yanayoendelea kujitokeza katika vyombo vya mawasiliano ya jamii. Viongozi hawa wakuu, walitafakari kwa kina na mapana kuhusu hali na kiwango cha umaskini, vita, kinzani na athari zake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inagusia kuhusu mashindano ya utengenezaji na biashara haramu ya silaha duniani na madhara yake katika maisha ya watu. Ukosefu wa haki jamii, kuenea kwa rushwa na ufisadi; ukosefu wa haki na fursa sawa; kumong’onyoka kwa tunu na kanuni maadili pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Ni katika muktadha huu, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inataka kukumbatia ya mbeleni kwa imani na matumaini makubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Ni hati inayowachangamotisha waamini wa dini mbali mbali kujenga na kuimarisha imani yao kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa na imani na udugu wa kibinadamu, ili waweze kushirikiana, kushikamana na kufanya kazi katika umoja na udugu. Hati hii inaweza kuwa ni dira na mwongozo kwa vijana wa kizazi kipya kama sehemu ya majadiliano ya kidini na kitamaduni; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, huku wakiheshimu neema ya Mwenyezi Mungu inayotenda kazi ndani mwao. Hati hii inakazia maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Inawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na huruma, kwa kuonesha ukarimu kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji; wahanga wa vita na mashambulizi mbali mbali; wafungwa wa vita na watu wasiokuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Udugu wa kibinadamu usaidie kuganga na kuponya: kinzani na mipasuko inayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia kwa kutumiwa na wajanja wachache kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Hati hii inakazia uhuru, haki, amani; upendo, msamaha na huruma kama mambo msingi ya imani. Hati inajielekeza zaidi katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ushirikiano na mshikamano; kwa kuzingatia kanuni maadili, vigezo na viwango kuzingatiwa. Waamini wote wanasubiri siku ya hukumu kwa kuzingatia wajibu wa waamini hawa kimaadili na kiutu. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inawaalika: Viongozi wa kidini; viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa; Watunga sera; Wachumi wa Kimataifa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushirikiana na kushikamana katika ujenzi wa utamaduni wa maridhiano, haki na amani, ili hatimaye, kusitisha vita, kinzani na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Umefika wakati wa kugundua tena tunu msingi zinazofumbatwa katika amani, haki, wema, uzuri, udugu wa kibinadamu, upendo na mshikamano. Huu ni mwamba salama wa wokovu kwa watu wote; mambo yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Kwa kutambua umuhimu na uzito wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, kumeundwa Kamati ya Utekelezaji wa Hati hii na kati ya wajumbe wake ni pamoja na: Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu. Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Amiri Jeshi Msaidizi, watahakikisha kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatekelezwa kwa dhati kabisa na Kamati iliyoundwa, ili kumwilisha malengo yaliyobainishwa kwenye Hati hii.

Kamati pamoja na mambo mengine, itakuwa na dhamana ya kuandaa miradi maalum itakayotumika kumwilisha hati hii katika ngazi ya kikanda na kimataifa. Kamati inatarajiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa dini, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na watu mashuhuri duniani, ili kuunga mkono hati hii pamoja na kuendeleza malengo ya Hati ya Udugu wa Kibinadamu ambayo itaendelea kuwa rejea ya kihistoria kwa sasa na kwa siku za usoni. Inafikiriwa kuwahusisha pia watunga sera pamoja na wabunge ili kuwahamasisha kushiriki katika utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu katika ngazi ya kitaifa, ili tunu msingi za haki, amani na maridhiano kati ya watu ziweze kukita mizizi yake kwa waamini wa dini mbali mbali kuheshimiana na kuthaminiana. Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu utaratibiwa na kusimamiwa na Jumba la Makumbusho la “Abrahamic Family House” yaliyotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Hija ya 27 ya Kitume kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019 iliyoongozwa na kauli mbiu “Nifanye chombo cha amani”.

Ziara hii ilipania kuandika ukurasa mpya wa historia na matumaini ya watu wa Mungu mintarafru majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika kutafuta, kulinda na kudumisha amani duniani, ili kukihakikishia kizazi cha sasa na kile kijacho mazingira ya haki, amani na utulivu. Umoja wa Falme za Kiarabu umejitwalia dhamana ya kuhakikisha kwamba unaendeleza majadiliano ya kidini, kwa kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiutu, kiimani na kitamaduni, ili kuimarisha maridhiano, amani na ujenzi wa umoja wa kidugu miongoni mwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia!

Kamati: Udugu
21 August 2019, 16:16