Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko: Barua kwa Mapadre Wote Duniani: Shuhuda za Mapadre mbali mbali jinsi walivyoguswa na barua hii katika maisha na utume wao! Baba Mtakatifu Francisko: Barua kwa Mapadre Wote Duniani: Shuhuda za Mapadre mbali mbali jinsi walivyoguswa na barua hii katika maisha na utume wao! 

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Duniani: Shuhuda!

Mapadre wengi wameguswa na jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko alivyoiandika barua hii, kama rafiki wa Mapadre; Baba na Mwalimu wa maisha ya kiroho; anayetambua na kuguswa na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali katika maisha, wito na utume wa Kipadre. Mapadre watambue kwamba, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu, lakini bado ni muhimu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney inaonesha: Ukuu, wito na utakatifu wa maisha ya Kipadre. Katika barua hii, Baba Mtakatifu anakazia pamoja na mambo mengine: Maisha ya Kijumuiya, ili kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa Mapadre, huku wakisaidiana katika uhalisia wa maisha na utume wao. Ni kwa njia ya umoja na mshikamano, Mapadre wataweza kukabiliana uso kwa uso na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu ameandika Barua hii kama kiongozi na mchungaji mkuu anayetambua: furaha, shida, changamoto na fursa mbali mbali walizo nazo Mapadre katika maisha na huduma kwa watu wa Mungu. Barua hii ni matunda na safari ya utamaduni wa kukutana na kuzungumza na Mapadre kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama njia ya kushirikishana: ukuu, utakatifu, changamoto na fursa mbali mbali zinazojitokeza miongoni mwa Mapadre kama wahudumu wa Neno, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma yanayotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Mtakatifu Yohane Maria Vianney ni mfano bora wa kuigwa katika upendo na ukarimu wa kichungaji; sadaka na utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu. Wito na maisha ya Kipadre yanafumbatwa katika sadaka na majitoleo binafsi; huruma, upendo na unyenyekevu wa moyo; mambo ambayo mara nyingi yanafanyika sirini, lakini Baba yao wa mbinguni anayafahamu hayo yaliyofichika machoni pa waja wake. Mtakatifu huyu ni mfano bora wa kuigwa katika maisha kama mtu binafsi na kama Jumuiya ya Mapadre, wakitambua kwamba, wamepakwa mafuta kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.  Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili ya upendo na matumaini kwa watu wa Mungu. Licha ya udhaifu na mapungufu yanayooneshwa na baadhi ya Mapadre, lakini kuna umati mkubwa wa Mapadre unaoendelea kuandika kurasa za ushuhuda wa utakatifu wa maisha yanayosimikwa katika sadaka na huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Ni katika muktadha huu, Mapadre kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaendelea kutoa ushuhuda wa jinsi ambavyo wameguswa na barua hii ya Baba Mtakatifu Francisko inayopembua kwa kina na mapana: mateso na mahangaiko ya Mapadre sehemu mbali mbali za dunia. Shukrani kwa Mapadre kwa wito na majitoleo yao; Neno la faraja na mwishoni ni utukufu na ukuu wa Mungu. Padre Dominic Ngo Quang Tuyen kutoka Vietnam, mwenye umri wa miaka 71 anasema, katika maisha yake kama Padre, amewahi kutumikia kifungo cha miaka 13 akiwa gerezani; mara 7 amefanyiwa opresheni kubwa ya moyo ili kuokoa maisha yake, lakini pamoja na patashika nguo kuchanika, bado anaendelea na utume wake kama Padre nchini Vietnam. Kwa namna ya pekee kabisa ameguswa na jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko alivyoiandika barua hii, kama rafiki wa Mapadre; Baba na Mwalimu wa maisha ya kiroho; anayetambua na kuguswa na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali katika maisha, wito na utume wa Kipadre.

Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime Mapadre wote katika maisha na utume wao, ili watambue kwamba, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu, lakini bado wana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwani wao ni wahudumu wa Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma. Madonda ya maisha na utume wa Mapadre, yawasukume kukimbilia ili kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na faraja ya Mungu kwa watu wake! Kamwe Mapadre wasikubali kukata wala kukatishwa tamaa, bali waonje uwepo mwanana wa jirani zao, ili wasitumbukie katika upweke hasi unaoweza kuwatumbukiza hata katika kifo! Uchungu wa moyo utawanyima Mapadre kutekeleza utume wao kwa ari na moyo mkuu; watashindwa kuona umuhimu wa sala na hapo kwa hakika maisha yatakuwa ni magumu na machungu sana! Padre Dominic Ngo Quang Tuyen kutoka Vietnam anasema, ana mazoea ya kusoma nyaraka mbali mbali za Baba Mtakatifu Francisko, lakini Barua kwa Mapadre Wote Duniani, imemgusa na imekuwa kama kioo na faraja kwa maisha na utume wake. Ameguswa na upendo wa Baba Mtakatifu kwa Mapadre ambao kimsingi amekuwa ni: rafiki, baba na mwalimu.

Kwa upande wake Padre Santosh Kumar Digal kutoka India anasema, Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani imekuja kwa wakati muafaka kama chemchemi ya  imani, upendo wa kidugu, matumaini pamoja na kuwatia shime Mapadre kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu licha ya changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika ulimwengu mamboleo! Padre Santosh Kumar Digal anasema, ana miaka 19 tangu alipopewa Daraja ya Upadre. Katika maisha na utume wake, kuna wakati amewahi kujisikia upweke hasi, kiasi cha kujiuliza umuhimu wa kuendelea na wito na maisha kama haya ya Kipadre! Lakini katika Barua ya Baba Mtakatifu kwa Mapadre amepata neno la faraja, linalomtaka kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Hii ni huduma inayomtaka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Awe makini kwa kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Awe mstari wa mbele kuhimiza haki jamii licha ya changamoto pevu zilizoko mbele yake. Kwa hakika, kuna Mapadre wanaoteseka kutokana na makosa, mapungufu na udhaifu uliooneshwa na baadhi ya Mapadre katika maisha na utume wao!

Jambo la msingi ni kwa kila Padre kuendelea kuwa mwaminifu na mdumifu kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Barua hii imemkumbusha nyakati zile za furaha katika maisha na utume wake kama Padre; watu mbali mbali aliobahatika kukutana nao katika malezi na majiundo yake ya Kipadre, kiasi kwamba, wakawa ni chemchemi ambayo imemsaidia kuhifadhi tunu msingi za maisha na wito wa Kipadre, Barua hii imemkumbusha kwa mara nyingine tena changamoto ya utume wa kimisionari; umuhimu wa kuzama tena katika Injili ya Kristo, ili hatimaye, aweze kuwa ni chombo na shuhuda wa furaha ya Injili; upendo na matumaini kwa wale wote waliokata tamaa. Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani ni kikolezo cha maisha na utume wa Kipadre. Huu ni wakati wa “kusimama dede katika shughuli za kichungaji” kila Padre kadiri ya utume wake.

Naye Padre Juan Mardoqueo Aj Luis kutoka Guatemala anaungana na Baba Mtakatifu Francisko kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha ya Mapadre kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuyaambata ya mbeleni kwa matumaini makubwa na kwamba, maisha yao yote yawe ni wimbo wa utukufu kwa Mwenyezi Mungu. Mapadre wajifunze kujiaminisha na kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Wajenge na kudumisha maisha yao katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha; wakidumu katika ukweli na unyoofu, bila kumezwa na malimwengu. Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kielelezo makini cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Umaskini, magonjwa, shida na mahangaiko ya watu wa Mungu iwe ni sababu ya mshikamano na waamini wao kama kielelezo cha Kristo Yesu, Mchungaji mwema. Bikira Maria awe ni kimbilio na tunza ya Mapadre katika maisha na wito wao. Barua ya Baba Mtakatifu kwa Mapadre wote duniani ni amana na utajiri wa maisha ya kiroho.

Padre Andrea Simone, kutoka Jimbo Katoliki la Fabriano, Italia anasema, ametumia kipindi hiki cha likizo ya kiangazi kusoma na kutafakari kwa kina Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Wote Duniani na kugundua amana na utajiri mkubwa unaobubujika kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Anawashukuru, anawapongeza na kuwatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu ili kuendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa tunu msingi za Kiinjili, huku wakiendelea kujibidiisha kuwa kweli ni wachungaji wema, walio tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.  Padre Andrea Simone ameguswa kwa namna ya pekee na Sala ya Makuhani inayoboreshwa kwa kumwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu katika furaha, shida na mahangaiko yao ya kila siku. Mapadre wawe daima ni vyombo vya sala kwa ajili yao wenyewe na watu wa Mungu wanaowahudumia! Mapadre wasiwe na majibu ya mkato kwa waamini wao, bali sala iwe ni nguvu inayoongoza maisha yao, kwa kutambua karama na udhaifu wao wa kibinadamu. Mapadre wakuze mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu, ili kuungana naye daima, vinginevyo watakuwa kama taa zisizokuwa na mafuta.

Kwa njia hii, Mapadre wataweza kusumbukiana na kunyanyuana pale wanapojikuta wakiwa wanaogelea katika mawimbi mazito ya maisha. Mapadre wajenge mahusiano mema na adili na watu wanaowahudumia, kamwe wasikimbilie kujificha katika makundi ya wasomi. Padre awe kati pamoja na watu wake, awatie shime na kukubali kupokea ushauri kutoka kwao kwani wao pia wana utambuzi wa imani “Sensum fidei”. Kristo Yesu anawahamasisha Mapadre wake kuwa kati kati ya watu wa Mungu, kwa kuhakikisha kwamba, wanawajali watu wao, mtindo wa maisha ambao Yesu aliutumia kama njia ya kuinjilisha! Watu wa Mungu wanaona fahari kuwa karibu na Mapadre katika shida na mahangaiko yao; wakati wa raha na faraja. Mapadre wawe na ujasiri kama wa Bikira Maria wa kusema, “Fiati mihi” yaani “Nitendewe kama ulivyosema”.

Padre Tiziano Cantisani, Paroko wa Parokia ya Maratea, Jimbo la Tursi-Lagonegro, lililoko nchini Italia anasema, barua inahitaji umakini mkubwa kutoka kwa mwandishi na anayepelekewa ujumbe huu, anapaswa kuusoma kwa umakini mkubwa, ili ujumbe huu, uweze kumwangazia katika mapito yake. Hii ni barua ambayo ni muhtasari wa maisha, utume na wito wa Kipadre, katika utakatifu na changamoto zake. Ni barua inayowaangalisha Mapadre kujikita zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu kama chemchemi ya furaha, matumaini, imani na mapendo, licha ya mapungufu na udhaifu wao wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anawashukuru Mapadre kwa uaminifu na sadaka wanayotoa kila kukicha, kielelezo cha utekelezaji wa Agano la Mungu lisilokuwa na kikomo. Ni wakati wa kusherehekea uaminifu wa Mungu usiokuwa na kikomo, kwani bado anaendelea kuwaamini licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, kwa kutambua kwamba wanabeba wito huu mtakatifu katika vyombo vya udongo. Wanatambua kwamba, hata katika udhaifu wao, Mwenyezi Mungu anaweza kuonesha ukuu na ushindi kwa sababu huruma yake yadumu milele.

Baba Mtakatifu anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wito wa Upadre kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambao si kwa mastahili yao wenyewe, bali wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kipindi cha shida na magumu ya maisha, iwe ni fursa ya kurejea tena katika zile nyakati angavu za sadaka na huduma kwa watu wa Mungu, ili kugundua tena neema za Mungu katika maisha na utume wao, ili kuwasha tena furaha inayokita mizizi yake katika unyenyekevu, ili kamwe majonzi na uchungu wa moyo, yasizime ile furaha na uungwana! Baba Mtakatifu anawashukuru Mapadre, anawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu ili waendelee kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Barua kwa Mapadre: Ushuhuda
20 August 2019, 15:30