Vatican News
Papa Francisko anaendelea kuunga mkono jitihada za Makanisa mahalia katika kuimarisha mbinu mkakati wa ulinzi, usalama, ustawi, malezi na makuzi ya watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Papa Francisko anaendelea kuunga mkono jitihada za Makanisa mahalia katika kuimarisha mbinu mkakati wa ulinzi, usalama, ustawi, malezi na makuzi ya watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Nyanyaso za Kijinsia: Kipaumbele: Ulinzi: Usalama na malezi ya Watoto!

Kituo cha "CUIDA" kitajihusisha zaidi na ushahidi wa kisayansi ili kutengeneza sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso za kijinsia. Kituo hiki kinaundwa na wataalam na wanasayansi kutoka katika medani mbali mbali za maisha. Licha ya kushughulikia nyanyaso hizi katika jamii, lakini “CUIDA” inataka kujielekeza zaidi katika maisha na utume wa Kanisa, ili kulinda: Utu, heshima na haki msingi za watoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utume wa kukinga. Mfumo wa kukinga ni urithi na amana kubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane Bosco ambao unapaswa kukita mizizi yake katika sekta ya elimu. Huu ni mfumo ambao unawataka wadau wote kuwa macho, ili kamwe wanafunzi wasijikute wakiwa wanahadaiwa na hatimaye kutumbukizwa katika nyanyaso za kijinsia, matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia na mambo kama haya!

Ulinzi, usalama, ustawi, maendeleo, malezi na makuzi ya watoto katika maeneo ya Kanisa ni muhimu sana. Baba Mtakatifu anaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia kama sehemu ya mpango mkakati wa kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Familia ya Mungu nchini Chile ni kati ya watu walioathirika sana kwa kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video, aliowatumia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Chile pamoja na Mfuko wa “Fundaciòn para la Confianza”, walioweka sahihi ya makubaliano ya kuanzishwa kwa Kituo cha “CUIDA” kitakachofanya tafiti na hatimaye kuibua sera na mikakati kuhusu jinsi ya kukinga nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Kituo hiki kitajihusisha zaidi na ushahidi wa kisayansi ili kutengeneza sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso za kijinsia. Kituo hiki kinaundwa na wataalam na wanasayansi kutoka katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Licha ya kushughulikia nyanyaso hizi katika jamii, lakini “CUIDA” inataka kujielekeza zaidi katika maisha na utume wa Kanisa, ili kulinda, na kudumisha utu, heshima na haki msingi za watoto.

Tafiti na misaada mbali mbali ya kisayansi ilenge zaidi anasema Baba Mtakatifu Francisko, ulinzi na usalama wa watoto wadogo, kwani haya ni mambo ambayo yanachafua sana malezi, makuzi, utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wahudumiwe kwa huruma na upendo; kwa heshima na utu wema. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliothubutu kuanzisha wazo hili, walioamua kulitekeleza na kwa namna ya pekee Askofu Celestino Aós Braco, O.F.M. Cap. Msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Santiago nchini Chile na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Chile. Hiki ni kielelezo cha kiongozi anayethamini malezi na makuzi ya watoto ambao ni tumaini la Kanisa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Papa: Chile
16 August 2019, 11:20