Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwasha taa ya imani kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwasha taa ya imani kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Papa Francisko: Taa ya Imani inawashwa kwa: Sala, Neno, Sakramenti & matendo ya huruma!

Taa ya imani inatakiwa kuwashwa daima, ili kuweza kukutana na Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Waamini wajenge utamaduni wa kutembea na Neno la Mungu katika mikoba yao, ili wanapopata mwanya, waweze kuboresha maisha yao, kwa kujisomea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwaangalisha wafuasi wake kukesha daima, ili waweze kuwa tayari Mwenyezi Mungu anapowapitia katika hija ya maisha yao hapa ulimwenguni, kwa sababu daima anawatembelea waja wake. Yesu anawaonesha mtindo wa maisha wanaopaswa kuufuata yaani, viuno vyao viwe vimefungwa na taa zao ziwe zinawaka. Huu ni mwaliko kwa waamini kujiandalia mazingira ya hija, tayari kutoka na kuanza safari, kwa kutambua kwamba, hapa duniani hawana makazi ya kudumu. Ni kutokana na mwelekeo huu, wanapaswa kujiachilia na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anatambua magumu yanayoweza kuwasibu waja wake, ndiyo maana anaamua kutembea nao hatua kwa hatua katika maisha. Kwa mtu anayejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu katika maisha ya kiroho anatambua kwamba, maisha ya binadamu ni endelevu yanayopitia hatua mbali mbali hadi kufikia kilele chake. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu daima anapenda kuwashangaza waja wake kwa upya wa maisha!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 11 Agosti 2019 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wafuasi wa Kristo wanapaswa kukesha, huku taa zao zikiwa zinawaka, ili kuliangazia giza la maisha ya mwanadamu. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha imani yao katika ukweli na uhalisia wa maisha. Kila mtu katika maisha yake, amewahi kuonja mwanga angavu wa maisha ya kiroho na hata wakati mwingine, wameonja na kutumbukia katika usiku wa giza la maisha ya kiroho. Taa ya imani inatakiwa kuwashwa daima, ili kuweza kukutana na Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujijengea utamaduni wa kutembea na Neno la Mungu katika mikoba yao, ili wanapopata mwanya, waweze kuboresha maisha yao, kwa kujisomea Neno la Mungu pamoja na kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza katika ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.

Hakuna mtu anayeweza kuwa na uhakika wa wokovu wake binafsi, kwa “kuwageuzia wengine kisogo kana kwamba, wao si mali kitu”. Imani ya kweli inawasaidia waamini  kuwafungulia jirani zao hazina na utajiri wa nyoyo zao, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu; kipaumbele cha kwanza wakiwa ni maskini na wale wenye kuhitaji zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, ili kweli wafuasi wa Kristo Yesu waweze kuelewa maana ya maneno yake, anawapatia mfano wa watu wanaomngojea bwana wao atakaporudi kutoka arusini. Hapa Kristo Yesu anaendelea kukazia umuhimu wa kukesha na kuwa tayari kuweza kukutana kwa mara ya mwisho na Mwenyezi Mungu. Kila mtu ameandikiwa siku na saa ya kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Kristo Yesu anakaza kusema, “Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao”. Waamini wanakumbushwa kwamba, maisha ya binadamu hapa ulimwenguni ni hija endelevu kuelekea maisha na uzima wa milele.

Changamoto na mwaliko kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema karama, utajiri na amana ambazo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kujiandalia makao mbinguni, kwani hapa ulimwenguni wao ni wapita njia tu. Kumbe, wanapaswa kufikiri na kutenda wakiwa wamesimama imara hapa duniani, lakini akili na nyoyo zao, zikiwa zinaelekezwa mbinguni. Kristo Yesu anawafafanulia waja wake kuhusu furaha ya maisha na uzima wa milele ni pale ambapo, Mwenyezi Mungu atajifunga ili aweze kuwahudumia watoto wake badala ya mtindo wa maisha waliokuwa wameuzoea wa kutaka kumhudumia Mwenyezi Mungu. Huu ndio mwelekeo wa maisha anaoutekeleza Kristo Yesu kuanzia hata wakati huu, kwa kuwaombea na kuwahudumia, hiki ndicho kielelezo cha furaha na uzima wa milele. Waamini wasiwe na wasi wasi wala woga wa kukutana kwa mara ya mwisho na Mwenyezi Mungu, Baba wa milele, mwingi wa huruma na mapendo, anayewakirimia matumaini na kuwahimiza kuchuchumilia toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, ili kujenga na kudumisha ulimwengu unaosimikwa katika haki na udugu!

Papa: Kesheni
11 August 2019, 09:58