Baba Mtakatifu Francisko anasema, moto uliowashwa na Kristo Yesu ni upendo kwa Mwenyezi Mungu na jirani; moto unaotenganisha wema na ubaya ili kuambata utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, moto uliowashwa na Kristo Yesu ni upendo kwa Mwenyezi Mungu na jirani; moto unaotenganisha wema na ubaya ili kuambata utakatifu wa maisha. 

Papa Francisko: Moto wa Yesu ni upendo kwa Mungu na jirani

Moto uliowashwa na Yesu: Ni upendo unaokita mizizi yake katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Upendo wa kweli ndio kielelezo na utambulisho wa wafuasi wa Kristo Yesu. Huu ni upendo ambao umewashwa na Roho Mtakatifu kati ya watu wa Mataifa na wala hauna kizuizi hata chembe ni upendo unaotambaa na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 18 Agosti 2019 amekita mawazo yake kwenye Injili ya Jumapili ya XX ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, ambamo Kristo Yesu anazungumzia kuhusu ujio wake na moto alioutupa hapa duniani, na ikiwa kama moto huu umekwisha washwa, nini atakalo zaidi? Hii ni sehemu muhimu sana ya angalisho linalotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake, akiwataka kufanya maamuzi magumu katika maisha. Moto uliotupwa na Kristo Yesu duniani, unalenga kuwasaidia Wakristo kusimama kidete kwa kuondokana na uchovu wa imani, tabia ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine na hata kushindwa kupokea moto wa upendo wa Mungu ambao umewashwa ndani mwao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo pamoja na Kipaimara. Waamini wakumbuke kwamba, ni Roho Mtakatifu anayewawezesha kukoleza upendo wao kwa Mungu Baba Mwenyezi pamoja na jirani zao.

Wakristo wote wanaye Roho Mtakatifu ndani mwao! Katika sehemu hii ya Injili, Kristo Yesu anawafunulia rafiki zake, ile ari, hamu na shauku ya kuwasha moto wa upendo wa Mungu Baba; upendo unaotakasa, unaoganga, kuponya na kuokoa. Huu ni upendo unaokita mizizi yake katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Upendo wa kweli ndio kielelezo na utambulisho wa wafuasi wa Kristo Yesu. Huu ni upendo ambao umewashwa na Roho Mtakatifu kati ya watu wa Mataifa na wala hauna kizuizi hata chembe ni upendo unaotambaa na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hii ndiyo hali ambayo imeonekana tangu mwanzo wa Kanisa. Ushuhuda wa Injili umetambaa na kusambaa kama “moto wa kifusi” kwa kubomolea mbali vizingiti vya utengano kati ya watu wa Mataifa mbali mbali, makundi ya kijamii na hali zao za kijamii. Ushuhuda wa Injili, unachoma na kuunguza tabia ya kujiona na kujikweza, inakuza na kupyaisha upendo unaowaambata wote, lakini kipaumbele cha kwanza kikiwa ni kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hao ndio “akina yakhe, pangu pakavu, tafadhali tia mchuzi”.

Wakristo wanahimizwa kuambata na kuukumbatia moto wa Injili ya Kristo unaowataka  kumwabudu Mwenyezi Mungu na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Mwenyezi Mungu anawataka waja wake, kujifunza Sala ya Kumwabudu na hivyo kuhakikisha kwamba, wanaimwilisha sala hii katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Pili, wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza waamini mbali mbali ambao katika kipindi hiki cha likizo ya kipindi cha kiangazi Barani Ulaya, bado wako wanaendelea kutoa huduma ya upendo kwa ajili ya wagonjwa, maskini na walemavu. Waamini wanahimizwa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kusoma alama za nyakati, tayari kusimama kidete, kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha maskini katika ulimwengu mamboleo kwa njia huduma ya upendo. Kwa kumwabudu Mwenyezi Mungu na huduma ya upendo kwa jirani, Injili inajipambanua kuwa ni moto unao okoa, moto unaokita mizizi yake katika toba na wongofu wa ndani, ili kuleta mabadiliko ya dhati kwa kila mwamini.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anaendelea kukazia kwamba, hakuja duniani ili kuleta amani, bali mafarakano yanayotekelezwa kwa moto wa Injili. Huu ni moto unaotenganisha uzuri, wema na ubaya wa moyo; haki na ukosefu wa haki. Yesu amekuja kuleta “mafarakano” yanayopania kufanya maboresho makubwa katika maisha ya wafuasi wake kwa kuondokana na ndoto ya kutaka kuchanganya mambo matakatifu, wakati huo huo, wakiendelea kumezwa na malimwengu, kiasi hata cha kuwadharau na kuwanyanyasa hata jirani zao. Ni moto unaotenganisha imani katika Kristo Yesu na Kanisa lake, na ile imani potofu inayofumbatwa katika mambo ya kishirikina: kwa kupiga ramli chonganishi pamoja na kuvikwa hirizi kama kinga ya maisha! Baba Mtakatifu anasema, yote haya ni ubatili mtupu ni kinyume kabisa cha imani kwa Mwenyezi Mungu, Kristo Yesu na Kanisa lake. Moto wa Injili unawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili, kiasi hata cha kuwa tayari kulipa gharama ya kuwa Mkristo!

Ni rahisi sana kwa mwamini kujiita “Mkristo”, lakini yataka moyo sana kuwa “Mkristo wa kweli” katika uhalisia wa maisha; kwa kushuhudia ukweli wa Injili, ambao kimsingi ni upendo kwa Mungu na jirani. Mwishoni wa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili awasaidie kutakasa nyoyo zao kwa moto uliowashwa na Kristo Yesu; kwa kuumwilisha katika uhalisia wa maisha sanjari na kuhakikisha kwamba, wanafanya maamuzi maalum na yenye ujasiri.

Papa: Moto wa upendo
18 August 2019, 10:18