Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amebariki Rozari Takatifu 6, 000 zitakazo pelekwa nchini Siria kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu Francisko amebariki Rozari Takatifu 6, 000 zitakazo pelekwa nchini Siria kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Salini Rozari Takatifu kuombea amani nchini Siria

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 15 Agosti, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, amebariki Rozari Takatifu 6, 000 zilizotengenezwa kwa ajili ya waamini nchini Siria na Watawa wa Shirika la Wakarmeli wanaotekeleza utume wao mjini Bethlehemu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia ya ukombozi inayowasaidia waamini kwa njia ya Bikira Maria, kumfahamu zaidi Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Ni sala inayowawezesha waamini kukimbilia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, kwa ajili ya kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hii ni sala ya waamini wa kawaida inayowahakikishia uwepo endelevu wa Bikira Maria katika safari ya maisha yao hapa duniani. Waamini wanakumbushwa umuhimu wa kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea: toba na wongofu wa ndani; amani na utakatifu wa maisha.

Injili ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Mama Kanisa! Kimsingi, Kanisa linaitwa na kutumwa kuonesha Uso wa upendo na huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, ili kuwaganga na kuwahudumia kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, watu waliopondeka moyo na kukata tamaa ya maisha! Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 15 Agosti, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, amebariki Rozari Takatifu 6, 000 zilizotengenezwa kwa ajili ya waamini nchini Siria na Watawa wa Shirika la Wakarmeli wanaotekeleza utume wao mjini Bethlehemu.

Baba Mtakatifu anasema, amependa kubariki Rozari hizi, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho na baadaye, zitapelekwa kwenye Jumuiya za Kikristo, ili waamini waweze kugawiwa, kielelezo makini cha uwepo wa karibu na endelevu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu wanaoendelea kuteseka kwa vita na kinzani za kijamii huko nchini Siria. Walengwa wakuu ni zile familia ambazo zimewapoteza ndugu, jamaa na marafiki kutokana na vita huko Mashariki ya Kati. Sala inayomwilishwa katika imani tendaji ina nguvu za ajabu sana anasema Baba Mtakatifu na anaendelea kuwahimiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati na Ulimwenguni katika ujumla wake. Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji linaendelea kuunga mkono jitihada za Mama Kanisa katika kuwahudumia watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha uwepo wake wa karibu na mshikamano kwa njia ya sala kwa watu wote walioathirika vibaya kutokana na mvua kubwa za kipindi cha Monsoon huko Barani Asia na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu, mali na miundo mbinu mbali mbali. Baba Mtakatifu anawaombea wale wote waliofariki dunia, ili waweze kupata faraja, amani na mwanga wa milele uweze wa kuwaangazia. Anawakumbuka na kuwafariji watu wote wasiokuwa na makazi maalum baada ya nyumba zao kubomolewa na mafuriko. Kwa watu hawa, Baba Mtakatifu anawaombea kwa Mwenyezi Mungu ili awatie shime na kuwapatia nguvu wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu.

Papa: Rozari

 

15 August 2019, 15:49