Tafuta

Vatican News
Nia za Baba Mtakatifu Francisko: Nia Mwezi Agosti 2019: Familia kama shule za maendeleo ya binadamu. Nia za Baba Mtakatifu Francisko: Nia Mwezi Agosti 2019: Familia kama shule za maendeleo ya binadamu.  (ANSA)

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Agosti 2019: Familia shule za maendeleo ya binadamu

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2019 anajielekeza zaidi katika familia kama shule za maendeleo ya binadamu. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anapenda kuwauliza watu wa Mungu, Je, aina gani ya dunia wanayotaka kuiacha kwa siku za usoni? Jengeni familia imara na thabiti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa katika maisha na utume wake anapenda kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mpango wa Mungu kwa mwanadamu sanjari na Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia.

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2019 anajielekeza zaidi katika familia kama shule za maendeleo ya binadamu. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anapenda kuwauliza watu wa Mungu, Je, aina gani ya dunia wanayotaka kuiacha kwa siku za usoni? Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanaiacha dunia na familia imara na thabiti kama zawadi na tunu msingi ya maisha. Kwa njia hii, anawaalika kuzijali na kuzithamini familia zao kwa sababu ni shule halisi kwa siku za usoni; ni nafasi ya uhuru na kitovu cha ubinadamu. Waamini wanahimizwa kutenga nafasi ya pekee kwenye familia zao kwa ajili ya kukuza na kudumisha ari na moyo wa sala binafsi na sala za kifamilia.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, waendelee kuziombea familia zao, ili kwa njia ya maisha yao ya sala na upendo, familia ziendelee kuwa ni shule dhahiri na halisi za maendeleo ya binadamu. Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, asilimia 16% ya familia zote katika Umoja wa Ulaya zinaundwa na mzazi mmoja mmoja, yaani, watoto wanaishi na mzazi mmoja tu. Nchini Marekani, takwimu zinaonesha kwamba, 44% ya wazazi wote ni wale waliofunga ndoa, lakini pia kumekuwepo na ongezeko la asilimia 20% ya watu wanaoishi peke yao bila kufunga ndoa na asilimia 8% ni wale wanaoishi uchumba sugu! Takwimu za kimataifa zinaonesha kwamba, Colombia inaongoza duniani kwa kuwa na watu wanaoishi uchumba sugu 35% ya wananchi wote wa Colombia, huko Amerika ya Kusini. Kimsingi, kuna watoto ambao ni asilimia 27% wanaoishi katika familia ya mzazi mmoja mmoja.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunga kibwebwe kwa ajili ya kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa sababu hizi ni shule dhahiri za maisha ya binadamu kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anawataka wanafamilia kujenga na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kushirikishana: furaha, machungu na wasi wasi zinazowanyima usingizi na furaha ya maisha. Wanandoa na familia wawe wepesi kutoa na kupokea msamaha, kwa sababu ni katika kuta za familia, watu wanajifunza kupenda na kupendwa; kusamehe na kusahau. Vinginevyo anasema Baba Mtakatifu familia zitageuka kuwa ni “kichaka” cha ubinafsi unaochakachua ule umoja, upendo na mafungamano ya kifamilia, kiasi cha kugeuza familia kuwa ni uringo wa mapambano, uadui na upweke katika maisha ya watu! Kila familia ina utofauti wake, kwani ina mazuri, magumu na changamoto zake.

Kumbe, familia zinapaswa kukua na kukomaa; ili ziweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, kama njia ya kuganga na kuponya madonda yanayojitokeza katika uhalisia wa maisha. Familia zijitahidi kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kwa kusaidiana na kuhudumiana. Mambo msingi yanayounganisha familia anasema Baba Mtakatifu Francisko ni maisha ya sala na upendo wa dhati, chachu muhimu katika kukuza tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kijamii. Kwa hakika, familia ni shule dhahiri katika ukuaji wa kibinadamu.

Papa: Nia Agosti
02 August 2019, 14:36