Tafuta

Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba, Edith Stein ni shuhuda wa imani na mwanamke wa shoka aliyejibidisha kumtafuta Mwenyezi Mungu katika uaminifu na upendo! Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba, Edith Stein ni shuhuda wa imani na mwanamke wa shoka aliyejibidisha kumtafuta Mwenyezi Mungu katika uaminifu na upendo! 

Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba, Shuhuda wa wongofu & imani kwa Kristo Yesu!

Papa Francisko anasema, Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba, maarufu kama Edith Stein, Bikira na Shahidi; Msimamizi mwenza wa Bara la Ulaya. Shuhuda wa imani na mwanamke wa shoka, aliyejibidisha kumtafuta Mwenyezi Mungu katika uaminifu na upendo. Ni shuhuda wa udugu kati ya Wayahudi na Wakristo na daraja makini la majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini hizi mbili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam na matashi mema kwa waamini na mahujaji waliohudhuria Katekesi yake, Jumatano, tarehe 7 Agosti 2019, amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 8 Agosti 2018, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Dominico de Guzman, Mwanzilishi wa Shirika la Wadominican, maarufu sana kwa kuhubiri. Mtakatifu Dominico alikuwa mtumishi mwaminifu wa Kristo na Kanisa lake, mfano bora wa kuigwa na waamini, na hasa zaidi, wale wote wanaoitwa kwa jina la Dominico. Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, tarehe 9 Agosti 2019, Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba, maarufu kama Edith Stein, Bikira na Shahidi; Msimamizi mwenza wa Bara la Ulaya. Shuhuda wa imani na mwanamke wa shoka, aliyejibidisha kumtafuta Mwenyezi Mungu katika uaminifu na upendo.

Ni shuhuda wa udugu kati ya Wayahudi na Wakristo na daraja makini la majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini hizi mbili. Baba Mtakatifu anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuangalia maamuzi yake yanayofumbata ujasiri; yakamwilishwa katika wongofu kwa Kristo Yesu! Ni mfano bora wa kuigwa dhidi ya tabia na itikadi zinazopandikiza mbegu za chuki na uhasama kati ya watu. Baba Mtakatifu anamwomba, Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba, aliombee Bara la Ulaya ili lisikumbwe na ubaridi, Mwenyezi Mungu apewe sifa na mwanadamu na akombolewe! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni watu wa shukrani kwa wema na ukarimu wanaopata kutoka kwa Mwenyezi Mungu pengine hata bila mastahili yao. Wawe ni mashuhuda na vyombo vya ukaribu wa Mungu kwa watu wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha.

Waamini wawe na kumbu kumbu hai ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu aweze kuwakirimia uwezo wa kushuhudia yote haya kwa sifa ya Mwenyezi Mungu na huduma makini kwa jirani! Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aendelee kuwa ni alama ya imani na matumaini kati ya watu wa Mungu, dhamana inayopaswa pia kutekelezwa na waamini wenyewe! Waamini waendelee kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili Ufalme wake ufike na hatimaye, aweze kuwaponya na magonjwa ya kiroho na kimwili. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa maisha ya sala; kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Wawe ni nguvu ya faraja kwa njia ya uwepo na huduma yao kwa jirani na wahitaji zaidi. Waendelee kutafakari kazi ya uumbaji, kwa kumtukuza, kumsifu na kumshangilia Mwenyezi Mungu kwa hekima na upendo wake kwa binadamu.

Papa: Watakatifu
07 August 2019, 15:03