Baba Mtakatifu Francisko, asikitishwa sana na mauaji ya kinyama nchini Marekani. Baba Mtakatifu Francisko, asikitishwa sana na mauaji ya kinyama nchini Marekani. 

Papa Francisko asikitikishwa na mauaji ya kinyama nchini Marekani

Taarifa kutoka Marekani zinaonesha kwamba, mauaji ya El Paso huko Texas yamepelekea watu 20 kupoteza maisha na wengine 26 kujeruhiwa. Inasadikiwa kwamba mauaji haya yanatokana na chuki za ubaguzi wa rangi. Ohio, watu 9 wamefariki dunia na wengine 27 wamejeruhiwa na California watu 3 waliuwawa. Wapenda amani wanasema, haya ndiyo madhara ya biashara ya silaha duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 4 Agosti 2019 ameonesha masikitiko yake makuu kutokana na mauaji ya kinyama yaliyotokea hivi karibuni huko Texas, California na Ohio, nchini Marekani na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine kupata majeraha ya kudumu. Wote hawa wamekumbukwa na Baba Mtakatifu kwa sala, iliyoungwa mkono na waamini pamoja na mahujaji waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Taarifa kutoka Marekani zinaonesha kwamba, mauaji ya El Paso huko Texas yamepelekea watu 20 kupoteza maisha na wengine 26 kujeruhiwa vibaya. Inasadikiwa kwamba mauaji haya yanatokana na chuki za ubaguzi wa rangi.

Huko Ohio, watu 9 wamefariki dunia na wengine 27 wamejeruhiwa na California watu 3 waliuwawa. Wachunguzi wa mambo wanasema haya ndiyo madhara ya biashara ya silaha duniani! Kuhusiana na mauaji ya kinyama yaliyotokea Jumamosi, tarehe 3 Agosti 2019 kwenye duka kubwa la “Cielo Vista Mall in El Paso”, taarifa ya Jimbo kuu la San Antonio inaonesha kwamba, kuna watu 20 waliofariki dunia na wengine 19 wamejeruhiwa vibaya kwa risasi na kwamba, wanaendelea kupata matibabu hospitalini. Askofu mkuu Gustavo Garcia Siller kwa niaba ya familia ya Mungu Jimbo kuu la San Antonio, Marekani, anapenda kuchukua fursa hii kuvishukuru vyombo vya ulinzi na usalama pamoja wale wote waliojisadaka kwa ajili ya huduma ya kwanza kwa waathirika.

Askofu mkuu Gustavo Garcia Siller anawataka watu wa Mungu nchini Amerika kujizatiti katika kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mauaji kama haya yasijirudie tena, kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka Mungu. Wakati huo huo, Kardinali Daniel DiNardo, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki anasema, umefika wakati kwa Serikali ya Marekani kuhakikisha kwamba, inaratibu umiliki wa silaha, ili zisiendelee kuwa ni chanzo cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Mauaji haya ni ugaidi wa ndani unaopaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo!

Papa: Mauaji Marekani
04 August 2019, 09:53