Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko afanya marekebisho kwenye Katiba ya Benki Kuu ya Vatican IOR kwa kukazia: Kanuni maadili, ukweli na uwazi katika matumizi ya fedha za Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko afanya marekebisho kwenye Katiba ya Benki Kuu ya Vatican IOR kwa kukazia: Kanuni maadili, ukweli na uwazi katika matumizi ya fedha za Kanisa. 

Baba Mtakatifu Francisko afanya marekebisho kwenye Katiba ya Benki ya Vatican, IOR

Marekebisho ya Katiba ya Benki Kuu ya Vatican, IOR; Mkaguzi wa nje; Muundo wa Benki chini ya Tume ya Makardinali; Baraza la Washauri, Askofu, Uongozi, sheria, kanuni na taratibu za kutunza taarifa za mikutano ya Benki Kuu ya Vatican. Kanisa halina budi kuendelea kujikita katika misingi ya ukweli, uwazi, uadilifu na maadili katika matumizi ya fedha na mali ya Kanisa kwa uinjilishaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Benki Kuu ya Vatican, IOR,  iliyoanzishwa kunako mwaka 1942 na Papa Pio XII, inajihusisha na huduma kwa mashirika ya kitawa, kazi za kitume na shughuli za uinjilishaji unaofanywa na Kanisa la Kiulimwengu. Papa Pio XII akafanya mabadiliko kwenye Katiba yake kunako mwaka 1944 na kunako mwaka 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II akarekebisha Katiba hii na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 10 Agosti 2019 amefanya marekebisho makubwa kuhusu Katiba ya Benki Kuu ya Vatican, IOR, kwa kusoma alama za nyakati. Katika marekebisho ya Katiba hayo, Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu lengo la Benki Kuu ya Vatican, IOR; Mkaguzi wa nje; Muundo wa Benki chini ya Tume ya Makardinali; Baraza la Washauri, Askofu, Uongozi, sheria, kanuni na taratibu za kutunza taarifa za mikutano ya Benki Kuu ya Vatican.  Kanisa halina budi kuendelea kujikita katika misingi ya ukweli, uwazi, uadilifu na maadili katika matumizi ya fedha na mali ya Kanisa ambayo kimsingi ni kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kanuni ya ukweli, uwazi, uadilifu, weledi na maadili ni mambo msingi sana katika mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu na hata utakatishaji wa fedha haramu. Benki Kuu ya Vatican kwa marekebisho ya Katiba hii, Baba Mtakatifu anapania kuona kwamba, Benki ya Vatican inatoa huduma ya shughuli za Kikanisa pamoja na matendo ya huruma. Mabadiliko msingi ni uwepo wa Mkaguzi wa Benki kutoka nje atakayeteuliwa na Baraza la Washauri na kupitishwa na Tume ya Makardinali. Kisheria ndiye atakayehusika na jukumu la kupitisha Bajeti ya Benki Kuu ya Vatican baada ya kupitia na kukagua mahesababu yoye ya Benki. Katika muundo wa Benki Kuu ya Vatican, kuna Tume ya Makardinali inayoundwa na Makardinali watano wanaoteuliwa na Baba Mtakatifu na watatekeleza wajibu huu kwa muda wa miaka mitano tu. Kuna Baraza la Washauri wa Benki Kuu ya Vatican litakaloundwa na wajumbe saba watakaoteuliwa na Tume ya Makardinali na watatekeleza utume wao kwa muda wa miaka mitano. Rais wa Baraza la Washauri wa Benki kuu ya Vatican ndiye mwakilishi wa Benki kuu ya Vatican kisheria.

Askofu atateuliwa na Tume ya Makardinali, ili kusimamia: sheria, kanuni na maadili ya Kanisa Katoliki. Atakuwa ni mhifadhi mkuu wa “Nyaraka za Tume ya Makardinali". Mkurugenzi mkuu wa Benki Kuu ya Vatican atakayetueliwa ataendelea kuwa madarakani hadi atakapotimiza miaka 70 ya kuzaliwa. Iwapo kutakuwa na pengo lolote litazibwa kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Benki. Wafanyakazi wa Benki kuu ya Vatican hawataruhusiwa kufanya kazi nyingine yoyote iwe ndani au nje ya Vatican. Sheria, Taratibu na Kanuni za Kanisa zitafuatwa kikamilifu. Benki Kuu ya Vatican itaendelea kuwekeza katika huduma ya kifedha kwa ajili ya kupambana na umaskini, ujinga na maradhi duniani. Benki itajikita katika kugharimia shughuli za kimisionari. Benki kuu ya Vatican kadiri ya taarifa ya Mwaka 2018 inaoesha kwamba, ina jumla ya wateja 14, 953. Mashirika ya Kitawa ni asilimia 53%, Mabaraza la Kipapa, Sekretarieti kuu pamoja na Balozi za Vatican ni asilimia 12%; Mabaraza ya Maaskofu, Majimbo na Parokia ni asilimia 9%.

Taasisi zenye haki za Sheria za Kanisa ni asilimia 8%, Wakleri ni asilimia 8%. Wafanyakazi na wastaafu ni asilimia 8% na taasisi nyinginezo ni asilimia 2%. Mabadiliko yanayoendelea kufanyika mjini Vatican, hayana budi kuendelezwa na kutekelezwa hata katika Taasisi za fedha zinazoendeshwa na Makanisa mahalia na taasisi zote zinazosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa. Hizi ndizo cheche za mabadiliko zinazoletwa na Baba Mtakatifu Francisko, wanasema Makardinali, "hapa hakuna kulala hadi kieleweke"!

Papa: IOR
10 August 2019, 14:51