Papa Francisko: Mahojiano Maalum na "La Stampa- Vatican Insider": Utambulisho wa Umoja wa Ulaya; Wakimbizi & Wahamiaji; Sinodi & Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Papa Francisko: Mahojiano Maalum na "La Stampa- Vatican Insider": Utambulisho wa Umoja wa Ulaya; Wakimbizi & Wahamiaji; Sinodi & Athari za Mabadiliko ya Tabianchi 

Papa Francisko: Mahojiano na "La Stampa": Umoja wa Ulaya, Sinodi, Wakimbizi & Mazingira

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Bwana Domenico Agasso, mwandishi wa Gazeti “La Stampa – Vatican Insider” amegusia kuhusu: Utambulisho wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya; Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia pamoja na Athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utaifa wa kupindukia utasababisha maafa makubwa duniani, ikiwa ni pamoja na vita, jambo la msingi ni Jumuiya ya Ulaya kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Siasa safi na makini inayofumbwa katika ubunifu, hekima na busara ni kwa ajili ya huduma ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Hii ni changamoto ya kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia: utu, heshima na haki zao msingi. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto kubwa inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kutokana na athari zake na kwamba, waathirika zaidi ni maskini na watu wa Mungu kutoka katika nchi changa zaidi duniani! Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani".

Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali kuhusu: haki jamii, malezi awali na endelevu, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Sinodi hii itajikita zaidi katika mchakato wa uinjilishaji Ukanda wa Amazonia. Haya ni kati ya mambo mazito yaliyozungumzwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Bwana Domenico Agasso, mwandishi wa Gazeti  “La Stampa – Vatican Insider”. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa nchi wanachama wa Umoja wa Jumuiya ya Ulaya kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, wanautegemeza umoja huu, ili usije kusambaratishwa na watu wenye misimamo mikali kuhusu utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko pamoja na watu wanaojitafutia umaarufu. Umoja wa Ulaya hauna budi kupyaishwa ili uweze kusonga mbele bila ya kuvurugwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Baba Mtakatifu anasema, mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na waasisi wa Umoja wa Ulaya hapo tarehe 25 Machi 1957, walijiwekea sera na mikakati ya kukabiliana na changamoto mamboleo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, lakini hasa kwa kuwekeza katika ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu. Walitaka kulinda na kudumisha uhai, udugu na haki, kama chachu muhimu sana ya mabadiliko Barani Ulaya, baada ya patashika nguo kuchanika wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Waasisi wa Umoja wa Ulaya walikazia kwa namna ya pekee zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya. Jumuiya ya Ulaya itaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama itaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Ulaya.

Hii ilikuwa ni changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengenano, ili kuokoa maisha ya familia zilizokuwa zinaogelea katika dimbwi la umaskini, vita na mipasuko ya kijamii, inayoendelea kushuhudiwa hata leo hii. Matatizo na changamoto za uongozi ndani ya Jumuiya ya Ulaya yanapaswa kupewa ufumbuzi wa kudumu. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha matumaini yake kwa Ursula Von Der Layen aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa Rais wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Kimsingi wanawake wanao uwezo wa kuunganisha na kwa wakati huu, Mama Ursula anaonekana kuwa na uwezo wa kuendeleza ndoto ya waasisi wa Umoja wa Ulaya. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila mtu ni muhimu sana katika ulimwengu huu na kwamba, kila mtu anao utambulisho wake. Utambulisho wa Jumuiya ya Ulaya ni tunu ambazo zinapaswa kukuzwa na kuendelezwa, kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii Barani Ulaya.

Ili kufanya majadiliano ya kiekumene na waamini wa Kanisa la Kiorthodox, Wakatoliki wanapaswa kutambua kwanza utambulisho wao, ili kuweza kuingizwa katika mafungamano haya. Tatizo kubwa ni pale ambapo watu wanapenda kukuza mambo, kiasi cha kufungia utambulisho wao katika “makasha ya kihistoria”. Ikumbukwe kwamba, utambulisho wa watu ni amana na utajiri unaofumbatwa katika misingi ya kitamaduni, kitaifa na kisanii. Kila taifa lina utambulisho na vipaumbele vyake, vinavyopaswa kufungamanishwa katika Umoja wa Ulaya kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuweza kupokea kutoka katika nchi nyingine mambo makubwa zaidi. Baba Mtakatifu anasema, anatishika sana na dhana ya utaifa na tabia ya watu kujitafutia umaarufu wa kisiasa usiokuwa na mashiko wala mvuto hata kidogo kama ilivyokuwa kwa Hitler kunako mwaka 1934. Katika kipindi hiki watu walimezwa na ubinafsi kiasi cha kujifikiria wao binafsi na kuwafungia wengine malango ya matumaini katika maisha.

Hali hii ikadhohofisha mahusiano na mafungamano na mataifa mengine na matokeo yake ni maafa makubwa ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna umati mkubwa wa watu wanaokimbia nchi zao kutokana na vita, njaa na umaskini; hawa ni watu wanaopaswa kuoneshwa mshikamano wa upendo ili kuandika tena ukurasa wa matumaini kwa ajili yao wenyewe, pamoja na familia zao. Kumbe, wote wanapaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa amani unaotoa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hizi ni tunu msingi zilizobainishwa na waasisi wa Umoja wa Ulaya, lakini ikumbukwe kwamba, mizizi ya tunu hizi ni utamaduni na Mapokeo ya Kikristo yanayozingatia kwa namna ya pekee kabisa: Uhai, utu, heshima, uhuru na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anasema kwa msisitizo kwamba, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha kwa kuzingatia hali halisi ya taifa husika pamoja na uwezo wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji hawa.

Kipaji cha ubunifu kinaweza kutumika hapa, kiasi kwamba, wahamiaji na wakimbizi wakasaidia kuziba pengo la uhaba mkubwa wa nguvu kazi katika sekta ya kilimo! Kuna baadhi ya nchi Barani Ulaya ambazo zina idadi ndogo sana ya nguvu kazi kutokana na ukweli kwamba, kuna idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya. Nguvu kazi hii inaweza kuwa ni chachu ya kufufua mchakato wa ukuaji wa uchumi Barani Ulaya. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaibua mbinu mkakati wa kuzisaidia kiuchumi nchi ambazo zinazalisha wimbi kubwa la wakimbizi duniani, pamoja na kusaidia kutoa ufumbuzi wa kudumu wa mambo yanayopelekea watu wengi kuzikimbia nchi zao. Bara la Afrika linahitaji kuungwa mkono katika mapambano dhidi ya umaskini, baa la njaa pamoja na vita. Changamoto kubwa anasema Baba Mtakatifu ni biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuivalia njuga changamoto hii inayoendelea kufikirisha sana!

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali kuhusu: haki jamii, malezi awali na endelevu, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Sinodi hii itajikita zaidi katika mchakato wa uinjilishaji Ukanda wa Amazonia. Sinodi hii ni matunda ya changamoto changamani iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya ekolojia ya mazingira, uchumi na jamii, mambo ambayo hayawezi kutenganishwa kama ilivyo pia hata katika mambo ya kiakili, maisha ya kiroho, kisiasa na kiuchumi kwani yana athari zake katika mchakato mzima wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. 

Takwimu za Jumuiya ya Kimataifa zinaonesha kwamba, tangu tarehe 29 Julai 2019 mwanadamu “amekwisha komba rasilimali zote zilizozalishwa katika kipindi cha mwaka 2018”. Kuna hatari kubwa inayoendelea kujitokeza kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuna ongezeko kubwa la kina cha bahari, uchafuzi wa mazingira unaofanywa na takataka za plastiki ambazo kwa sasa ni tishio kwa viumbe hai; kuna ongezeko kubwa la Jangwa pamoja na ukame wa kutisha bila kusahau mafuriko na maporomoko ya ardhi yanayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yanapania pamoja na mambo mengine, kuganga na kuponya uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na hivyo kuanza mchakato wa njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani. Hapa Mama Kanisa anakazia kuhusu: Unabii wa Kanisa sanjari na Maendeleo fungamani ya binadamu, mambo ambayo ni sawa na chanda na pete, kwani yanategemeana na kukamilishana.

Mama Kanisa anataka kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kusimama kidete katika shughuli za kichungaji; utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kuhimiza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hili ni tukio la Kikanisa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Dhana ya Kanisa kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa watu waliooa yaani kwa lugha la Kisheria “Viri probati” si mada itakayopewa uzito sana katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, bali ni sehemu ya mada za kutendea kazi kwa Mababa wa Sinodi. Ukanda wa Amazonia una umuhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu duniani kote. Kumbe, kutoweka kwa rasilimali zilizoko Ukanda wa Amazonia ni sawa na kuitumbukiza dunia katika maafa makubwa!

Rushwa, ufisadi wa mali ya umma; sera na ukoloni wa kiitikadi pamoja na uchafuzi wa mazingira ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuwekeza katika maisha na utume kwa vijana, kwa kuwajengea imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto changamani inayoendelea kutolewa na mitandao ya vijana kimataifa kama alivyofanya Greta Thunberg kwani wanatambua kwamba, leo na kesho ya ulimwengu iko mikononi mwa vijana wa kizazi kipya! Kumbe hapa kuna haja ya kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira kwa kuanzia na mambo madogo madogo, lakini yenye athari kubwa katika utunzaji bora wa mazingira!

Papa: Mahojiano
09 August 2019, 14:30