Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wajumbe wa Kongamano la kimisionari kitaifa nchini Indonesia kutafakari kuhusu: Kubatizwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wajumbe wa Kongamano la kimisionari kitaifa nchini Indonesia kutafakari kuhusu: Kubatizwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo! 

Ujumbe wa Papa Francisko kwenye Kongamano la Kimisionari Kitaifa

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa njia ya Ubatizo, waamini wanampokea Roho Mtakatifu; wanapokea pia amana na utajiri wa Neno la Mungu linalobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Utajiri huu, uwahamasishe waamini kuwa na ari na moyo mkuu wa kutaka kuwatangazia na kuwashuhudia wengine. Waamini wakuze na kudumisha ari na moyo wa kimisionari, kielelezo cha Ubatizo wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”.  Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni wakati kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa.

Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma na upendo wa Mungu hadi miisho ya dunia! Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili, ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu, ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne, ni huduma ya Injili ya upendo kama kielelezo cha imani tendaji!

Familia ya Mungu nchini Indonesia, kuanzia tarehe 1 Agosti hadi tarehe 4 Agosti 2019 inaadhimisha Kongamano la Kimisionari Kitaifa linaloongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, amewatumia ujumbe kwa njia ya video, washiriki wote, kwa kukazia umuhimu wa kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”. Kwa njia ya Ubatizo, waamini wanampokea Roho Mtakatifu; wanapokea pia amana na utajiri wa Neno la Mungu linalobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Utajiri huu, uwahamasishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na ari na moyo mkuu wa kutaka kuwatangazia na kuwashuhudia wengine ile furaha ya Injili.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kubatizwa na kutumwa ndiyo mambo msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi na wajumbe wa Kongamano la Kimisionari Kitaifa nchini Indonesia. Washiriki wanapaswa kujiuliza maswali magumu, Je, mimi ninaishi namna gani Ubatizo wangu? Je, katika maisha yangu binafsi nimejitahidi kuwa ni chachu ya Injili ili kuyachachua malimwengu katika mwanga wa Injili? Mmebatizwa na kutumwa: hii ni dhamana na utume ambao waamini wanapaswa kuukumbuka daima. Baba Mtakatifu anasema, Mkristo ni mwamini ambaye daima anasonga mbele, ni mwiko kurejea tena nyuma; vinginevyo ni kupingana na kauli hii.

Kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu ndiyo dhamana inayotekelezwa na yule aliyetumwa. Waamini watambue kwamba, wanaongozwa na Roho Mtakatifu anayewatia shime ya kuendelea mbele na mchakato wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Baba Mtakatifu anawataka Wakristo nchini Indonesia kutambua kwamba, wamebatizwa na kutumwa, kumbe, wanapaswa kuwa na ujasiri wa kusonga mbele daima pasi na kukata tamaa. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuombea tukio hili, ili kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, nyota ya uinjilishaji, aweze kuwalinda na kuwasimamia ili waweze kusonga mbele. Anawaalika pia waamini kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu amehitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa kuwapatia baraka zake za kitume!

Papa: Indonesia
01 August 2019, 14:58