Vatican News
Papa Francisko asema, maajabu na ishara zilizotendwa na Mitume wa Yesu zilikuwa ni ufunuo wa Umungu wa Kristo. Papa Francisko asema, maajabu na ishara zilizotendwa na Mitume wa Yesu zilikuwa ni ufunuo wa Umungu wa Kristo.  (Vatican Media )

Papa Francisko: Maajabu na ishara za Mitume ni ufunuo wa Umungu wa Kristo

Maandiko Matakatifu yanasema, Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilidumu katika fundisho la Mitume, na katika ushirika na katika kuumega mkate na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na Mitume katika Jina la Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Maajabu na ishara nyingi zilizotendwa na Mitume wa Yesu zilikuwa ni ufunuo wa Umungu wa Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuenea kwa Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia ni matunda ya Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya maisha mapya. Mitume waliendelea kuwa watiifu, wakawa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali pamoja nao wanawake, na Mariam Mama yake Yesu. Walikuwa wanajiandaa kupokea zawadi na nguvu ya Mungu kutoka juu, ili kuimarisha umoja na mshikamano kati yao na huo ukawa ni mwanzo wa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo! Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 7 Agosti 2019, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI ulioko mjini Vatican ameendeleza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume. Hii ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji.

Kiini cha uinjilishaji ni Neno la Mungu wahusika wakuu ni Roho Mtakatifu sanjari na Ushuhuda wa Mitume. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilidumu katika fundisho la Mitume, na katika ushirika na katika kuumega mkate na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na Mitume katika Jina la Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Maajabu na ishara nyingi zilizotendwa na Mitume wa Yesu zilikuwa ni ufunuo wa Umungu wa Kristo. Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, amefafanua kwamba, muujiza wa kwanza kabisa kutendwa na Mitume Petro na Yohane pale kwenye mlango wa Hekalu uitwao Mzuri, kwa kumponya yule kiwete toka tumboni mwa mama yake ulikuwa na lengo la kimisionari kwa kupyaisha imani, uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya sala ambayo bado yalikuwa yamefungamanishwa na imani ya Waisraeli. Hata Wakristo wa Kanisa la Mwanzo waliendelea kusali Hekaluni.

Mwinjili Luka anakazia muda wa sala kwamba, ulikuwa ni saa 9 Alasiri, muda wa kutolea sadaka kwa Mwenyezi Mungu. Itakumbukwa kwamba, hata Kristo Yesu alikata roho ilipotimia saa 9 Alasiri, akayamimina maisha yake kama sadaka ya Agano Jipya na la milele. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kadiri ya Sheria za Musa mtu ambaye alikuwa na ulemavu hakuruhusiwa kutoa sadaka kwani ulemavu katika Agano la Kale ulihesabiwa kuwa ni kielelezo cha uwepo wa dhambi. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa yule mtu aliyezaliwa kipofu tangu tumboni mwa mama yake. Watu wakamuuliza Kristo Yesu ni nani aliyekuwa ametenda dhambi kiasi cha mtu yule kuzaliwa kipofu. Ulemavu ulihesabiwa kuwa ni kielelezo cha dhambi, kiasi hata cha kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Walitengwa na kuwekwa nje ya Hekalu, huku wakiendelea kuomba kila siku ya maisha yao!

Ni katika muktadha huu, Mitume Petro na Yohane badala ya kutoa fedha au dhahabu kwa yule Kiwete, wakampatia kile walichokuwa nacho: “Kwa jina la Yesu wa Nazareti simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi, akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya Hekalu pamoja nao, akienda, akirukaruka na kumsifu Mungu. (Rej. Mdo 3: 5-10). Baba Mtakatifu anasema huu ndio mtindo ambao Mwenyezi Mungu anapenda kuutumia kwa ajili ya kujifunua mbele ya watu kwa kujenga na kudumisha mahusiano yanayokita mizizi yake katika majadiliano, ili kugusa undani wa mhusika mwenyewe, kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake katika mwanga wa upendo. Hekalu lilitumika kama kituo kikuu cha maisha ya kiroho, yaani nyumba ya Ibada na sala, lakini pia lilitumika kama soko, yaani mahali pa biashara na shughuli za kiuchumi.

Itakumbukwa kwamba, Manabii wengi walikemea sana mtindo na mwelekeo huu wa maisha, kiasi hata siku moja, Kristo Yesu aliwafukuza Hekaluni, kwa sababu walikuwa wameligeuza Hekalu kuwa ni pango na wevi na wanyang’anyi. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, mwelekeo kama huu unaweza kuzikumba Parokia na kuzigeuza kuwa ni Kituo cha biashara na shughuli za kiuchumi na kusahau kwamba, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa. Ni mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa Kanisa kuendelea kujikita katika ufukara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, yule Kiwete alipoomba msaada hakupewa fedha na badala yake akakutana na Jina la Yesu Mnazareti linalo okoa na kumsimamisha tena kati ya watu!

Kitendo cha Mtume Petro kumshika mkono wa kuume na kumwinua ni kielelezo cha ufufuko kutoka kwa wafu kama anavyotafsiri Mtakatifu Yohane Krizostom. Hiki ni kielelezo cha Kristo Yesu anayejitaabisha kuwanyanyua wale wote wanaoogelea katika shida na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Haya ndiyo maisha na utume wa Kanisa ambalo kamwe haliwezi kuwapatia watu kisogo na badala yake, linayaangalia mateso na mahangaiko ya binadamu, kwani Kanisa ni Mama na Mwalimu, ni chombo cha urafiki na mshikamano wa dhati. Kanisa hadi leo hii linaendelea kuganga na kuponya watu katika shida na mahangaiko yao. Kanisa linataka kuwatazama watu kwa moyo wa huruma na mapendo, kama kielelezo cha ukaribu wa Kristo kwa watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu anakazia sanaa ya kusindikiza, kwa kuthamini utakatifu wa maisha ya binadamu; ili kuwajengea matumaini wale waliokata tamaa; ili kweli waweze kuponywa na huruma ya Mungu sanjari na kuwekwa huru katika shida na mahangaiko yao, tayari kusonga mbele katika maisha ya Kikristo!

Huu ndio mwendelezo wa maisha na utume wa Yesu anayetaka kuwanyanyua na kuwasimamisha tena wale waliokata tamaa katika maisha kutokana na sababu mbali mbali, ikiwa ni pamoja na dhambi. Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumpatia mkono Kristo Yesu anayetaka kuwanyanyua tena kutoka mavumbini! Waamini waendelee kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu katika shida na mahangaiko yao ya ndani, ili kujenga na kudumisha urafiki, umoja na mshikamano na Kristo Mfufuka. Mtume Paulo anasema, wanaweza kuonekana kama wenye huzuni bali siku zote wao ni watu wenye furaha; wanaweza kuonekana kama maskini, bali wanaendelea kuwatajirisha watu wengi zaidi; wanaweza kuonekana kuwa hawana kitu, lakini ni watu wenye vitu vingi. (Rej. 2 Kor 6:10). Utajiri wa Kanisa unafumbatwa katika Injili inayoonesha nguvu ya jina la Kristo Yesu linaloendelea kutenda maajabu na ishara nyingi.

Baba Mtakatifu anawauliza waamini na watu wote wenye mapenzi mema Je, amana na utajiri wao uko wapi? Je, nini wanachoweza kufanya ili kuwatajirisha jirani zao? Waamini wajitaabishe kukumbuka huruma na matendo makuu ya Mungu katika maisha, ili na wao pia waweze kuwa ni mashuhuda wa sifa na utukufu wa Mungu katika maisha yao. Wawe na ujasiri wa kuwanyooshea wengine mikono, tayari kuwasimamisha! Waruhusu mikono yao, iweze kutumiwa na Kristo Yesu kwa ajili ya kuwakomboa wanyonge na maskini duniani!

Papa: Katekesi

 

07 August 2019, 15:54