Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana wa Chama cha Skauti Barani Ulaya kuhakikisha kwamba, wanawekeza katika huduma ya upendo kwa jirani zao! Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana wa Chama cha Skauti Barani Ulaya kuhakikisha kwamba, wanawekeza katika huduma ya upendo kwa jirani zao!  (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko: Skauti wekezeni katika huduma ya upendo

Wapeni watu vitu nanyi mtapewa ni ujumbe, dira na mwongozo wa maisha. Leo hii, watu wengi wanamegubikwa na ubinafsi kiasi cha kutaka kupewa mara moja bila kuchelewa! Wanataka kumiliki na kamwe hawawezi kuridhika na kile wanachokipata, matokeo yake ni mahangaiko ya ndani. Ndiyo maana Kristo Yesu, anawataka wafuasi wake kukita maisha yao katika kutoa kuliko kupokea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 3 Agosti 2019 amehitimisha likizo yake ya kipindi cha kiangazi na kuanza shughuli za kawaida kwa kukutana na vijana 5000 wa Chama cha Skauti Barani Ulaya. Hawa ni vijana wenye umri kati ya miaka 16-21 kutoka katika nchi 20 Barani Ulaya. Wamekuwepo nchini Italia kuanzia tarehe 27 Julai hadi tarehe 3 Agosti, ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha vijana wa kizazi kipya na kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 25 tangu vijana kama hawa walipokutana na Mtakatifu Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana wa kizazi kipya kukita hija ya maisha yao katika ukarimu na huduma, ili waanze kuwajibika barabara kwa leo na kesho iliyo bora zaidi Barani Ulaya. Vijana wawe na ujasiri wa kuleta mageuzi Barani Ulaya kwa kubomoa kuta za utengano, ili kujenga na kuimarisha madaraja na utamaduni wa kukutana na wengine, kwa kufanya hija ya pamoja na wala si kukaa kitako na “kuanza kula bata”!

Hija ya vijana wa Skauti imewawezesha kukutana na baadhi ya watakatifu ambao wameacha alama ya kudumu Barani Ulaya. Hawa ni Mtakatifu Paulo Mtume, Mtakatifu Benedikto wa Norcia, Watakatifu Cyril na Methodi, Mtakatifu Francisko wa Assisi pamoja na Mtakatifu Katarina wa Siena. Hawa ni watakatifu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zao, wakajiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao, urithi, amana na utajiri wanaowaachia vijana wa kizazi kipya ni huu “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa” (Lk 6:38). Huu ni ujumbe, dira na mwongozo wa maisha. Kwa bahati mbaya, leo hii, watu wengi wanamegubikwa na ubinafsi kiasi cha kutaka kupewa mara moja bila kuchelewa! Wanataka kumiliki na kamwe hawawezi kuridhika na kile wanachokipata, matokeo yake ni mahangaiko ya ndani. Ndiyo maana Kristo Yesu, anawataka wafuasi wake kukita maisha yao kwa kutoa kuliko kupokea.

Kutoa maana yake ni kuanza kuchakarika katika maisha, kwa kuondokana na mambo ya raha, starehe na anasa za dunia hii, yanayowafanya vijana wengi kujitafuta wenyewe! Huu ni mwaliko wa kutoka kifua mbele, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kuboresha hali ya maisha ya walimwengu! Vijana wa kizazi kipya wasiridhike kukaa kitako na kuangalia luninga au kuzama katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Ndoto ya furaha ya kweli katika maisha ya ujana inapatikana kwa kujikita katika matumaini, uvumilivu na uwajibikaji kwa kukataa njia za mkato katika maisha. Mwenyezi Mungu aendelee kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya katika hija hii ya maisha na kwamba, yuko pamoja nao, ili kuwatia shime na kuwaunga mkono.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kulinda na kutunza asili yao, kwani Mwenyezi Mungu amemuumba kila mmoja jinsi alivyo, akamapatia jina kwa makusudi kamili na kamwe vijana wasikubali kugeuzwa kuwa ni “vivuli” au “photocopy” kama wanavyosema wenye lugha zao! Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya vijana ambao wamepoteza asili na utambulisho wao, wamegeuka kuwa kama bendera fuata upepo! Hawa ni watu wasiojali wala kuguswa na shida na mahangaiko ya watu wengine! Ni vijana waliokengeuka na sasa wamekuwa ni karaha mbele ya jamii. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Baada ya kufafanua kuhusu dhana ya kutoa, Baba Mtakatifu ameendelea pia kufafanua kwamba, baada ya kutoa hata wao watapewa na Mwenyezi Mungu mambo makuu hata yale ambayo kamwe hawawezi hata kuthubutu kufikiria.

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa ukarimu na upendo, kamwe hawezi kuwaacha watoto wake mikono mitupu na wala si nia yake kumpokonya kijana mambo yake. Lakini, jambo la msingi kwa vijana ni kuhakikisha kwamba, wanafanya hija, inayowaweka huru kutoka katika undani wa maisha yao, dhidi ya ulaji wa kupindukia unaowafanya vijana kuweweseka na toleo jipya la simu ya mkononi au “pamba nyepesi” iliyoingia kwenye mitindo ya mavazi! Lakini yote haya ni ubatili mtupu ni mambo ya kuja na kupita na kamwe hayawezi kumwachia mtu furaha ya kweli. Furaha ya kweli inapatikana pale mtu anapojisikia kupenda na kupendwa. Kumbe, kutoa ni sehemu ya ufunguo wa maisha unaomsukuma kijana kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zake, kama alivyofanya Mama Theresa wa Calcutta kwa kuwaheshimu, kuwathamini na kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu, hata kama kulikuwa na umati mkubwa wa maskini sehemu mbali mbali za dunia, lakini alifanya kile alichoweza kufanya!

Kila mtu anaitwa kutoa kile alicho nacho kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya ulimwengu, ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Kila mtu ana nafasi ya pekee na ana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha vijana wa Skauti kwamba,  mwanzo wao ni huduma inayomwilishwa katika udugu wa vijana wa Skauti na kwa njia hii ya maisha, kwa hakika hata wao watapewa! Huu ni mwaliko wa kushikamana na kutembea kwa pamoja kama ndugu, kwa kuondokana na upweke unaoweza kuwatumbukiza vijana katika ombwe la mawazo mazito na ndoto za mchana! Vijana wa kizazi kipya watumie mikono yao kwa ajili ya kujenga na kuhudumia pamoja na kuwajali wengine jinsi walivyo.

Vijana waendelee kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho. Kazi ya uumbaji ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ni sawa na kitabu kilicho wazi, kinachoendelea kutoa mafundisho ya hekima na busara. Mazingira kazi ya uumbaji ni daraja kati ya Mungu na binadamu. Kumbe, vijana wa kizazi kipya wanapaswa kujenga madaraja na utamaduni wa kukutana na wengine. Hawa ni watu wenye historia na ukweli wa maisha na kwamba, wana haki pia ya kuishi katika ulimwengu huu. Vijana wa Chama cha Skauti Barani Ulaya wanaongozwa na kauli mbiu “Parate viam Domini” yaani “Tengenezeni njia ya Bwana popote pale mlipo” kwa kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo. Vijana wajitahidi kuwa ni raia wema na wachapakazi.

Mwanzilishi wa Chama cha Skauti Baden Powel aliwahi kusema, “Mwenyezi Mungu, hatafuti watu wema, lakini anawatafuta watu wanaoweza kutenda mema”. Watu wenye upendo wa dhati kwa Bara la Ulaya; watakaochakarika usiku na mchana katika mchakato wa kulisongesha mbele Bara la Ulaya katika mchakato wa upatanisho na maendeleo fungamani ya binadamu. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka vijana wa Chama cha Skauti Barani Ulaya kujifunga kibwebwe ili kuleta mabadiliko makubwa Barani Ulaya, kwa kutoa nafasi, ili kujenga na kudumisha madaraja na utamaduni wa watu kukutana. Bara la Ulaya linahitaji madaraja ya kuwakutanisha watu. Chama cha Skauti kinalenga kuwafunda vijana katika misingi ya ukweli, utu wema, ustawi na maendeleo ya wengi. Vijana wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao!

Papa: Skauti

 

05 August 2019, 11:43