Tafuta

Papa Francisko asikitishwa na vifo vya wakimbizi na wahamiaji 150 waliokufa maji hivi karibuni kwenye Pwani ya Libya. Papa Francisko asikitishwa na vifo vya wakimbizi na wahamiaji 150 waliokufa maji hivi karibuni kwenye Pwani ya Libya. 

Papa Francisko asikitishwa na vifo vya wahamiaji 150 baharini

Papa Francisko amewakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji waliofariki dunia kwenye ajali ya boti hivi karibuni. Hizi ni athari za utandawazi usiojali wala kuguswa na utu, heshima na haki msingi za binadamu! Papa anatoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kutenda kwa haraka na kufanya maamuzi mazito yatakayosaidia kudhibiti maafa kama yasitokee ili kuokoa maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) limesema hivi karibuni kwamba, wahamiaji zaidi ya 150 wanahofiwa kufamaji kwenye ajali ya kuzama kwa boti katika Bahari ya Mediterrania, Pwani ya Libya. Habari zinasema watu hao waliondoka Libya wakiwa wamepanda boti kabla ya maji kujaa ndani ya boti hiyo na kuzama kufuatia injini yake kupata hitilafu. Wengi wa watu waliofariki dunia ni wanawake na watoto ambao hawakuweza kuokoa maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 28 Julai 2019, amewakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji waliofariki dunia kwenye ajali hiyo ya boti. Hizi ni athari za utandawazi usiojali wala kuguswa na utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kutenda kwa haraka na kufanya maamuzi mazito yatakayosaidia kudhibiti maafa kama haya kwa kuokoa maisha ya watu sanjari na kulinda utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye, ili kusali kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliofariki dunia katika ajali ya boti pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zao na wala makaburi yao hayataweza kuoneka kamwe! Baba Mtakatifu akirejea katika tafakari yake kuhusu Sala ya Baba Yetu, amewaomba waamini kumuuliza Mwenyezi Mungu, Je, Baba Yetu, yote haya yana maana gani? Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia, linaendelea kuunda maisha ya watu wengi duniani: kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Ili kuweza kukabiliana na changamoto kubwa kama hii, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inakuwa na mbinu mkakati wa kuwashirikisha wahamiaji na wakimbizi hawa katika shughuli za maisha ya jamii inayowapatia hifadhi; kwa kuzingatia: utu na heshima ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya ubaguzi wanayotendewa baadhi ya wahamiaji kutokana na mahali wanakotoka au dini yao! Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alisema,  Kanisa linamtambua Kristo Yesu anayeteseka miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi, ustawi na maendeleo yao, kwani hawa ni watu wanao kimbia: vita, kinzani na athari za mabadiliko ya tabianchi! Wakristo kwa kushirikiana na wadau mbali mbali duniani wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ukarimu na mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji!

Kuna haja ya kuwa na wongofu wa mawazo potofu dhidi ya wakimbizi na wahamiaji, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana katika kukabiliana na changamoto za maisha, ili hatimaye, kujenga dunia inayosimikwa katika msingi ya: haki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu!

Papa: Maafa

 

28 July 2019, 10:04