Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amebainisha Mpango Mkakati wa Wayesuit katika maisha na utume wa Kanisa kuanzia mwaka 2019-2029. Baba Mtakatifu Francisko amebainisha Mpango Mkakati wa Wayesuit katika maisha na utume wa Kanisa kuanzia mwaka 2019-2029. 

Papa Francisko: Mpango Mkakati wa Wayesuit katika maisha na utume wa Kanisa 2019-2029

Mpango Mkakati wa Wayesuit katika maisha na utume wa Kanisa 2019-2029: Kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na mafungo ya kiroho; Kushikamana na maskini, Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao na kutunza mazingira. Haya ni mambo ambayo yanabainishwa na Papa Francisko katika barua aliyomwandikia Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wayesuit katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo makuu yafuatayo: Kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na mafungo ya kiroho; Kushikamana na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao; Mwishoni, kutunza mazingira nyumba ya yote. Haya ni mambo ambayo yanabainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit kama sehemu ya mpango mkakati wa maisha na utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani kuanzia mwaka 2019-2029. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi pia ndivyo vipaumbele vya Kanisa la Kiulimwengu kwa wakati huu! Mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sinodi za Maaskofu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Vipaumbele hivi vinachota utajiri wake kutoka katika Wosia wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”, ambamo Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, furaha inayobubujika kutoka katika imani, inaganga na kuponya madonda na changamoto za maisha na utume wa Kanisa, daima Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya kueneza Furaha ya Injili baada ya kukutana na Kristo Yesu katika: Neno lake, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma kwa jirani. Baba Mtakatifu anendelea kufafanua kwamba, vipaumbele vya Wayesuit katika kipindi cha miaka kumi kuanzia sasa ni msingi wa uhusiano na mafungamano kati ya Wayesuit na Kristo Yesu; mambo yanayomwilishwa katika maisha binafsi na katika Jumuiya inayosali na kufanya mang’amuzi ya pamoja.

Vipaumbele hivi ni sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Wayesuit ambao umefanyiwa kazi katika kipindi cha miaka miwili, ili kuhakikisha kwamba, Wayesuit wanatumia kikamilifu rasilimali watu, vitu na fedha, ili kufikia lengo hili muhimu, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati. Kuendeleza mchakato wa mang’amuzi na mafungo ya kiroho ni mambo msingi katika maisha na utume wa Wayesuit anasema Padre Arturo Sosa. Hapa kinachohitajika ni kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu, kwa kuwashirikisha watu kutoka katika makundi na medani mbali mbali za maisha, ili kugundua amana na utajiri unaofumbatwa katika mafungo ya kiroho yanayotolewa na Wayesuit. Kushikamana na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Wayesuit kuhakikisha kwamba, wanaonesha mshikamamo wa huruma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, haki jamii inapewa msukumo wa pekee, ili kweli mabadiliko makubwa yanayojitokeza katika masuala ya: kiuchumi, kijamii na kisiasa, yanazingatia haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Hii ni changamoto pia ya kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia pamoja na matumizi mabaya ya madaraka! Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao ni pamoja na kuyaangalia yale mema, mazuri na matakatifu yanayowazunguka vijana katika ulimwengu wao, kwa kusikiliza na kujibu kiu na matamanio yao halali kadiri ya mabadiliko ya jamii kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Hii ni changamoto ya kuwapatia vijana fursa ya kuonesha vipaji na ubunifu wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Umefika wakati kwa viongozi wa Kanisa kujifunza kutoka kwa vijana wa kizazi kipya! Mwishoni, ni utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kushiriki katika sera, mbinu na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira, pamoja na kuangalia sera mbadala, ili kuweza kudhibiti uharibifu wa mazingira unaoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu wengi duniani. Hii ni changamoto ya kushirikiana na wadau mbali mbali kama sehemu ya mbinu mkakati wa utekelezaji wa malengo haya katika maisha na utume wa Wayesuit.

Papa: Wayesuit

 

 

31 July 2019, 14:18