Tafuta

Vatican News
Papa Francisko awapongeza viongozi wakuu wa Marekani na Korea ya Kusini kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana ili kukoleza mchakato wa amani duniani! Papa Francisko awapongeza viongozi wakuu wa Marekani na Korea ya Kusini kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana ili kukoleza mchakato wa amani duniani!  (AFP or licensors)

Papa: Awapongeza Rais Trump & Kim Jong-u: Amani duniani

Papa amepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Kim Jong-un wa Korea ya Kaskazini katika mchakato wa kutafuta ili hatimaye kudumisha amani, si tu kwa ajili ya Korea ya Kaskazini, bali amani kwa ulimwengu mzima. Rais Trump na Rais Kim Jong-un, wamekutana kwenye mpaka kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, huko "DMZ".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 30 Juni 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Kim Jong-un wa Korea ya Kaskazini katika mchakato wa kutafuta ili hatimaye kudumisha amani, si tu kwa ajili ya Korea ya Kaskazini, bali amani kwa ulimwengu mzima. Rais Trump na Rais Kim Jong-un, wamekutana kwenye mpaka kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, sehemu inayojulikana  kama “Demilitarised Zone, DMZ, yaani” “Sehemu ya amani”. Viongozi hawa wawili wamekuwa na mazungumo ya muda wa saa nzima, wamezungumzia mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa “Nyumba ya uhuru” huko kwenye mpaka wa Korea ya Kusini. Mkutano huu umehudhuriwa pia na kwa muda mfupi na Rais Moon Jae-in wa Korea ya Kusini.

Itakumbukwa kwamba, viongozi hawa wawili, mwaka 2018 walikutana huko Singapore na wakaweka mkakati wa kudhibiti silaha huko Korea ya Kaskazini, jambo linalotishia usalama na amani duniani. Mapema mwaka huu wa 2019, viongozi hawa walikutana tena, lakini mkutano ukavunjika, bila ya kuwa na maendeleo makubwa na kwa sasa viongozi hawa wamejiwekea mkakati wa kuunda kikosi kazi cha majadiliano, ili kuhakikisha kwamba, haya wanayojadili yanatekelezeka kwa ajili ya kujenga na kudumisha usalama, amani, ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu katika ujumla wake! Wachunguzi wa mambo wanasema, hii ni hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini, ndiyo maana Baba Mtakatifu anapongeza jitihada hizi zinazopania kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kufahamiana, kujadiliana na hatimaye, kusaidiana kwa hali na mali.

Rais Trump amepata nafasi ya kukanyaga kwa dakika chache ardhi ya Korea ya Kaskazini na kutoa mwaliko kwa Rais Kim Jong-un kutembelea Ikulu ya Marekani, ingawa tarehe maalum bado haijapangwa na Serikali zote mbili. Tukio hili adhimu limemfanya Rais Trump wa Marekani, kuwa ni Rais wa kwanza kutoka nchini humo kuweza kukanyaga ardhi ya Korea ya Kaskazini, tangu baada ya kumalizika kwa Vita Baridi! Jumuiya ya Kimataifa inawahitaji mashuhuda na wajenzi wa amani duniani, kwani vita imeendelea kuwa ni sababu ya majanga makubwa yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo!

Papa:Korea: Amani
01 July 2019, 08:54