Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Mfumo wa umaskini mpya duniani: Watu wanaonyanyaswa na kupuuzwa; wagonjwa, wazee na watoto; wakimbizi na wahamiaji duniani! Papa Francisko: Mfumo wa umaskini mpya duniani: Watu wanaonyanyaswa na kupuuzwa; wagonjwa, wazee na watoto; wakimbizi na wahamiaji duniani!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Lampedusa: Kumbu kumbu ya Miaka 6: Wakimbizi & Wahamiaji

Leo hii kuna aina mbali mbali za umaskini zinazomwandama mwanadamu. Hawa ni wale wanaonyanyaswa na kupuuzwa; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watoto wadogo, wazee na wagonjwa bila kuwasahau wale ambao jamii haiwathamini. Mawazo ya Papa yanawaendea maskini wanaomlilia Kristo Yesu, ili aweze kuwaokoa na shida pamoja na magumu yanayowaandama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 8 Julai 2013 kwa mara ya kwanza kabisa, Baba Mtakatifu Francisko, baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alipofanya ziara yake ya kwanza kutoka mjini Vatican ili kwenda kwenye Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko Kusini mwa Italia, kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahifadhiwa Kisiwani hapo. Lakini pia, Baba Mtakatifu alipenda kusali na kuwaombea wale wote waliofariki dunia na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania na makaburi yao hayana alama wala kumbu kumbu tena! Hili ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kiasi hata cha kuanzisha Idara ya Wakimbizi na wahamiaji kwenye Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, inayowajibika moja kwa moja kwake binafsi!

Jumatatu, tarehe 8 Julai 2019, Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, ambao wamepoteza maisha yao, wakiwa njiani kutafuta, hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee wokovu wa Mungu uliojidhirisha katika maisha ya Yakobo anayejiaminisha mbele ya Mungu pamoja na ukombozi unaobubujika kutoka kwenye huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa maskini na wale wote wanaoteseka na kukata tamaa kutokana na magonjwa na kifo! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Yakobo alipokuwa akitoka Beer-sheba kwenda Harani, akiwa njiani alichoka na safari, akalala usingizi, na kuota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni.

Tena tazama Malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake, kielelezo cha daraja linalomuunganisha Mwenyezi Mungu na binadamu na daraja hili limepewa tafsiri yake kuwa ni Fumbo la Umwilisho. Hiki ni kielelezo cha ufunuo wa upendo wa Mungu kwa waja wake na kwamba, ngazi inaonesha jitihada za Mwenyezi Mungu zinazotangulia juhudi za binadamu, ambao walitaka kwa nguvu na jeuri yao binafsi kupanda kwenda mbinguni kwa kujifanya kuwa miungu! Lakini, Mwenyezi Mungu anashuka na kujifunua kuwa ni Mungu anayeokoa. Huyu ni Mungu pamoja na watu wake yaani ni “Emmanuel” anayetekeleza ahadi zake kwa njia ya upendo unaomwilishwa katika huruma inayomkirimia mwanadamu zawadi ya maisha tele! Ni katika muktadha wa ufunuo wa Mungu, Yakobo anajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kujiwekea dhamana ya kumtambua Mungu na kumwabudu, chemchemi ya historia nzima ya wokovu.

Yakobo anamwomba Mwenyezi Mungu amlinde katika safari yake na kumpatia mahitaji msingi, naye akirejea kwa amani nyumbani mwa baba yake, ndipo Bwana atakuwa Mungu wake! Yakobo anajiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu Bwana ndiye kimbilio lake na ngome yake, ni usalama wa maisha yake na ni Mungu anayemtumainia. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapatia ulinzi na tunza yake ya kibaba wale wote wanaomkimbilia kwa imani na matumaini. Ndiyo maana ya sala za waamini zinaogopesha pale wanapotambua kwamba, sala zao si mali kitu, bali nguvu na usalama wa maisha yao unatoka kwa Mungu aliye juu, huyu ndiye Mungu anayeokoa! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya somo la kwanza na Injili ya siku inayomwonesha Kristo Yesu alivyomfufua binti wa jumbe na alivyomponya mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, aliyekuja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake.

Yote haya ni matendo yanayoonesha nguvu ya Kristo Yesu inayomwokoa mwanadamu kutoka katika magonjwa na kifo. Huruma na upendo wa Yesu unawagusa na kuwaambata wote bila kuwatenga hata kidogo. Ikumbukwe kwamba, mwanamke aliyekuwa anatoka damu kwa muda wa miaka kumi na miwili alihesabiwa kuwa ni najisi, lakini Yesu kwa huruma na upendo wake, anamwona yule binti aliyekuwa amefariki dunia pamoja na mwanamke aliyekuwa akitoka damu kwa muda wa miaka kumi na miwili kuwa ni kielelezo  cha maskini na wale watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Hawa ndio wale watu anaotaka kuwaonjesha upendo na kuwanyanyua juu “kama mlingoti wa simu”! Yesu mbele ya Mitume wake, anawafunulia upendeleo kwa maskini; wanaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika umwilishaji wa Injili ya upendo.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, leo hii kuna aina mbali mbali za umaskini zinazomwandama mwanadamu. Hawa ni wale wanaonyanyaswa na kupuuzwa; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watoto wadogo, wazee na wagonjwa bila kuwasahau wale ambao jamii haiwathamini tena kutokana na hali yao ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka sita tangu alipotembelea Kisiwa cha Lampedusa, mawazo yake yanawaendea maskini wanaomlilia Kristo Yesu, ili aweze kuwaokoa na shida pamoja na magumu yanayowaandama. Hawa ndio wale wanaorubuniwa kutokana na umaskini wao na baadaye kutelekezwa kwenye jangwa na utupu wa maisha! Ni watu wanaoteswa, wanaonyanyaswa na kudhulumiwa utu na heshima yao; wanaodharirishwa na kubakwa katika kambi na vizuizi vya wakimbizi na wahamiaji.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, hawa ni wale wanaopambana na mawimbi mazito ya Bahari ya Mediterrania; watu wanaoteseka kwenye vizuizi vya wakimbizi na wahamiaji kwa muda mrefu. Hii ni mifano ya watu ambao Yesu anawataka wafuasi wake kuwaonesha upendo na kuwainua tena katika utu, heshima na haki zao msingi. Inasikitisha kuona kwamba, pembezoni mwa miji mbali mbali duniani kumesheheni watu waliotelekezwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni watu wanaotengwa na kubaguliwa; wanaonyanyaswa na kudhulumiwa; maskini, wagonjwa na wale wanaoteseka. Kristo Yesu, kwa njia ya Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho yake makuu, anawataka wafuasi wake kuwafariji na kuwahurumia wale wanaoteseka; kuwalisha na kuwanywesha wenye njaa na kiu ya haki; ili wasikie kutoka katika undani wa maisha yao kwamba wanapendwa na Mungu na hatimaye, kuwaonesha njia inayowapeleka mbinguni kwa Baba.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa si wakimbizi peke yao, bali ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kielelezo cha maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ile ngazi ya Yakobo ni kielelezo cha Kristo Yesu ambaye amekuwa ni ngazi kati ya mbingu na dunia. Hii ni ngazi ambayo inaweza kutumiwa na wote pamoja na kuwahakikishia usalama wa maisha yao. Lakini ili kuweza kuipanda kunahitaji nguvu ya ziada na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanyonge, maskini na wagonjwa wanapaswa kusaidiwa na wenye nguvu, ambao watakuwa kama wale Malaika waliokuwa wanapanda na kushuka, vinginevyo maskini hawa wataendelea kubaki nyuma na kudidimia katika umaskini na utupu wao.

Huu ni wajibu na dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanashirikiana ili kuleta wokovu na ukombozi kwa watu hawa. Jambo hili linawezekana kwa njia ya umoja, ushirikiano na mshikamano. Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma, ulinzi na ustawi wa wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni alama ya utu, shukrani na mshikamano wa dhati!

Papa: Lampedusa
08 July 2019, 14:46