Papa Francisko: Mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu: Ni kutoa elimu itakayosaidia ujenzi wa udugu na utamaduni wa upendo, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Papa Francisko: Mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu: Ni kutoa elimu itakayosaidia ujenzi wa udugu na utamaduni wa upendo, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. 

Vipaumbule vya Kanisa katika Sekta ya Elimu Duniani: Udugu na utamaduni wa upendo!

Kardinali Timothy Dolan: Utume wa Kanisa katika maendeleo ya sekta ya elimu duniani: Kanisa linasukumuzwa na imani kutoka kifua mbele, ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na katika muktadha huu, linataka kupambana na ujinga pamoja na kuendelea kukabiliana na changamoto zinazoibuka katika sekta ya elimu kila kukicha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Hivi karibuni, Jimbo kuu la New York Marekani, limeadhimisha Kongamano la Elimu Katoliki Kimataifa, OIEC, 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Elimu ya udugu wa kibinadamu katika ujenzi wa utamaduni wa upendo”. Mambo makuu matatu yamepewa kipaumbele cha pekee: Mosi: Mwongozo wa Elimu Katoliki Duniani. Pili, Elimu kadiri ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Tatu, ni Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya utekelezaji wa misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa kongamano hili kutoka sehemu mbali mbali za dunia amekazia kuhusu: Elimu ya Kikristo kama ilivyopembuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Changamoto mamboleo katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu pamoja na umuhimu wa kutoa kipaumbele cha pekee cha mshikamano na maskini, ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano! Baba Mtakatifu anasema, ushiriki wa wajumbe hawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika utume wa kuelimisha mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaelimisha watoto wanaohudhuria katika shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi, zile shule ambazo ziko pembezoni mwa jamii na huko ndiko Mama Kanisa anataka kuelekeza nguvu zake zaidi! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walilitaka Kanisa kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya, kwa kukazia haki ya elimu na maana ya elimu kadiri ya Mafundisho ya Kanisa. Wanadamu wote wa taifa lolote, cheo chochote na umri wowote, kwa mujibu wa hadhi yao ya kibinadamu wanayo haki isiyofutika ya kupata elimu.

Elimu inayofaa kwa shabaha ya maisha yao, elimu inayolingana na tabia, utofauti wa jinsia, utamaduni, mila na desturi za taifa lao. Elimu isaidie kujenga na kudumisha udugu na watu wa mataifa mengine; umoja na amani ya kweli duniani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, watoto na vijana lazima wasaidiwe kustawisha utaratibu wa johari za kimwili, za kimaadili na za kiakili. Wawe ni watu wanaopania ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na kuwa tayari kujadiliana na wengine, ili kukuza na kudumisha umoja na ushirikiano na wengine. Elimu makini inakita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi za binadamu kama anavyokaza kusema Mtakatifu Yohane Paulo II.

Elimu lazima isaidie kumwilisha tunu msingi za maisha ya: haki, amani, mahusiano na mafungamano sahihi ya: watu binafsi, jamii na serikali ili kukuza na kudumisha mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni. Huu ni udugu wa kibinadamu unaopaswa kupenyeza mizizi yake hata katika masuala ya maendeleo na uchumi fungamani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Elimu makini lazima igusie pia elimu ya ekolojia inayozingatia mahusiano mema kati ya ubinadamu na mazingira katika ngazi mbali mbali yaani ekolojia linganifu inapania kuleta utulivu mioyoni mwa watu, maumbile na kwa viumbe wengine na hivyo kuwasaidia watu kudumisha amani kati yao na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, hii ni changamoto pevu inayopaswa kushughulikiwa kwa umoja na mshikamano; kwa kufanya mang’amuzi ya pamoja, kuangalia fursa zilizopo, matatizo na hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa elimu makini, kwa kuendelea kuchota amana na utajiri kutoka katika shuhuda za watakatifu waliosadaka maisha yao katika elimu, mwanga angavu hata kwa wadau wa elimu kwa wakati huu! Changamoto kubwa kwa wakati huu ni tabia ya kutaka kubomoa udugu kutokana na uchoyo, ubinafsi, ulaji wa kupindukia, utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine pamoja na tabia ya kutaka kumong’onyoa tunu msingi za maisha ya kijamii.

Ili kuweza kukabiliana na changamoto hii kuna haja ya kuangalia hali halisi na ukweli katika sekta ya elimu. Familia ni mahali pa awali kabisa pa kujifunza kuishi inavyokubalika na jamii. Ni mahali pa kwanza pa kujifunza kuhusiana na wengine, kusikilizana na kushirikishana; kuvumiliana, kuheshimiana pamoja na kusaidiana. Wazazi, walezi na walimu wanatakiwa kushirikiana katika utekelezaji wa taaluma yao, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, ili kuwasaidia vijana waweze kuwa ni wajenzi hai wa ulimwengu unaosimikwa katika mshikamano, haki na amani. Taasisi za elimu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki vina dhamana na utume wa kuhakikisha kwamba, vinawasaidia vijana kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho.

Upendeleo wa pekee, uwe ni kwa ajili ya wanafunzi wanaoishi pembezoni mwa jamii; ili kujenga mtandao wa elimu fungamani, ili hatimaye, kuvunjilia mbali kuta za utengano kielimu, ili hatimaye, kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, ili kudumisha haki, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii inafaa kwa tafakari ya kina na hatimaye, utekelezaji wake!

Changamoto nyingine inayojitokeza dhidi ya elimu ya udugu wa kibinadamu ni kuhusu ukiritimba wa matokeo unaomgeuza mwanafunzi kuwa kama maabara ya majaribio, badala ya kukazia ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili matokeo yake, mtindo unaopewa kipaumbele ni ule uzalishaji na ulaji, kiasi cha kuwageuza watu kuwa kama watazamaji wa mchakato wa elimu. Ukuaji, utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa elimu. Mwalimu anapaswa kuwa na utaalam, sifa; utu na heshima; mambo yatakayomsaidia mwanafunzi kukua na kukomaa: kiutu na kiroho. Mwalimu awe na uwezo wa kuunganisha utaalam na ujuzi wake, tayari kuwahudumia jirani zake; mambo yanayohitaji majiundo endelevu.

Lengo ni kuwasaidia waalimu na wafanyakazi katika sekta ya elimu kuboresha elimu, ujuzi na maarifa yao bila kusahau maisha ya kiroho sanjari na malengo yake ya kiroho. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, sekta ya elimu haina budi kukabiliana na changamoto ya mwendo kasi wa mabadiliko kiasi hata cha kuwachanga wanafunzi. Mabadiliko ni jambo jema, lakini wakati mwingine mabadiliko haya yanakuwa ni chanzo cha wasi wasi pale ambapo yanasababisha madhara ulimwenguni na kwenye ubora wa maisha ya watu walio wengi. Watu wanahitaji muda wa kukua na kukomaa; muda wa ukimya na tafakari juu ya uzuri wa kazi ya uumbaji.

Lengo liwe ni kutafuta njia ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Mtindo na mifumo mipya ya maisha ilinde na kuheshimu vizazi vijavyo. Baba Mtakatifu anahitimisha kwa kusema kwamba, Kongamano la Elimu Katoliki Kimataifa kwa kuongozwa na kauli mbiu “Elimu ya udugu wa kibinadamu katika ujenzi wa utamaduni wa upendo” imekuwa ni fursa ya kuweza kufanya upembuzi yakinifu kuhusu changamoto mamboleo katika sekta ya elimu katika ulimwengu wa utandawazi na unaongozwa na mfumo wa kidigitali. Huu ni mwaliko kwa Kanisa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na taasisi za elimu kimataifa.

Wadau wa sekta ya elimu waendelee kujisadaka ili kusaidia mchakato wa elimu kuwa na mwelekeo mpana zaidi unaofumbatwa katika majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Taasisi za elimu Katoliki ziwe ni chemchem ya ukuaji katika mwanga wa Injili, ili kuwawezesha vijana kuwa wajenzi wa udugu wa kibinadamu tayari kushiriki katika utamaduni wa upendo. Kardinali Timothy Michael Dolan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la New York, Marekani katika ujumbe wake wa kuwakaribisha washiriki wa kongamano hili, amekazia umuhimu wa utume wa Kanisa katika maendeleo ya sekta ya elimu duniani. Kanisa linasukumuzwa na imani kutoka kifua mbele, ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na katika muktadha huu, linataka kupambana na ujinga pamoja na kuendelea kukabiliana na changamoto zinazoibuka katika sekta ya elimu kila kukicha!

Elimu bora ni kati ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Lengo hili linalenga kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora na fungamani, inayozingatia usawa na kutoa fursa kwa wote kujiendeleza. Linasisitiza kuwezesha kila mtu kusoma, kujifunza na kuhakikisha kwamba binadamu wote wanafikia vipawa vyao kikamilifu. Lengo hili linapania kupunguza idadi ya watu ambao hawajui kusoma na kuandika duniani huku likisisitiza kuboreshwa kwa mazingira ya kutolea elimu, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa walimu na vitabu vya kutosha vinavyokidhi vigezo, miundombinu bora kama madarasa, meza na madawati.

Vile vile linasisitiza juu ya utoaji fursa ya elimu kwa watu wote isiyokuwa na ubaguzi kwa watu wenye ulemavu, huku likidhamiria kuongeza idadi ya vijana na watu wazima wenye ujuzi pamoja na ufundi stadi kwa ajili ya ajira, kazi zenye heshima na ujasiriamali. Jimbo kuu la New York Marekani, kuanzia tarehe 5-8 Juni 2019 limekua likiadhimisha Kongamano la Elimu Katoliki Kimataifa kwa kuongozwa na kauli mbiu “Elimu ya udugu wa kibinadamu katika ujenzi wa utamaduni wa upendo. Kongamano hili limekita mizizi yake katika mambo makuu matatu: Mosi: Mwongozo wa Elimu Katoliki Duniani. Pili, Elimu kadiri ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.

Tatu, Baba Mtakatifu Francisko, katika Waraka wake wa kitume, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, anasistizia kuhusu utunzaji bora wa mazingira, changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani na mshikamano kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Kardinali Timothy Michael Dolan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la New York, Marekani katika ujumbe wake wa kuwakaribisha washiriki wa kongamano hili, amekazia umuhimu wa utume wa Kanisa katika maendeleo ya sekta ya elimu duniani. Kanisa linasukumwa na imani kutoka kifua mbele, ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na katika muktadha huu, linataka kupambana na ujinga pamoja na kuendelea kukabiliana na changamoto zinazoibuka katika sekta ya elimu kila kukicha!

Changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, hata watoto wa maskini, yaani wale “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanapata elimu bora, ufunguo wa maisha bora zaidi! Kongamano hili limehudhuriwa na wajumbe 1, 000 waliowawakilisha watu milioni 46 kutoka katika shule 210, 000 zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki katika nchi zaidi ya 100, na sehemu kubwa ya utume wa Kanisa katika sekta ya elimu umeegemea katika Nchi zinazoendelea duniani. Mafanikio, changamoto na fursa za elimu ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waweze kuonja tena ile furaha ya kazi ya ukombozi, iliyotekelezwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.

Elimu Katoliki
09 July 2019, 14:40