Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa na kifo cha Kardinali Paolo Sardi, kiongozi na shuhuda mwaminifu wa mafundisho ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa na kifo cha Kardinali Paolo Sardi, kiongozi na shuhuda mwaminifu wa mafundisho ya Kanisa.  (AFP or licensors)

Tanzia: Kardinali Paolo Sardi amefariki dunia! Shuhuda amini wa Kristo na Kanisa lake!

Marehemu Kardinali Sardi kutokana na moyo wake wa kipadre, majiundo yake ya kitaalimungu, karama mbali mbali alizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, pamoja na hekima na busara vilimwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kuchangia katika mafundisho ya Mt. Paulo VI, Papa Yohane Paulo wa kwanza, Mt. Yohane Paulo II na hatimaye, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Paolo Sardi, aliyefariki dunia tarehe 13 Julai 2019, akiwa na umri wa miaka 84 ya kuzaliwa. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi alizomtumia Bwana Pietro Angelo Sardi, kaka yake Marehemu Kardinali Sardi pamoja na ndugu, jamaa na wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu, anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Katika muktadha wa mwanga wa imani, Baba Mtakatifu anapenda kumtolea Mwenyezi Mungu: shukrani, sifa na utukufu kwa ushuhuda adhimu uliooneshwa na Marehemu Kardinali Sardi katika maisha na utume wake kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Vatican.

Baba Mtakatifu anaendelea kumwelezea Marehemu Kardinali Sardi kwa kusema kwamba, kwa hakika moyo wake wa kipadre, malezi na majiundo yake ya kitaalimungu pamoja na karama mbali mbali alizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, hekima na busara vilimwezesha kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa umakini mkubwa, na hivyo kumwezesha kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mafundisho ya Mtakatifu Paulo VI, Papa Yohane Paulo wa kwanza, Mtakatifu Yohane Paulo II na hatimaye, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Katika salam zake za rambi rambi, Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapenda kuunganisha salam hizi pamoja na “Litania ya Salam za rambi rambi” zinazobubujika kutoka kwa umati wa waamini waliokuwa wanamiminika kila siku, kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

“Esto Vigilans” ndiyo kauli mbiu yake ya Kiaskofu, iliyomwezesha kuwa ni Mtumishi mwaminifu ambaye alijitahidi kukesha daima. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kwa sala, tunza na maombezi ya Bikira Maria, Watakatifu Petro na Paulo Mitume; ili waweze kumpokea na hatimaye, kumshirikisha karamu ya maisha ya uzima wa milele! Ibada ya Misa Takatifu, imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 15 Julai 2019 na kuongozwa na Kardinali Tarcisio Bertone. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Italia. Mara baada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza sala ya buriani kwa Marehemu Kardinali Paolo Sardi. Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali Paolo Sardi alizaliwa tarehe 1 Septemba 1934, Jimboni Acqui, Kaskazini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Juni 1958 akapewa Daraja takatifu ya Upadre.

Ni kiongozi ambaye alijiendeleza sana katika masomo na hatimaye, kunako mwaka 1963 akatunukiwa shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian na baadaye akajipatia tena Shahada ya Uzamivu katika Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sacro Cuore cha Milano, kunako mwaka 1968. Katika maisha na utume wake, alibahatika kuwa ni Jaalimu wa Sheria za Kanisa. Kunako mwaka 1976 akaitwa kufanya utume wake kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Anakumbukwa sana katika utume wake wa kuhariri hotuba mbali mbali za Mapapa na kila siku asubuhi alikuwa anaadhimisha Ibada ya Misa takatifu mahali alipozikwa Mtakatifu Yohane XXIII kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tarehe 10 Desemba 1996 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na kuteuliwa kuwa Balozi wa Vatican kwa majukumu maalum. Tarehe 23 Oktoba 2004 akateuliwa kuwa ni “Camerlengo” Msaidizi wa Kanisa Katoliki. Huyu ni kiongozi  wa shughuli za Kanisa wakati kunapotokea kwamba, Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiko wazi kwa sababu mbali mbali. Tangu mwaka 2005 akasimamia na kuratibu Mikutano ya Makardinali wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 20 Novemba 2010 akamteuwa kuwa Kardinali na tarehe 22 Januari 2011 akang’atuka na kuachia madaraka ya Msaidizi wa “Camerlengo” wa Kanisa Katoliki.

Papa: Kardinali Sardi
15 July 2019, 15:58