Vatican News
Jukwaa la Vijana Kimataifa: Papa Francisko asema, vijana ni leo ya Mungu na Kanisa! Jukwaa la Vijana Kimataifa: Papa Francisko asema, vijana ni leo ya Mungu na Kanisa!  (AFP or licensors)

Jukwaa la Vijana Kimataifa: Vijana ni leo ya Mungu na Kanisa!

Ulimwengu umegubikwa na kinzani na migawanyiko mbali mbali inayodumaza mchakato wa ujenzi wa umoja, upendo, mshikamano kati ya watu. Vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja, upendo na mshikamano duniani. Mama Kanisa anawatambua vijana kuwa ni wadau wakuu wa mchakato mzima wa wongofu wa kichungaji, kama wanavyosema Mababa wa Sinodi.

Na Shemasi Amani Karoli Joseph, - Vatican.

Hivi karibuni, kumefanyika Jukwaa la Vijana Kimataifa. Huu ni mwendelezo wa tafakari ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa kumpatia nafasi Roho Mtakatifu kuendelea kuwatumia vijana katika maisha na utume wa Kanisa. Hii imekuwa ni fursa ya kufanya mang’amuzi ya kijumuiya, kwa kuendelea kujikita katika dhana ya Sinodi na ari ya kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa. Ulimwengu umegubikwa na kinzani na migawanyiko mbali mbali inayodumaza mchakato wa ujenzi wa umoja, upendo, mshikamano na urafiki kati ya watu. Vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja, upendo na mshikamano duniani. Mama Kanisa anawatambua vijana kuwa ni wadau wakuu wa mchakato mzima wa wongofu wa kichungaji, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018.

Jukwaa la Vijana Kimataifa, hivi karibuni limepata fursa ya kusali, kutafakari na kushirikishana mang’amuzi ya maisha, kielelezo cha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana Jukwaa la Vijana Kimataifa linaratibiwa na Baraza la Walei, Familia na Maisha Jukwaa hili mwaka huu liliwakutanisha zaidi ya vijana 350 kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni, wakiwemo watanzania wawili yaani: Flavian Jacob Rweyungura na Happiness Mbepera, nalo lilijikita katika kutafakari utekelezaji wa maazimio ya Sinodi ya Maaskofu mwaka 2018 mintarafu vijana iliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang'amuzi ya miito”. Jukwaa hilo lilianza kwa siku tatu za majadiliano na tafakari husika hasa na mwamko wa Kanisa na zaidi vijana katika kuyaishi yatokanayo na safari nzima ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, hususan Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, uliozinduliwa rasmi tarehe 2 Aprili 2019.

Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito”. Huu pia ni mwendelezo wa mchakato wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, kwani utume wa Kanisa kwa familia na vijana ni sawa na chanda na pete; unategemeana na kukamilishana! Tukio hili lilihitimishwa na hija katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Vatican ambako ilifanyika pia misa takatifu ikiongozwa na Kardinali Kevin Joseph Farrell Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Katika mahubiri yake Baba Kardinali Farrell aliwaasa vijana kuimarisha mahusiano binafsi na Mungu ili kuweza kuwa mashuhuda wa kweli wa kuitangaza injili kwa maneno na matendo mema. Kardinali alikazia kusema ulimwengu wa leo umechoka kuhubiriwa kwa maneno matupu pasipo matendo halisi.

Akitumia mfano wa Mtakatifu Paulo aliyeongoka na kubadili mwenendo wake kwa sababu alikutana na Yesu, amewasii vijana hasa wakristo waliokutana na Yesu kupitia sakramenti ya Ubatizo, kujitanibu  katika kuonesha imani yao kwa matendo mema kwa kuwa siku zote kukutana na Yesu kunabadilisha maisha na kuyapa sura mpya katika uzima. Zaidi amewakumbusha vijana kufuasa mfano wa Kristo Yesu mwenyewe ambaye katika ujana wake amethibitisha upendo wake kwa watu wote, akakubali kutimiza mpango wa ukombozi ulimwengu kwa mateso, kifo na ufufuko wake; na sasa Yu hai kweli na yuko nasi akiendelea kutualika kuenenda katika unyofu wa maisha katika kumtafuta Mungu. Kardinali Farrell alimaliza kwa kuwahimiza vijana kuguswa na mfano wa watakatifu Yohane Fisher na Tomaso Moro ambao licha ya rabsha za watawala wa ulimwengu wa kipindi chao walibaki imara katika imani na hata wakafa mashahidi.

Sanjari na hija na Misa Takatifu, vijana walioshiriki Jukwaa la Kimataifa la Vijana mwaka huu walipata fursa ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko katika ukumbi wa Clementina katika viunga vya Vatican. Katika ujumbe wake kwa vijana hawa Baba Mtakatifu Francisko aliwahimiza kutambua kwamba ulimwengu unawahitaji. Aliwaasa vijana kuendelea kukaza mwendo katika jitihada za uinjilishaji katika nafasi yao kama vijana. Alikazia kusema kwamba vijana hawapaswi kusimama, wakizubaa na kudorora bali kuchangamka kuendelea kukaza mwendo, kutembea ndani ya Kanisa linalotembea pia. Baba Mtakatifu aliwataka vijana kuwa wahusika (protagonists) kwelikweli wa wongofu wa utume wa vijana katika Kanisa. Baba Mtakatifu aliona pia kwamba kuhititmisha tukio la Jukwaa la vijana katika siku inayotangulia Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, kunaendana kwa dhati na roho ya Mababa wa Sinodi ya mwaka 2018

Mababa wa Sinodi waliona kwamba simulizi la wanafunzi wa Emmaus katika Injili ya Luka (Lk 24:13-35) linasadifu vyema uelewa wa utume wa Kanisa kwa vijana (Hati ya Sinodi no 4); kwani simulizi hilo linaeleza kwamba wanafunzi walimtambua Yesu baada ya kuketi nao chakulani; alipouchukua mkate, akaubariki, akaumega na kuwapatia. Ndipo wanafunzi wale walipata mwanga na ushujaa wa kuanza safari ya kuwatangazia wengine habari njema. Hivyo Baba Mtakatifu aliwaalika vijana kuwa mwanga wa ulimwengu, aliwahimiza kuchota nguvu katika sadaka ya Ekaristi Takatifu ambayo ni asili na kilele cha maisha ya kikristo (LG 11). Vilevile vijana walisisitizwa juu ya umuhimu wa umoja. Baba Mtakatifu alikazia kusema, ulimwengu wetu wa leo umegubikwa na migawanyiko na migogoro kadha wa kadha inayokwamisha maendeleo na kushusha hadhi ya utu wa binadamu.

Baba Mtakatifu aliwaita vijana leo ya Mungu na leo Kanisa. Vijana wanapaswa kujitahidi kuwa na umoja ili kuweza kutembea pamoja kwa sababu tunakutana na Kristo kwa namna fanisi katika jumuiya. Katika kuwashirikisha wengine juu ya mahusiano binafsi na Yesu ndipo tunaweza kuonja zaidi uwepo wake mioyoni mwetu na kati yetu, alikazia kusema. Kabla Baba Mtakakatifu hajawabariki vijana hao, kupiga nao “selfie” na kuwaaga, alitoa tangazo muhimu. Kwamba kwa maadhimisho ya siku ya vijana ulimwenguni mwaka 2022 ambayo yatafanyika huko Lisbon nchini Ureno, yataongozwa na kauli mbiu ''Maria akainuka na kwenda kwa haraka'' Injili ya Luka 1:39 . Vilevile kwa miaka miwili ijayo kuelekea siku ya vijana ijayo mjini Lisbon nchini Ureno, amewataka vijana kutumia muda kutafakari juu ya mistari hii miwili kutoka katika Maandiko Matakatifu; ''kijana nakuamuru amka'' (Lk 7:14; Christus vivit, 20) na pia ''Inuka sasa, simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu'' (Mat 26:16).

Baba Mtakatifu ametaka sehemu hizi mbili za Maandiko Matakatifu ziwe kama “kitafunwa safarini” katika tafakari kuelekea siku ya vijana duniani mwaka 2022 na vilevile mwendelezo wa safari  baada ya sinodi. Khalifa wa Mtakatifu Petro amewapatia vijana zawadi hiyo ya rejeo la tafakuri kwa mwaka 2020, mwaka 2021 na mpaka hapo watakapokutana naye tena kwa pamoja mnamo mwaka 2022, Mungu akipenda!

Jukwaa la Vijana

 

22 July 2019, 09:21