Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ameiandikia familia ya Mungu nchini Ujerumani barua maalum akiitaka kujikita katika utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko ameiandikia familia ya Mungu nchini Ujerumani barua maalum akiitaka kujikita katika utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. 

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu Ujerumani

Baba Mtakatifu anatambua hali ngumu ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani. Anaunga mkono jitihada zinazoendelea kufanyika hadi wakati huu! Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kama ambavyo imeshuhudiwa wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani uliofanyika mwezi Machi 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu, kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji! Baba Mtakatifu katika barua yake kwa familia ya Mungu nchini Ujerumani, anasihi Maaskofu kushikamana na kutembea kwa pamoja kama ndugu na kamwe asiwepo mtu anayetembea pweke pweke, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Roho Mtakatifu, aweze kupyaisha maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hiki ni kipindi cha mabadiliko makubwa yanayoibua matatizo na changamoto mpya na zile za zamani, mwaliko kwa familia ya Mungu kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu anatambua hali ngumu ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani, ndiyo maana ameamua kuwaandikia ujumbe huu, ili kuunga mkono jitihada zinazoendelea kufanyika hadi wakati huu! Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kama ambavyo imeshuhudiwa wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani uliofanyika mwezi Machi 2019. Mkutano huu uliwajumuisha: Maaskofu, wakleri, watawa, wajumbe kutoka kwa waamini walei, wataalam na mabingwa wa mambo mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa.

Wote hawa kwa pamoja wakajadili na hatimaye kupitisha mbinu mkakati wa kupambana  na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini Ujerumani. Umuhimu wa utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani ni matunda ya utafiti na upembuzi yakinifu uliofanywa na Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, DBK, inayowahusisha wawakilishi wa makundi mbali mbali ya familia ya Mungu nchini Ujerumani. Tume hii pamoja na mambo mengine, ilidadavua kwa kina na mapana kuhusu uwepo wa idadi kubwa ya waamini wenye umri mkubwa ndani ya Kanisa Katoliki, ikilinganishwa na idadi ya vijana wanaobatizwa kila mwaka. Tume hii ilipembua pia kuhusu kupungua kwa idadi ya miito ya kitawa na kipadre nchini Ujerumani, mafundisho tenge kuhusu tendo la kujamiiana au kama wanavyofahamu wengi, tendo la ndoa.

Tume iligusia pia hali na mtindo wa maisha na utume wa Mapadre nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu anasema, hana sababu msingi ya kuzama tena katika tafiti hizi, bali anapenda kujielekeza zaidi kwa kuchangia hoja zake katika maisha ya kiroho zaidi, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya. Kumbe, kipaumbele cha kwanza katika majadiliano haya yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kilenge kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa nchini Ujerumani. Familia ya Mungu nchini Ujerumani iendelee kujiweka chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu kwani historia inafundisha kwamba, pale ambapo Jumuiya ya waamini ilijiangalia yenyewe na kutaka kutatua matatizo na changamoto zake kwa kutumia nguvu zake yenyewe; mbinu na akili zake, imejikuta ikikuza na kuendeleza matatizo yaliyokuwa yanapaswa kupewa ufumbuzi wa kudumu.

Baba Mtakatifu anaikumbusha familia ya Mungu nchini Ujerumani kwamba, inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika umoja na utofauti; hii ni familia yenye ukarimu, inayojituma na kuwajibika barabara. Jambo la msingi ni kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Kuna hatari kubwa kwa waamini wengi kuendelea kukengeuka kutokana na kutopea kwa imani pamoja na kumong’onyoka kwa kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu; mambo ambayo athari zake zimeanza kutikisa misingi ya maisha ya kijamii na kitamaduni; changamoto ambayo haina majibu ya mkato! Baba Mtakatifu anakazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani kwa kuwashirikisha watu wa Mungu katika ngazi mbali mbali na baada ya sala, tafakari na majadiliano ya kina, matunda ya Sinodi yanarejeshwa tena miongoni mwa familia ya Mungu kwa utekelezaji unaowawajibisha wote; ili kuweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ipewe kipaumbele cha pekee nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu katika barua hii, anakazia umuhimu wa imani inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa nchini Ujerumani liendelee kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari kama sehemu ya mbinu mkakati wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ndani na nje ya Ujerumani. Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili uendelee kuimarishwa, ili kutoa utambulisho kwa waamini kwamba, wao ni sehemu ya watu wa Mungu wanaendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kuukumbatia utakatifu wa maisha!

Kamwe watu wa Mungu nchini Ujerumani wasitafute njia ya mkato, jambo ambalo ni kishawishi kikubwa kwa wakati huu; wawe makini wasitumbikie katika kishawishi hiki, kwani hakitaweza kuwaacha salama! Ujasiri na umakini wa kutekeleza sera na mikakati iliyoibuliwa kwa muda muafaka ni jambo la kukazia sana. Isiwachukue muda mrefu kutekeleza yale ambayo yameamriwa! Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni dira na mwongozo wa sera makini badala ya kutumbukia kwenye kishawishi cha kutaka kutekeleza matakwa ya baadhi ya makundi ya watu nchini Ujerumani. Mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa hauna budi kufumbata chachu na tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kimaadili; kwa kutambua kwamba, wao ni waamini wa Kanisa Katoliki.

Hapa kuna hja ya kuzama katika wongofu wa shughuli za kichungaji, kama dira na mwongozo wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa watu wa Mungu. Roho Mtakatifu awalinde na kuwaongoza watu wa Mungu nchini Ujerumani katika majadiliano yao ili kuwa na mwelekeo sahihi wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, vinginevyo, Sinodi pia inaweza kutumiwa vibaya na kuweza kusababisha kinzani na mipasuko miongoni mwa watu wa Mungu nchini humo. Kanisa linapaswa kuendeleza utume wake wa kinabii nchini Ujerumani, kwa kusaidia kuinjilisha na kutamadunisha maisha ya watu wa Mungu, ili hatimaye, waweze kupata maisha na uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, upyaisho wa kweli wa maisha na utume wa Kanisa unafumbatwa katika ujenzi wa utamaduni wa kukutana na wengine katika huduma hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni wakati wa kukuza na kudumisha Injili ya uhai, upendo na mshikamano dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya watu wengine! Ni vyema ikiwa kama familia ya Mungu nchini Ujerumani itaondokana kabisa na tabia ya maamuzi mbele na chuki dhidi ya wageni na wahamiaji nchini humo! Baba Mtakatifu anaendelea kukazia umuhimu wa utambuzi wa Kikanisa “Sensus Ecclesiae” katika utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ili wote waweze kutembea kwa pamoja na katika umoja.

Changamoto changamani ni pevu sana. Kuna maswali yanayoibuliwa na kamwe hayawezi kufumbiwa macho, bali kushughulikiwa, kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa ukweli wa mambo nchini Ujerumani. Kanisa lijenge na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza hasa maskini, wadogo na wanyonge ndani ya jamii. Katika hija hii ya Kanisa kama sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo,  hata katika tofauti zao, waamini wajiweke chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Kristo Yesu anawaonesha njia ya Heri za Mlimani kama dira na mwongozo wa maisha mapya!

Papa: Ujerumani
01 July 2019, 15:43