Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Mgogoro wa kivita Ukraine: Mambo msingi: Sala na Maisha ya kiroho; Shuhuda wa matumaini ya Kikristo; Ukaribu kwa watu wa Mungu & Dhana ya Sinodi katika utume wa Kanisa. Papa Francisko: Mgogoro wa kivita Ukraine: Mambo msingi: Sala na Maisha ya kiroho; Shuhuda wa matumaini ya Kikristo; Ukaribu kwa watu wa Mungu & Dhana ya Sinodi katika utume wa Kanisa.  (Vatican Media)

Papa: Vita Ukraine: Sala, Faraja, Matumaini, Ukaribu & Sinodi!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake elekezi amekazia umuhimu wa sala na maisha ya kiroho kama chemchemi ya faraja kutoka kwa Mungu; Kanisa liendelee kuwa ni shuhuda wa matumaini ya Kikristo kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; Kanisa lioneshe ukaribu kwa watu wanaoteseka sanjari na kuendelea kukazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameamua kumuita Askofu mkuu, wajumbe wa kudumu wa Sinodi pamoja na Maaskofu wakuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine, ili kukutana kwa pamoja mjini Roma kuanzia tarehe 5-6 Julai 2019. Viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican wanaohusika na eneo hili wanashiriki pia. Mkutano huu ni alama ya uwepo na mshikamano wa karibu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Ukraine. Mkutano huu ni fursa makini ya kuweza kufanya upembuzi yakinifu kuhusu: hali ya maisha na mahitaji halisi ya Ukraine kwa wakati huu, kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kanisa linataka kuchangia kwa hali na mali, ili kuwasaidia wale wote wanaoteseka kutokana na vita, kwa kushirikiana na Makanisa pamoja na Jumuiya mbali mbali za Kikristo, kielelezo cha uekumene wa huduma ya Injili na mshikamano wa upendo kwa maskini!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake elekezi kwa viongozi wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine amekazia umuhimu wa sala na maisha ya kiroho kama chemchemi ya faraja kutoka kwa Mungu; Kanisa liendelee kuwa ni shuhuda wa matumaini ya Kikristo kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; Kanisa lioneshe ukaribu kwa watu wa Mungu wanaoteseka na kwamba, kuna haja ya kuendelea kukazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Ukraine katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imejikuta ikitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe; vita ambayo imepelekea wananchi wa kawaida kulipa gharama kubwa. Hii ni kampeni inayochochea vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kisiasa na hata kidini. Lakini katika yote haya, watambue kwamba, daima ameendelea kuwabeba na kuwahifadhi katika sakafu ya moyo wake kwa njia ya sala na sadaka yake ya kila siku.

Papa anawashukuru na kuwapongeza kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, dhamana na utume ambao umewagharimu sana wakristo nchini Ukraine kama historia inavyoshuhudia! Baba Mtakatifu anawaombea kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Baba wa rehema na Mungu wa faraja yote ili awafariji katika dhiki yao. Anawaombea wanasiasa ili waweze kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha: ustawi, mafao ya wengi na amani ya kudumu. Mungu wa faraja zote awafariji wale wote waliogusa na kutikiswa na vita hii ambayo imewandolea ndugu zao; imewasababishia madonda makubwa: kiroho na kimwili, kiasi hata cha makundi makubwa ya watu kuikimbia nchi yao. Kila siku anawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.

Katika shida na mahangaiko ya watu kutokana na vita pamoja na madhara yake, Kanisa linapaswa kuwa ni shuhuda wa matumaini ya Kikristo, msingi wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati na kwamba, haya ni matumaini ambayo hayadanganyi kamwe! Watambue kwamba, wamehesabiwa haki, wamepatanishwa na kuokolewa na Mungu. Katika dhidi na mahangaiko waendelee kuwa na matumaini, saburi na uthabiti wa moyo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Matumaini ya Kikristo ni chemchemi ya ufufuko, maisha na mwanzo mpya! Katika shida, hali na mazingira magumu na hatarishi kama haya, waamini wajifunze daima kuwa karibu sana na Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini yao.

Huu ni umoja, mshikamamo na mafungamano yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo na kusimikwa katika imani, historia na shuhuda mbali mbali zinazotolewa na watakatifu ambao ni majirani zao. Watu wa Mungu nchini Ukraine wamejifunza kulipa ubaya kwa wema! Hawa ni watu wenye ushupaji na ushujaa kwa Kikristo kama unavyobainishwa kwenye Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Kristo Yesu kwa waja wake. Wamejifunza kuwapenda na kuwaombea adui zao, huku wakijichotea nguvu kutoka katika Fumbo la Msalaba. Ni watu ambao wameteseka, wakanyanyasika na kuuwawa kikatili, lakini hawa ndio waliovikwa taji ya ushindi kama mashuhuda wa Kristo Yesu, kwa kuandika kurasa chungu za imani, matunda ya mbegu ya matumaini ya Kikristo!

Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji inaongozwa na kauli mbiu “Parokia hai, ni mahali muafaka pa kukutana na Kristo aliye hai”. Katika mukadha huu, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu umuhimu wa Parokia kuwa ni mahali muafaka pa kukutana pa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Parokia iwe ni mahali pa kusikiliza Neno la Mungu, kuimarisha maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma kama kielelezo cha imani tendaji na Majiundo endelevu katika imani. Hapa ni mahali pa kujenga na kudumisha Injili ya amani na ujasiri wa kusonga mbele bila ya kukata tamaa. Waamini waendelee kuchota amana na utajiri wa maisha ya Kiroho, ili kuliwezesha Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa!

Baba Mtakatifu anakazia sala na maisha ya kiroho, ili kuwasaidia waamini kumkimbilia Kristo Yesu na Kanisa lake, ili awawezeshe kuwa watakatifu na bila mawaa mbele ya Mungu, tayari kuwatakatifuza jirani na ndugu zao. Waamini wawe ni watu wa kukesha na kusali ili wasitumbukie katika kishawishi cha usaliti kama ilivyokuwa kwa Yuda Iskarioti. Sala ni jibu makini ambalo Kristo Yesu anasubiri kutoka kwa waja wake, kama jibu makini linalopania kuzima vita, kinzani na misigano mbali mbali ya maisha! Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutekeleza utume wake wa shughuli za kichungaji kwa kuwa karibu na kati ya watu wa Mungu, kwa kusali pamoja nao wakati wa shida na magumu ya maisha. Ni kwa njia hii, viongozi wa Kanisa wanajenga mahusiano na mafungamano na waamini wao na kwa njia ya huduma makini, wanaweza kumwilisha pia Habari Njema katika uhalisia wa maisha yao, kutokana na ushuhuda wa viongozi wao wa Kanisa.

Wawe ni mashuhuda wa ukaribu na uwepo wa Mungu, chemchemi ya matumaini kwa waja wake. Kanisa ni mahali ambamo waamini wanajichotea Injili ya matumaini, mahali wanapofarijika na kutiwa shime kusonga mbele kwa imani na moyo mkuu. Kanisa ni mahali pa kusikiliza kwa makini shida na mahangaiko ya watu, bila kuwageuzia kisogo! Sala na Maisha ya kiroho, yaboreshwe pia kwa njia ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu, chemchemi ya upendo, mahali pa kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu ili kusaidiana kwa hali na mali. Si mwelekeo mwema kuwasahau ndugu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali anasema Baba Mtakatifu Francisko. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni utambulisho wa Kanisa kama Jumuiya ya waamini wanaotembea kwa pamoja.

Sinodi ni mahali pa majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya viongozi wa Kanisa na waamini walei. Dhana ya Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa kila siku, kwa kuwahusisha waamini wote hata wale wenye mawazo na maoni tofauti! Dhana ya Sinodi inakita mizizi take katika kusikilizana na kuheshimiana. Kwa kuwajibika barabara, ili kusaidiana, kurekebishana kidugu na kutiana moyo ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu na tayari kutembea katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo ambao unalitegemeza Kanisa unapaswa daima kusimikwa katika ukweli na uwazi na kwamba, waamini walei wanapaswa kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa, huku wakiendeleza mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Waamini walei, wakaribishwe na kupewa nafasi ya kusikilizwa!

Dhana ya Sinodi inamhusisha hata Mwenyezi Mungu pamoja na kutazama mahitaji msingi ya Kanisa la Kiulimwengu. Hii ni changamoto ya kushirikisha amana na utajiri wa kitaalimungu na kiliturujia. Kanisa la Ukaraine likuze na kudumisha uhusiano na mafungamano na Mabaraza ya Kipapa, ili kuimarisha umoja wa Kanisa la Kristo na kulipatia Kanisa utambulisho wake wa Kikatoliki. Mwishoni mwa hotuba yake elekezi, Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni fursa ya kusikilizana, kujadiliana katika msingi ya ukweli na uwazi, daima waktafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi mintarafu mwanga wa Injili pamoja na kutembea kwa pamoja katika umoja. Huu ni muda wa mang’amuzi ya pamoja kama Kanisa, kwa kukazia sala na maisha ya kiroho; kwa kukuza na kudumisha ukaribu wa Mungu kwa waja wake, lakini zaidi, kwa wale wanaoteseka. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, iwawezeshe kutembea kwa pamoja katika ukweli na uwazi; katika upole na unyenyekevu wa moyo.

Papa Ukraine
05 July 2019, 15:53