Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko: Watakatifu wapya watatangazwa rasmi tarehe 13 Oktoba 2019 wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu Francisko: Watakatifu wapya watatangazwa rasmi tarehe 13 Oktoba 2019 wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia. 

Papa Francisko: Watakatifu wapya kutangazwa rasmi 13 Oktoba 2019

Papa Francisko, tarehe Mosi, Julai, 2019 ameongoza Baraza la Makardinali kwa njia ya sala na hatimaye, kuwapigia kura Wenyeheri watano watakaotangazwa kuwa watakatifu, tarehe 13 Oktoba 2019. Watakatifu watarajiwa ni pamoja na: Kardinali John Newman, Giuseppina Vannini; Maria Theresa Chiramel Mankidiyan, Sr. Dulce Lopes Pontes pamoja na Margarita Bays! Mifano bora ya kuigwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa ni Takatifu kwa maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu anayetangazwa pamoja na Baba na Roho Mtakatifu kwamba ni peke yake mtakatifu, amelipenda Kanisa kama Bibi arusi wake, akajitoa mwenyewe kwa ajili yake ili alitakatifuze, akaliunganisha naye kama mwili wake, akalijazia kipaji cha Roho Mtakatifu, kwa utukufu wa Mungu! Kumbe, watu wote wa familia ya Mungu wanaitwa kuwa ni watakatifu! Haya ndiyo mapenzi ya Mungu. Kristo Yesu ndiye chemchemi na utimilifu wa utakatifu wote! Waamini wanahimizwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu na wawe na matunda ya Roho Mtakatifu ili wafanywe watakatifu. Kutokana na udhaifu wa binadamu, waamini wanahitaji mara kwa mara kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kudadavua kuhusu Fumbo la Kanisa kwa kusema, Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kushiriki utakatifu mmoja, kwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli; kwa kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa ni: mtii, fukara na mnyenyekevu wa moyo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa njia hii, wastahilishwe kushiriki utukufu wa Kristo! Upendo wa dhati ni njia inayoweza kuwapeleka waamini katika utakatifu! Wanapaswa pia kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; wajitahidi kushiriki mara kwa mara Sakramenti za Kanisa; kwa kujitia uthabiti katika kusali, kujinyima pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe Mosi, Julai, 2019 ameongoza Baraza la Makardinali kwa njia ya sala na hatimaye, kuwapigia kura Wenyeheri watano watakaotangazwa kuwa watakatifu, tarehe 13 Oktoba 2019 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Watakatifu watarajiwa ni pamoja na Kardinali John Newman, muasisi wa Kituo cha Michezo cha Mtakatifu Filippo Neri, nchini Uingereza. Maisha ya Kardinali John Newman yalikuwa ni hija kuelekea ukweli mkamilifu. Alizaliwa kunako mwaka 1801, akawekwa wakfu kuwa Shemasi, Kanisa Anglikani. Baada ya tafakari ya kina na ya muda mrefu, akaongokea kwenye Kanisa Katoliki na Mwaka 1847 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, akateuliwa kuwa Kardinali na Papa Leo XIII na kufariki dunia kunako mwaka 1890.

Hii ni changamoto kwa waamini kuutafuta na kuuambata ukweli unaowaweka huru, ingawa una gharama zake. Ni kiongozi aliyejibidiisha kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo kwa wagonjwa, maskini pamoja na wafungwa gerezani. Maisha na wito wa kila Mkristo ni kuambata utakatifu wa maisha. Sr. Giuseppina Vannini, Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Camillus aliyezaliwa kunako mwaka 1859 mjini Roma, akapata malezi makini kutoka katika familia ya Kikristo. Akiwa na umri wa miaka 32, kunako mwaka 1891 akajiunga na maisha ya kitawa, baada ya safari ndefu ya maisha ya kiroho, mwaka 1892 akaanzisha Shirika na kukubaliwa na Kanisa kunako mwaka 1909, baada ya changamoto nyingi. Tarehe 23 Februari 1911 akafariki dunia na kuacha Shirika lake likiwa na watawa 156. Tarehe 16 Oktoba 1994, akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mwenyeheri.

Maria Theresa Chiramel Mankidiyan, Muasisi wa Shirika la Watawa wa Familia Takatifu aliyezaliwa kunako mwaka 1876. Alipata malezi makini kutoka kwa Mama yake na katika ujana wake, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, wagonjwa pamoja na kutoa hifadhi kwa watu ambao hawa kuwa na makazi maalum. Akajaliwa neema ya kuwa na maono, akapata mang’amuzi ya Madonda Matakatifu mwilini wake, na hatimaye, akabahatika kuanzisha Shirika la Watawa wa Familia takatifu kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa waliokuwa kufani pamoja na elimu na majiundo makini kwa wasichana wa kizazi kipya. Akafanikiwa kuliongoza Shirika kwa kipindi cha miaka 12. Akafariki dunia kunako mwaka 1926 na kutangazwa Mwenyeheri na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000.

Sr. Dulce Lopes Pontes wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mama wa Mungu, alizaliwa kunako mwaka 1914, akiwa na umri wa miaka 18 alijiunga na Shirika la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mama wa Mungu. Alivutiwa sana na maisha na wito wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Akasaidia sana kuunda umoja wa wafanyakazi wa Mtakatifu Francisko, ili kuwasaidia wafanyakazi waliokuwa wanakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha. Kunako mwaka 1959 akaanzisha Hospitali kama kielelezo cha huduma ya upendo. Akafariki dunia kunako mwaka 1992. Ni mtawa ambaye alikita maisha yake katika sala iliyomwilishwa kwenye huduma ya upendo kwa wagonjwa, kiasi kwamba, upendo wake, ukavunjilia mbali kuta zilizokuwa zinawatenganisha watu! Leo hii amekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika uchaji na utakatifu wa maisha!

Margarita Bays, Bikira na mtawa wa Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, alizaliwa kunako mwaka 1815. Katika maisha yake alikuwa ni mshonaji, dada wa nyumbani na katekista, akabahatika kupata Madonda Matakatifu mwilini wake. Kwa muujiza, akaponeshwa saratani ya tumbo tarehe 8 Desemba 1854 wakati Papa Pio IX alipokuwa anatangaza kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mungu Mwenyezi, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Akafariki dunia katika hali ya neema kunako mwaka 1879. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mwenyeheri kunako mwaka 1995.

Wenyeheri hawa wanatarajiwa kutangazwa kuwa Watakatifu tarehe 13 Oktoba 2019 wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali:kuhusu: haki jamii, malezi awali na endelevu, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Watakatifu wapya, wanawekwa mbele ya macho ya watu wa Mungu kama mfano na kielelezo cha kufuatwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Papa: Kard. Newman
01 July 2019, 16:17