Tafuta

Uchumi wa Francisko 26-28 Machi 2020: Vijana wanaalikwa kuanza kujisajili na mwisho ni tarehe 30 Septembe 2019. Uchumi wa Francisko 26-28 Machi 2020: Vijana wanaalikwa kuanza kujisajili na mwisho ni tarehe 30 Septembe 2019. 

Mkutano wa Uchumi wa Francisko: Usajili waanza, vijana changamkeni

Tayari wachumi mashuhuri wameanza kujisajili ili kuweza kushiriki katika mpango mkakati wa “Uchumi wa Francisko”. Tangu sasa vijana ambao wamehamasika kutokana na mwaliko wa Baba Mtakatifu wanaweza kuanza kujiandikisha kuanzia sasa na mwisho wa kujisajili ni tarehe 30 Septemba 2019. Vijana wanaweza kujisajili kwa anuani ifuatayo: www.francescoeconomy.org.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni tukio ambalo linatarajia kuwakusanya wachumi na wajasiriamali wachumi vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuanzia tarehe 26 - 28 Machi 2020 huko Assisi, nchini Italia. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, unaotekelezwa kwa namna ya pekee, na Baba Mtakatifu Francisko. Hii itakuwa ni nafasi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kukutana na kuzungumza na vijana wanaojifunza uchumi unaotekelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu!  Baba Mtakatifu anataka kuzama zaidi katika uchumi unaouhisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika utamaduni wa kifo. Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu, heshima na haki msingi za binadamu; uchumi unaokita mizizi yake katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Tayari wachumi mashuhuri wameanza kujisajili ili kuweza kushiriki katika mpango mkakati wa “Uchumi wa Francisko”. Vijana wanaolengwa hapa ni wale wasiozidi umri wa miaka 35. Tangu sasa vijana ambao wamehamasika kutokana na mwaliko wa Baba Mtakatifu wanaweza kuanza kujiandikisha kuanzia sasa na mwisho wa kujisajili ni tarehe 30 Septemba 2019. Vijana wanaweza kujisajili kwa anuani ifuatayo: www.francescoeconomy.org. Tayari washindi wa tuzo ya Nobeli wamekwisha kujisajili kati yao ni Muhammad Yunus na Amarthya Sen. Wengine ni Bruno Frey, Tony Meloto, Carlo Petrini, Kate Raworth, Jeffrey Sach, Vanda Shiva pamoja na Profesa Stefano Zamagni. Itakumbukwa kwamba,  hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko alimteua Profesa Stefano Zamagni, kuwa Rais wa Taasisi za Kipapa za Sayansi Jamii.

Profesa Stefano Zamagni ni mwanachama wa Taasisi mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa kuhusiana na masuala ya mchakato wa kupambana na balaa la umaskini duniani, sera na mikakati ya uchumi endelevu na fungamani ya binadamu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Argentina. Profesa Zamagni ni mtaalam aliyebobea katika masuala sera za uchumi kimataifa, kanuni maadili na sheria za uchumi; nadharia za ulaji, maamuzi ya kijamii pamoja na nadharia mbali mbali za uchumi. Amechapisha vitabu na Makala nyingi kuhusiana na mada hizi, kitaifa na kimataifa! Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii, ikisaidiwa na wataalam katika sekta hii imeweza kuona uhusiano wa karibu uliopo kati ya Ukristo na haki msingi za binadamu; umuhimu wa kulinda na kuheshimu haki hizo; kwa kukazia haki ya maisha, tunu msingi za maisha ya kifamilia, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini na dhamiri na haki ya mtu kuishi vizuri.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kukuza na kudumisha utandawazi wa mshikamano, haki na amani. Kumbe, kwa kuheshimu utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kujikita katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mambo msingi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa! Hili ni kongamano ambalo linapania kuonesha jinsi nadharia inavyoweza kumwilishwa katika matendo, ili kukuza ari na mwamko wa utamaduni wa watu kukutana, kufahamiana na kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Itakuwa ni fursa ya kusimama, kukaa kimya na kutafakari shuhuda mbali mbali zitakazokuwa zinatolewa ili kusaidia kujenga nadharia ya mfumo mpya wa uchumi fungamani. Vijana wanaohamasishwa kushiriki ni wale wanaosoma kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, wanaofanya tafiti zao katika masuala ya kiuchumi.

Mwaliko huu unawahusu hata vijana wafanyabiashara na wale ambao wamebahatika katika ujana wao kuwa ni viongozi katika masuala ya kiuchumi. Baba Mtakatifu anawaalika pia vijana wenye ushawishi mkubwa katika masuala ya uchumi fungamani ili kushirikisha pia uzoefu na mang’amuzi yao, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uchumi wa Francisko pamoja na mambo mengine unapania kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani na mshikamano, ili wale watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa wakati huu, wajengewe uwezo wa kusimamia uchumi ambao ni fungamani, kwani unagusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni uchumi unaotoa fursa kwa kila mtu kushiriki kikamilifu katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si uchumi unaomilikiwa na kuendeshwa na watu wachache tu ndani ya jamii!

Kwa vijana wote watakaotuma maombi yao, jopo la kongamano hili, litawachagua vijana 500 watakaoshiriki maandalizi ya tukio hili hapo tarehe 24-25 Machi 2020. Kongamano lenyewe litaendelea rasmi kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 26 – 28 Machi 2020. Ni matumaini ya Kanisa Barani Afrika kwamba, kutakuwepo na ushiriki mkubwa katika kongamano hili! Huu ni wakati wa kuchangamkia fursa zinapojitokeza!

Uchumi wa Francisko
27 July 2019, 15:44