Tafuta

Vatican News
Papa Francisko ameiandikia barua Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiislam kutoka Israeli inayoishi nchini Argentina: Kumbu kumbu ya Miaka 25 ya Shambulio la kigaidi nchini Argentina! Papa Francisko ameiandikia barua Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiislam kutoka Israeli inayoishi nchini Argentina: Kumbu kumbu ya Miaka 25 ya Shambulio la kigaidi nchini Argentina!  (ANSA)

Papa Francisko: Shambulio la Kigaidi Argentina Miaka 25 Iliyopita

Ilikuwa ni tarehe 18 Julai 1994, Miaka 25 iliyopita, “Associazione Mutualità Israelita in Argentina, AMIA”Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiislam kutoka Israeli, inayoishi nchini Argentina, iliposhambuliwa kwa vitendo vya kigaidi na kusababisha watu 85 kufariki dunia na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa vibaya. Papa Francisko analikumbuka tukio hili kwa huzuni na majonzi makubwa moyoni mwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vitendo vya kigaidi ni ukweli ambao unaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao; kiasi hata cha watu kukosa amani na utulivu wa ndani, kwa kuendea kuishi katika hofu na wasi wasi wa kushambuliwa. Vitendo hivi vimeharibu urithi mkubwa wa utamaduni, utambulisho wa watu pamoja na historia yao. Hadi sasa Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Vitendo vya kigaidi ni unyama dhidi ya: maisha, utu na heshima ya binadamu. Huu ni uhalifu dhidi ya binadamu na haki zake msingi. Vitendo vya kigaidi vinahatarisha usalama, maisha, mafungamano ya kijamii pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu. Hivi ni vitendo vinavyokwenda kinyume na uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini sanjari na umuhimu wa kutunza dhamiri nyofu! Vitendo vya kigaidi vinapaswa kulaaniwa na kushutumiwa na viongozi wa kidini pamoja na Jumuiya ya Kimataifa bila “kupepesa pepesa macho”.

Ilikuwa ni tarehe 18 Julai 1994, Miaka 25 iliyopita, “Associazione Mutualità Israelita in Argentina, AMIA”Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiislam kutoka Israeli, inayoishi nchini Argentina, iliposhambuliwa kwa vitendo vya kigaidi na kusababisha watu 85 kufariki dunia na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu Francisko analikumbuka tukio hili kwa huzuni na majonzi makuu na kwamba, mawazo, sala na sadaka yake anapenda kuielekeza kwa wale wote waliopoteza maisha katika tukio hili la kigaidi, bila kujali dini wala imani zao, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, tofauti zao msingi ni utajiri na amana kubwa inayopaswa kuendelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe hazipaswi kutumiwa kwa ajili ya kujenga chuki, uhasama, kinzani, mipasuko na vita!

Baba Mtakatifu katika barua yake kwa Jumuiya ya Waamini wa dini ya Kiislam kutoka Israeli, inayoishi nchini Argentina, anasema, Kumbu kumbu hii ya Miaka 25 ya Mauaji ya Kigaidi inaamsha tena dhamiri za waamini ili kutambua na kuambata haki na wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha udugu wa familia ya binadamu. Inafahamika wazi kwamba, si dini inayochochea vita, kinzani na mipasuko, bali ni giza katika akili na nyoyo za waamini wenye misimamo mikali wanaofanya vitendo hivi vinavyokwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, tangu siku ile ya kwanza ya shambulio hili la kigaidi, ameendelea kuwakumbuka na kuwaombea, wale wote waliopoteza maisha, ili waweze kupata pumziko la milele katika Makao ya Baba wa mbinguni. Anawakumbuka na kuwaombea pia wale wote waliojeruhiwa katika shambulizi hili ambalo limeacha alama ya kudumu katika maisha yao.

Kitendo hiki cha kigaidi kilisababisha madhara makubwa ndani na nje ya Argentina. Kimsingi, mashambulizi ya kigaidi ni sawa na Vita ya Tatu ya Dunia inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia inayoendelea kurindima vipande vipande! Vitendo vya kigaidi vinatishia maisha ya leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama kati ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa dini mbali mbali duniani kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu, kwa kukuza na kudumisha dhamiri nyofu na uwajibikaji wa pamoja kama ndugu, wito na dhamana kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kila mwamini. Watu wakumbuke kwamba, wameumbwa ili kuishi pamoja na katika umoja kama ndugu. Udugu wa kibinadamu unavuka mipaka ya kijiografia, kidini na kiitikadi.

Udugu huu unakumbatia: umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili kujenga na kudumisha familia kubwa ya binadamu! Misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu ni urithi mkubwa kwa kizazi cha leo na kile kijacho! Binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu wana haki na wajibu sawa na kwamba, wana utu na heshima sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwamba, kusema, bado anawakumbuka wote walioguswa na kutikiswa na shambulio la kigaidi huko Buones Aires, Argentina, Miaka 25 iliyopita!

Papa: Argentina
13 July 2019, 14:53