Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Urussi. Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Urussi.  (ANSA)

Papa akutana na kuzungumza na Rais Putin wa Urussi!

Mazunguko kati ya Papa Francisko na Rais Putin yamefanyika katika hali ya amani na utulivu pamoja na kuridhishwa kwao na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili, ambao umeimarishwa zaidi kwa kutiliana sahihi katika protokali ya ushirikiano kati ya Hospitali ya Bambino Gesu, inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican pamoja na Hospitali za Watoto nchini Urussi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 4 Julai 2019 amekutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Urussi ambaye baadaye, amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Mazunguko kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Rais Putin yamefanyika katika hali ya amani na utulivu pamoja na kuridhishwa kwao na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili, ambao umeimarishwa zaidi kwa kutiliana sahihi katika protokali ya ushirikiano kati ya Hospitali ya Bambino Gesu, inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican pamoja na Hospitali za Watoto nchini Urussi.

Viongozi hawa wamegusia pia kuhusu maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Russia. Baadaye katika mazungumzo yao wamejielekeza zaidi katika masuala ya kiekolojia pamoja na mambo msingi ya kimataifa, hususan hali ya vita nchini Syria, Ukraine na Venezuela. Baba Mtakatifu amemzawadia Rais Putin Ujumbe wa Maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 ulioongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Kwa muhtasari Baba Mtakatifu anakazia Injili ya amani kama sehemu ya utume wa Kanisa; Changamoto za siasa safi; Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi na amani; anagusia kuhusu vilema vya wanasiasa; umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; anasema, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa ujenzi wa amani.

Baba Mtakatifu amemzawadia pia Waraka wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Baba Mtakatifu amemzawadia pia Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Waraka huu unawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Sinodi ya vijana na familia.

Baba Mtakatifu amemzawadia pia Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri. Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.  Raid Vladimir Putin kwa upande wake amemshukuru Baba Mtakatifu kwa mazungumzo yaliyosheheni hekima na busara; pamoja na muda wake. Mazungumzo haya yamedumu kwa takribani  muda wa saa moja! Rais Putin pia amemzawadia Baba Mtakatifu Film.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu Vatican hivi karibuni alisikika akisema, Ziara ya Rais Putin wa Urussi ni muda muafaka kwa Vatican kuweza kujadiliana naye kuhusu mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee kwenye Diplomasia ya Vatican, kwa mfano hali ya Syria na vita huko nchini Ukraine.  Hii ni mnara ya tatu kwa Rais Putin kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Mara ya kwanza, mazungumzo ya viongozi hawa wawili yalifanyika tarehe 25 Novemba 2013. Mkutano huu uligusia masuala ya amani huko Mashariki ya Kati na Syria, jambo ambalo bado limeendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Rais Putin akakutana tena na Papa Francisko 10 Juni 2015: Mchakato wa amani ya kudumu Ukraine na huko Mashariki ya Kati, vikapewa kipaumbele cha pekee kwemnye mazungumzo haya. Jitihada hizi zilianza kuzaa matunda yaliyomwezesha Kardinali Pietro Parolin kuanzia tarehe 21-23 Agosti 1997 kutembelea Urussi, chachu ya kuimarika kwa mahusiano ya kidplomasia kati ya Vatican na Urussi. Kardinali Parolin alibahatika pia kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Kanisa la Kiorthodox, mwanzo mpya wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki. Ilikuwa ni fursa ya kujadili hata yale maswala tete kati ya Makanisa haya mawili, ili kuvuka kuta za kinzani, tayari kuimarisha uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma.

Patriaki Cyrill wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima alikazia umuhimu wa Makanisa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano mintarafu hali tete ya Ukraine. Ushirikiano, mshikamano na ushuhuda wa Injili ya huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji huko Mashariki ya kati ni kati ya mambo ambayo yanaungwa mkono na Makanisa haya mawili. Hizi ni juhudi zinazoimarishwa pia na uekumene wa utakatifu wa maisha unaoyaunganisha Makanisa haya mawili chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari.

Papa: Rais Putin
04 July 2019, 17:29