Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawasihi wahusika wakuu wa mgogoro wa kisiasa nchini Venezuela kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani, ili kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Papa Francisko anawasihi wahusika wakuu wa mgogoro wa kisiasa nchini Venezuela kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani, ili kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Papa Francisko: Mgogoro wa Venezuela: Patateni ili kudumisha: Ustawi na mafao ya wengi!

Papa Francisko anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaangazia wahusika wakuu katika mgogoro wa kisiasa na kijamii nchini Venezuela, waweze kufikia muafaka na hatimaye, kukomesha mateso na mahangaiko ya watu. Uamuzi huu uwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi ndani na nje ya Venezuela.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kufafanua kwa kina na mapana kuhusu Mfano wa Msamaria mwema wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican,Jumapili, tarehe 14 Julai 2019 amesikika akisema kwamba, Wakristo watakuwa wafuasi wa kweli wa Yesu, ikiwa kama watakuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waamini wanakumbushwa kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma; kwani ni kwa njia ya Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani inakuwa ni sheria msingi katika maisha ya kila mwamini.

Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu ameyaelekeza mawazo yake kwa familia ya Mungu nchini Venezuela, ambayo inaendelea kuogelea katika kinzani za kisiasa na kijamii; hali mbaya ya uchumi pamoja na kuandamwa na maafa mbali mbali. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala pamoja na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaangazia wahusika wakuu katika mgogoro wa kisiasa na kijamii nchini Venezuela, waweze kufikia muafaka na hatimaye, kukomesha mateso na mahangaiko yanayoendelea kuwakumba wananchi wa Venezuela. Uamuzi huu uwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Venezuela na Ukanda mzima wa Amerika ya Kusini!

Hivi karibuni, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM, limetuma ujumbe wa umoja, upendo na mshikamano kwa familia ya Mungu nchini Venezuela. Kwa hakika Venezuela inakabiliwa na hali ngumu ya: kisiasa, kiuchumi na kijamii, mambo yanayohatarisha demokrasia shirikishi, utu, heshima, haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. CELAM inaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela kutaka ufanyike uchaguzi utakaowapatia wananchi viongozi halali watakaosadia kuleta ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Venezuela katika ujumla wao.

CELAM inalipongeza Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Venezuela, Caritas Venezuela kwa huduma makini kwa watu wa Mungu nchini humo. Perù kwa upande wake, itaendelea kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kadiri ya uwezo wake. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini linakaza kusema, Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani", itakuwa ni fursa ya kuibua mbinu mkakati wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; sera na mikakati ya shughuli za kitume pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali:kuhusu: haki jamii, malezi awali na endelevu, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia unaoziunganisha nchi tisa ambazo ni: Bolivia, Brazil, Colombia, Equador, Perù, Venezuela, Suriname na Guyana. Hatua zote za maandalizi tayari zimekwisha kutekelezwa na kwamba, “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi” imekwisha kamilika na sasa inaendelea kufanyiwa kazi kwenye ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa, ili hatimaye, iweze kuchambuliwa na kupembuliwa kwa kina wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela linaendelea kuwahamasisha viongozi wa Serikali na upande wa upinzani kushiriki katika mazungumzo katika ukweli na uwazi yanayopania kwa namna ya pekee kabisa: ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Venezuela; mazungumzo yanayoratibiwa Serikali ya Norway. Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema kumekuwepo na uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu nchini Venezuela. Ushiriki wahusika wote kwenye mgogoro wa Venezuela ni muhimu sana kwani wananchi wanasubiri majibu na utekelezaji wa maamuzi yatakayokuwa yamefikiwa.

Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, majadiliano haya yanaibua mradi unaopania kujenga na kuimarisha demokrasia shirikishi; ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; ili hatimaye juhudi zote hizi wanasema Maaskofu Katoliki wa Venezuela ziweze kusaidia mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Venezuela. Maaskofu wanaiomba Serikali ya Venezuela kuhakikisha kwamba, inaondoa vikwazo, ili watu waweze kupatiwa msaada wa chakula na dawa kwani wanakabiliwa na hali ngumu sana ya maisha. Vyombo vya ulinzi na usalama nchini Venezuela vitekeleze dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia misingi ya: haki, ukweli na usawa na wala visitumiwe kunyanyasa na kuwadhulumu watu haki zao msingi!

Papa: Venezuela

 

 

14 July 2019, 10:01