Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Utunzaji Bora wa Mazingira: Muhimu: Sifa na utukufu wa Mungu; Ekaristi Takatifu kama zawadi na Sadaka kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Papa Francisko: Utunzaji Bora wa Mazingira: Muhimu: Sifa na utukufu wa Mungu; Ekaristi Takatifu kama zawadi na Sadaka kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. 

Papa: Utunzaji bora wa Mazingira: Utukufu, Ekaristi & Kufunga!

Papa Francisko anazipongeza Jumuiya za “Laudato si” zinazoendelea kuragibisha Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu utunzaji bora wa mazingira kwa kujikita katika mchakato wa kufanya mabadiliko katika mtindo wa maisha yanayofumbatwa katika kuzingatia: Utukufu wa Mungu; Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja kufunga. kujinyima na kujisadaka kwa ajili ya mafao makubwa zaidi ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani na maendeleo fungamani ya binadamu kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu Francisko anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia na kwa kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki. Uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika mtindo wa maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote duniani! Ili kuweza kutekeleaza changamoto za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, hivi karibuni kumeanzishwa Jumuiya za “Laudato si”, utume unaofanywa na familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Rieti na Kampuni ya “Slow food”.

Jumuiya kama hizi zinaendelea kuanzishwa kwenye Majimbo mbali mbali ndani na nje ya Italia anasema Askofu Domenico Pompili wa Jimbo Katoliki Rieti, Italia. Lengo ni kumwilisha jitihada za  wongofu wa kiekolojia ili kukuza na kudumisha ekolojia fungamani. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini jitihada hizi, Jumamosi tarehe 6 Julai 2019 ametuma ujumbe kwa washiriki wa Jukwaa la Jumuiya za “Laudato si” wakati wa kongamano lake huko Amatrice, Italia. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa washiriki hawa anapenda kukazia mambo makuu matatu: Utukufu kwa Mungu, Ekaristi Takatifu pamoja na Kufunga!

Baba Mtakatifu anasema, kongamano hili linafanyika katika mji wa Amatrice ulioharibiwa sana na tetemeko la ardhi lililoikumba Italia kunako mwezi Agosti, 2016 na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.Kumbe, mkutano huu ni alama ya matumaini mapya, katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kuonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na wale wote walioguswa na kutikiswa sana na tetemeko hilo. Uharibifu wa mazingira unaacha madonda makubwa katika maisha ya binadamu anasema Baba Mtsakatifu Francisko. Haiwezekani kuwa na upyaisho kuhusiana na mazingira bila ya kuwepo upyaisho wa mwanadamu mwenyewe.

Ekolojia fungamani na utu wa mwanadamu ni sawa na chanda na pete na madhara yake ni makubwa katika maisha ya mwanadamu. Mwaka 2018, Jumuiya za “Laudato si” zilifanya kongamano kuhusu madhara ya taka za plastiki katika maisha ya viumbe hai. Hali hii inajionesha pia kwenye Ukanda wa Amazzonia kama ambavyo imefafanuliwa katika Hati ya Kutendea Kazi, “Instrumentum Laboris” kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazzonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani.” Hali ya Ukanda wa Amazzonia inatisha sana kwani watu wanaendelea kujikita katika kutafuta faida kubwa kiasi hata cha kwenda kinyume cha haki msingi za binadamu.

Haki jamii inapaswa kulindwa na kudumishwa na wote kwani madhara ya uchafuzi mkubwa wa mazingira huko Amazzonia yana athari zake katika kiwango cha kimataifa. Kuna maelfu ya watu ambao wamelazimishwa kuyakimbia maeneo yao, kiasi kwamba, wamekuwa tena wageni hata katika ardhi yao wenyewe; utu, heshima, mila, tamaduni na mapokeo yao mazuri, yamesiginwa. Katika hali na mazingira haya, binadamu hawezi kukaa na kuangalia haya yanayotendeka, sembuse Kanisa? Kilio cha maskini kama alivyosema Mtakatifu Paulo VI hakina budi kusikika midomoni mwa Kanisa.Baba Mtakatifu anazipongeza Jumuiya za “Laudato si” zinazoendelea kuragibisha Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kujikita katika mchakato wa kufanya mabadiliko katika mtindo wa maisha yanayofumbatwa katika kuzingatia: Utukufu wa Mungu; Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja kufunga na kujinyima kwa ajili ya mafao makubwa zaidi. Mwanadamu anapaswa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na uzuri wa kazi ya uumbaji.

Sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu ni matunda ya tafakari ya kina kuhusu kazi ya uumbaji inayomwajibisha mwanadamu kuilinda, kuitunza na kuiendeleza kama njia inayofaa kwa ajili ya kuheshimu kazi ya uumbaji na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumba mwenyewe! Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na mwelekeo wa Kiekaristi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kutambua kwamba, kazi ya uumbaji ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitunza na kuiendeleza. Kumbe, anawajibu wa kushirikishana zawadi hii na jirani zake, ili watu wengi zaidi waweze kupata furaha kwa kushiriki matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kwa heshima na nidhamu unadai mchakato wa kufunga na kujinyima, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni changamoto ya kujikita katika wongofu wa kiekolojia unaowataka watu kuondokana na tabia ya uchoyo pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa dunia, kwa kuanza kujenga na kudumisha ekolojia kwa heshima na nidhamu.Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumuiya za “Laudato si” zitakuwa ni mbegu ya upyaisho, ili kuchangia matumaini mapya kwa ulimwengu ujao, kwa kulinda na kutunza uzuri wa mazingira nyumba ya wote; kwa ajili ya ekolojia fungamani na kwa ajili ya maisha ya viumbe hao wote, “Ad maiorem Dei gloriam” yaani “kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu!

Papa: Laudato si

 

06 July 2019, 14:42