Tafuta

Papa Francisko, tarehe 8 Julai 2019 anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu: Siku ya kusali na kutafakari na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji wanaokufa maji huko Baharini! Papa Francisko, tarehe 8 Julai 2019 anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu: Siku ya kusali na kutafakari na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji wanaokufa maji huko Baharini! 

Papa Francisko kuadhimisha Misa: Lampedusa:2013-2019: Miaka sita!

Wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 250 walioteuliwa kutoka sehemu mbali mbali za Italia pamoja na wale wanaoendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na maisha yao kama binadamu, watashiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 5:00 Adhuhuri. Utu & Haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 8 Julai 2013 kwa mara ya kwanza kabisa, Baba Mtakatifu Francisko, baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki alipofanya ziara yake ya kwanza kutoka mjini Vatican ili kwenda kwenye Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko Kusini mwa Italia, ili kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahifadhiwa Kisiwani hapo. Lakini pia, Baba Mtakatifu alipenda kusali na kuwaombea wale wote waliofariki dunia na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania na makaburi yao hayana alama wala kumbu kumbu tena! Hili ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Jumatatu, tarehe 8 Julai 2019, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, ambao wamepoteza maisha yao, wakiwa njiani kutafuta, hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 250 walioteuliwa kutoka sehemu mbali mbali za Italia pamoja na wale wanaoendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na maisha yao kama binadamu, watashiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 5:00 Adhuhuri. Ibada hii ya Misa Takatifu imeandaliwa na kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Tukio hili litatangazwa moja kwa moja na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican.

Baba Mtakatifu anataka Ibada hii ya Misa iwe ni kwa ajili ya kusali na kufanya tafakari ya kina, ili kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliopoteza maisha kwa kukimbia vita, umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na hali ngumu ya maisha. Baba Mtakatifu anataka kuwatia moyo wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji; watu wanaowapokea na kuwahudumia watu hawa wanaohitaji kushuhudiwa Injili ya matumaini. Sera na mikakati ya Kanisa katika huduma kwa wakimbizi inafumbatwa katika misingi mikuu minne yaani: Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha katika maisha ya watu wanaowapokea na kuwapatia hifadhi.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Kuwapokea maana yake ni kutoa fursa kwa wakimbizi na wahamiaji kuingia katika nchi husika kwa njia salama zinazozingatia sheria za nchi; kwa kutoa hati za kusafiria na kuwapatia wakimbizi na wahamiaji nafasi ya kuweza kukutana na kujiunga tena na familia zao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya na Mashirika mbali mbali yatasaidia kutoa msaada wa kiutu kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliwa na hali tete zaidi. Watu wanaokimbia vita, nyanyaso na uvunjifu wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu, waangaliwe kwa jicho la huruma kwa kupewa hati za muda na huduma makini kadiri ya utu na heshima yao kama binadamu, ili kutoa nafasi kwa watu hawa kukutana na wenyeji wao, ili hatimaye, kuboresha huduma, daima usalama na utu wa mtu, ukipewa kipaumbele cha kwanza kabla hata ya kuangalia usalama wa taifa, sanjari na kuvifunda vyema vikosi vya ulinzi na usalama kwenye mipaka ya nchi.

Baba Mtakatifu anasema, Kuwalinda maana yake ni kuhakikisha kwamba haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu zinalindwa na kudumishwa, kwa kupatiwa huduma ya faraja; kwa kulinda na kutunza nyaraka na utambulisho wao; kwa kuwapatia fursa za haki, nafasi ya kuweza kufungua akaunti ya fedha benki pamoja na huduma makini ya maisha; kwani kwa hakika, wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ni hazina na amana kwa jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi.

Baba Mtakatifu anafanua kwama, Kuwaendeleza wakimbizi na wahamiaji maana yake ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya inayowapokea na kuwakirimia inawapatia pia fursa ya kujiendeleza katika utimilifu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wapewe uhuru wa kuabudu na kuungama imani yao; fursa za kazi na ajira; nafasi ya kujifunza lugha na tamaduni za watu mahalia, ili kweli waweze kushiriki kikamilifu katika maisha ya Jamii inayowahifadhi. Watoto wadogo walindwe dhidi ya kazi za suluba zinazoweza kuwapoka utu na heshima yao kwa kuwadumaza!

Baba Mtakatifu anasema, Kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji ni kuhakikisha kwamba, hata katika mwingiliano wa tamaduni, mila na desturi, bado wakimbizi na wahamiaji watabakia na utambulisho wao, lakini wajenge madaraja ya kufahamiana na kuheshimiana, ili kujenga watu wa mila na tamaduni mbali mbali, zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu! Mchakato huu unaweza kuendelezwa kwa haraka kwa kutoa vibali vya uraia na vibali vya kuishi kwa muda mrefu, daima utamaduni wa watu kukutana, kufahamiana na kusaidiana ukipewa kipaumbele cha kwanza, ili kujenga mchakato wa kuwahusisha na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika uhalisia wa maisha ya jamii inayowahifadhi.

Papa: Misa: Wakimbizi
05 July 2019, 15:33