Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na taarifa ya kifo cha Vincent Lambert kilichotokea baada ya kusitishiwa huduma ya chakula na maji kwa amri ya Mahakama! Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa sana na taarifa ya kifo cha Vincent Lambert kilichotokea baada ya kusitishiwa huduma ya chakula na maji kwa amri ya Mahakama!  (ANSA)

Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Vincent Lambert!

Vincent Lambert ambaye tarehe 20 Septemba 2019 angekuwa anatimiza miaka 43 ya kuzaliwa kwake, tangu tarehe 2 Julai 2019 alikuwa amelazwa Hospitalini na madaktari wakaamua kusitisha huduma ya chakula na maji na huo ukawa ni mwanzo wa mapambano ya kisheria! Kwa muaka wa miaka 10 Lambert amekuwa akiishi katika hali ya kutojitambua baada ya kupatwa na ajali mbaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Vincent Lambert kilichotea Alhamisi tarehe 11 Julai 2019 huko Reims, Kaskazini mwa Ufaransa. Vincent Lambert ambaye tarehe 20 Septemba 2019 angekuwa anatimiza miaka 43 ya kuzaliwa kwake, tangu tarehe 2 Julai 2019 alikuwa amelazwa Hospitalini na madaktari wakaamua kusitisha huduma ya chakula na maji na huo ukawa ni mwanzo wa mapambano ya kisheria! Kwa muda wa miaka 10, Vincent Lambert amekuwa akiishi katika hali ya kutojitambua baada ya kupatwa na ajali mbaya sana ya barabarani iliyopelekea kukosa fahamu kwa miaka yote hii.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Vincent Lambert, ili aweze kupokelewa kwenye makazi ya maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala: ndugu, jamaa, marafiki na wale wote waliojisadaka kwa upendo na huruma bila ya kujibakiza ili kusaidia kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hakuna mtu mwenye mamlaka ya kufyekelea mbali uhai wa mtu, kwa sababu, maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ndiye chanzo na kilele cha maisha ya mwanadamu.

Ni dhamana na wajibu wa watu wote kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, na hivyo kuondokana na kishawishi cha kutumbukia katika utandawazi usiojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wengine! Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Jumatano tarehe 10 Julai 2019, aliwakumbuka na kuwaombea wagonjwa waliotelekezwa na kuachwa pweke katika mateso na mahangaiko yao, katika dakika za mwisho wa maisha yao.

Jamii inayoheshimu na kuthamini maisha, utu na heshima ya binadamu, inawajibu na dhamana ya kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya binadamu, tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kwa upande wake, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha na Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Ndoa na Familia ya Yohane Paulo II anasikitika kusema, ukatili dhidi ya Vincent Lambert, kwa kunyima chakula na maji, hadi kifo chake ni dalili za jamii kukumbatia utamaduni wa kifo unaosigina maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Papa: Kifo Lambert

 

11 July 2019, 15:46