Tafuta

Vatican News
Papa Francisko analitaka Kanisa kujielekeza zaidi katika sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso za kijinsia ndani ya kanisa ili kujenga utume wa kuzuia nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Papa Francisko analitaka Kanisa kujielekeza zaidi katika sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso za kijinsia ndani ya kanisa ili kujenga utume wa kuzuia nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.  (ANSA)

Papa Francisko: Kashfa ya nyanyaso za kijinsia: Kipaumbele cha kwanza ni Utume wa kukinga!

Mfumo wa kukinga ni urithi na amana kubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane Bosco ambao unapaswa kukita mizizi yake katika sekta ya elimu. Huu ni mfumo ambao unawataka wadau wote kuwa macho, ili kamwe wanafunzi wasijikute wakiwa wanahadaiwa na hatimaye kutumbukizwa katika nyanyaso za kijinsia, matumizi haramu ya dawa za kulevya, pombe na mambo kama haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video aliowatumia wanafunzi wa Kituo cha Tafiti na Malezi kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mexico, “Ceprome”, waliokuwa wanahudhuria kozi maalum kuhusu protokali sanjari na sera pamoja na mbinu mkakati wa kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia amekazia umuhimu wa Kanisa kujikita katika sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa. Kozi hii imehitimishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kuzuia nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa.

Anatambua kwamba, hili ni tatizo na changamoto pevu, iliyogeuka na kuwa ni kashfa katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema kwa uchungu mkubwa, asiwepo mtu au kikundi cha watu waliokengeuka na kutopea katika mmong’onyoko wa maadili na utu wema watakao wazuia watoto kukutana na Kristo Yesu katika Kanisa lake. Baba Mtakatifu anatambua umuhimu wa kozi hii katika maisha na utume wa Kanisa ndan na nje ya Mexico. Yesu katika Injili anawahimiza Mitume wake, kuwapatia nafasi watoto ili waende kwake! Huu ni mwaliko unaowagusa watu wote bila ubaguzi, yaani: Maaskofu, mapadre, watawa au waamini walei.

Wale wote wenye mielekeo ya kutaka kuleta kashfa tena ndani ya Kanisa, washughulikiwe kikamilifu; kwa kurekebishwa au kuadhibiwa ikiwa kama watapatikana na kosa la jinai. Hapa mkazo unaotolewa ni heri kuzuia kuliko kuponya kama wanavyosema waswahili, ili watoto wadogo wasitumbukizwe kwenye kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Huu ndio utume wa kuzuia ambao unapaswa kuvaliwa njuga na Makanisa mahalia, sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni urithi na amana kubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane Bosco ambao unapaswa kukita mizizi yake katika sekta ya elimu, kwa kujenga na kuimarisha “Mfumo wa Kukinga” “Preventive System”.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, huu ni mfumo ambao unawataka wadau wote kuwa macho, ili kamwe wanafunzi wasijikute wakiwa wanahadaiwa na hatimaye kutumbukizwa katika nyanyaso za kijinsia, matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevina mambo kama haya! Yote haya ni matendo yanayoonesha kukengeuka kwa watu pamoja na kutopea kwa kanuni maadili na utu wema. Kozi hii ya Kituo cha Tafiti na Malezi kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mexico, “Ceprome”, ilifunguliwa rasmi na Askofu mkuu Franco Coppola, Balozi wa Vatican nchini Mexico, ambaye katika hotuba yake elekezi, amekazia umuhimu wa kuwakinga watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Kozi hii imeongozwa na kauli mbiu “Mbinu Mkakati wa Kuzuia Nyanyaso za Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo ndani ya Kanisa Amerika ya Kusini”. Kituo cha Ceprome ni matunda ya ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mexico, tangu mwaka 2016. Kituo hiki kimeanza maandalizi ya Kongamano la kwanza la Udhibiti wa Nyanyaso za Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo ndani ya Kanisa, Amerika ya Kusini. Kongamano hili litaadhimishwa kuanzia tarehe 6 hadi 8 Novemba 2019. Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia inahusu nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Sheria hizi zinawalazimisha wakleri na watawa kutoa taarifa pale kunapokuwepo na shutuma kama hizi. Kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wakleri na watawa kwamba, wao ni nuru ya ulimwengu na kwamba, Kristo Yesu anawaita na kuwataka kuwa waaminifu na mfano mahiri wa tunu msingi za maisha, uadilifu na utakatifu. Hii ni sehemu ya mafundisho mazito yaliyomo kwenye barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia zinazoweza kutendwa na wakleri pamoja na watawa.

Nyanyaso za kijinsia ni uhalifu unaosababisha madhara makubwa ya kimwili, kisaokolojia na kiroho si tu kwa waathirika bali hata kwa Jumuiya ya waamini. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Huu ni wajibu wao wa kimaadili. Hati hii ni matunda ya mkutano wa ulinzi wa watoto wadogo uliofanyika mjini Vatican, mwezi Februari 2019. Hizi ni sheria kwa ajili ya Kanisa Katoliki katika ujumla wake. Hadi kufikia Juni 2020, Majimbo yote ya Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, yatapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Sheria hii inahusu pia matumizi ya picha za ngono pamoja na viongozi wa Kanisa kuficha kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Kumbe, Sheria inatoa mwanya kwa kila jimbo kuhakikisha kwamba linatenda kadiri ya tamaduni na mazingira ya Kanisa mahalia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waathirika wa nyanyaso za kijinsia wanapokelewa na kusikilizwa, hata kama kunaweza kutokea pia shutuma za uongo, lakini shutuma hizi zitapaswa kushughulikiwa kikamilifu. Wakleri na watawa wote wanawajibika sasa kisheria kutoa taarifa kuhusu nyanyaso za kijinsia wanazozifahamu, haraka iwezekanvyo kwa uongozi wa Jimbo!

Watapaswa pia kutoa taarifa pale ambapo kiongozi wa Kanisa hakutimiza wajibu wake au amefumbia macho uwepo wa nyanyaso za kijinsia katika eneo lake. Hadi wakati huu, wajibu wa kutoa taarifa kuhusu nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa lilibaki ni jambo la dhamiri ya mtu binafsi, lakini kuanzia sasa na kuendelea huu ni wajibu wa kisheria kwa wakleri, watawa pamoja na waamini walei! Familia ya Mungu katika ujumla wake inapaswa kusimama kidete kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa kutoa taarifa. Hati hii inaendelea kuwabana hata wakleri wanapowakosea haki watawa au nyanyaso dhidi ya waseminari na wanovisi.

Kuficha kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni kesi ambayo imepewa uzito wa pekee kabisa. Haya ni matukio yanayoweza kufanyika moja kwa moja au kwa kutotimiza wajibu; kwa kuingilia au kuvuruga uchunguzi unaofanywa na vyombo vya kiraia au kadiri ya Sheria za Kanisa na uongozi dhidi ya mkleri au mtawa aliyemdhalilisha mtu kijinsia. Wahusika wakuu ni wale waliopewa dhamana na wajibu ndani ya Kanisa, badala ya kufuatilia kashfa ya nyanyaso za kijinsia zilizotendwa na watu wengine, wao wamezificha na kujenga ngome ya kuwalinda watuhumiwa badala ya kuwalinda waathirika. Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi ya kichungaji, “Kama Mama mpendelevu” iliyochapishwa Juni, 2016, anasema: nyanyaso za kijinsia ni kati ya makosa makubwa ambayo yamebainishwa barabara kwenye Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza viongozi wa Kanisa kuwa macho dhidi ya nyanyaso za kijinsia wanazoweza kufanyiwa watoto wadogo; anaonesha hatua zitakazochukuliwa ili kutekeleza vifungu vya Sheria ambavyo viko tayari kwenye Sheria za Kanisa Namba 193§ 1 na Sheria za Kanisa la Mashariki Namba 975§1. Mkazo hapa ni wajibu wa viongozi wa Kanisa katika kutekeleza dhamana na utume wao! Malezi na majiundo endelevu kwa Maaskofu ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wanayo dhamana na wajibu kwa wakleri na watawa wanaoishi na kufanya utume katika maeneo yao, kwa kuangalia utakatifu wa maisha na utume wao!

Kumbe, uchaguzi wa vijana wanaotaka kuingia katika wito na maisha ya kipadre na kitawa ni muhimu sana! Maaskofu wanapaswa kufuatilia malezi na majiundo yao katika hatua mbali mbali na kwamba, Askofu anapaswa kuwa karibu zaidi na mapadre pamoja na watawa wake, ili kujenga na kudumisha majadiliano katika udugu, ili aweze kuwasindikiza katika shida na mahangaiko yao, katika furaha na matarajio yao kwa siku za usoni. Shutuma za nyanyaso za kijinsia dhidi ya mapadre na watawa zinapaswa kushughulikiwa kadiri ya Sheria za Kanisa na Sheria za nchi husika. Watuhumiwa wasaidiwe kutambua hali yao!

Haki za pande zote zinazohusika zinapaswa kudumishwa, lakini waathirika wa nyanyaso za kijinsia wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, hali ambayo itamlazimisha Askofu mahalia kumsimamisha Padre wake kutoa huduma ya hadhara. Kwa hakika kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa imesababisha madhara makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, wajibu wa kwanza ni kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia.

Papa: Mexico
22 July 2019, 10:06