Papa Francisko asema, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu: Ni damu ya watu wasiokuwa na hatia inayomwagika bararabani! Papa Francisko asema, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu: Ni damu ya watu wasiokuwa na hatia inayomwagika bararabani! 

Papa Francisko: Kashfa ya biashara ya binadamu duniani!

Papa Francisko anasema kwamba, biashara ya ngono ni uhalifu unaowanyanyasa wasichana na wanawake kiasi cha kuwatumbukiza katika utumwa, unaodhalilisha utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Padre A. Bonaiuto anafuata nyayo za Don Oreste Benzi na Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Papa Yohane XXIII ni wamisionari wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikuwa ni fursa adhimu kwa huruma ya Mungu kuwa ni kiini cha tafakari ya maisha na utume wa Kanisa; tafakari ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Imekuwa ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, alijiwekea utaratibu wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili, katika maisha yake, dhamana ambayo anajitahidi kuiendeleza kila wakati anapopata fursa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kutembelea Jumuiya ya Papa Yohane XXIII iliyoanzishwa na Don Oreste Benzi kunako mwaka 1968. Tangu wakati huo, Jumuiya imeenea katika nchi 42, Tanzania ikiwemo, imekuwa ni kama hospitali katika uwanja wa mapambano sehemu mbali mbali za dunia dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Mapambano dhidi ya utumwa mamboleo yanaendelea kushika kasi na katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu, tarehe 30 Julai 2019, Padre Aldo Bonaiuto amezindua kitabu kinachosomeka kwa jina “Donne Crocifisse, La Vergogna della tratta raccontata dalla strada”, kilichochapishwa na Rubbettino chenye kurasa 219 na utangulizi wake umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Anasema kwa uchungu mkubwa kwamba, biashara ya ngono ni uhalifu unaowanyanyasa wasichana na wanawake kiasi cha kuwatumbukiza katika utumwa, unaodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Padre Aldo Bonaiuto anafuata nyayo za  Don Oreste Benzi na Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Papa Yohane XXIII ni wamisionari wa huruma ya Mungu. Katika maadhimisho ya Ijumaa ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko alikutana uso kwa uso na wasichana pamoja na wanawake waliokuwa wamenyanyasika, wakadhulumiwa na kujaribiwa sana, kiasi cha kuwatambua kwamba, hawa ni wanawake waliokuwa wamesulubishwa kwa kutumbukizwa katika utumwa mamboleo. Katika chumba cha mkutano walimokuwemo wasichana na wanawake wale, Baba Mtakatifu anakiri kwamba, alionja kutoka katika undani wake uchungu, ukosefu wa haki na upendo wa dhati.

Kwake, huu ulikuwa ni mwanya wa kugusa tena na tena Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu yanayojionesha katika wafuasi wake sehemu mbali mbali za dunia na kwa namna ya pekee, wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo. Alipata nafasi ya kusikiliza kwa makini shuhuhuda zilizotolewa na wasichana pamoja na wanawake hao ambao walikuwa wamenyanyuliwa na kuondolewa barabarani ambako walikuwa wanafanyishwa biashara ya ngono na wajanja wachache ambao kwa hakika wamekengeuka na kutopea katika dhuluma na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Baadhi yao walikuwa na watoto migongoni mwao, kiasi hata cha kumfanya Baba Mtakatifu kutaka kuwaomba msamaha, kutokana na nyanyaso ambazo wamekumbana nazo barabarani ili kuridhisha tamaa ya wateja wao ambao wengi wao wanajiita eti ni Wakristo!

Baba Mtakatifu katika dibaji ya kitabu hiki anapenda kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kusaidia mchakato wa ukarimu unaopania kuwasaidia wasichana na wanawake hawa kutoka kwenye mzunguko wa biashara ya ngono na mateso. Hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kamwe hawawezi kugeuzwa kuwa kama bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni! Baba Mtakatifu anasema, anaandika dibaji hii kwa moyo mkunjufu kabisa ili watu wengi waweze kutambua amana, utajiri na mchango unaotolewa na Padre Aldo Bonaiuto pamoja na Jumuiya ya Papa Yohane XXIII, ambayo kwa hakika imekuwa kweli ni wamisionari wa huruma ya Mungu.

Hawa ni watu wanaoendeleza karama ya Don Oreste Benzi. Si lelemama kuweza kutekeleza utume huu, kwani unatekelezwa katika hali na mazingira magumu na hatarishi. Hapa wanagusa vyanzo vya fedha haramu kwa makundi ya uhalifu kitaifa na kimataifa. Ni matamanio halali ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kitabu hiki kitaweza kupata wasomaji watakaoguswa na historia na idadi ya wasichana na wanawake wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na hata wakati mwingine na viungo vyake. Jambo la msingi ni wateja wa biashara ya ngono kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kubadilisha mtindo wa maisha na kwa njia hii, biashara ya binadamu, ngono na utumwa mamboleo vitaweza kusitishwa kutoka katika uso wa dunia.

Tabia ya watu kukengeuka na kutopoea katika dhuluma na nyanyaso mbali mbali, inaweza kurekebishwa kwa mtu binafsi kuzama katika undani wake na kuanza kuchunguza dhamiri, hali hii inaweza pia kuwa katika ngazi ya kijamii na hatimaye, Kanisa katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema kwa macho makavu kabisa kwamba, aina yoyote ile ya ukahaba ni tendo linalonyanyasa utu, heshima na haki msingi za binadamu, kiasi cha kuwatumbukiza wahusika katika dimbwi la utumwa. Huu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha vilema vya dhambi. Huu ni ukatili unaovishwa “gunia la upendo”.

Matukio yote haya anasema Baba Mtakatifu yanaacha ukakasi katika dhamiri za watu, kwa kuwageuza wasichana na wanawake kuwa kama bidhaa zinazouzwa na kununuliwa sokoni. Huu ni ugonjwa unaoendelea kuwaandama walimwengu na kwa hakika ni mwelekeo potofu wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa kuwakomboa wasichana na wanawake hawa kutoka katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni tendo la huruma, ni dhamana na wajibu wa watu wote. Kilio cha wasichana na wanawake waliotumbukizwa katika biashara ya ngono, hakiwezi kuendelea kugonga mwamba, kinapaswa kusikilizwa na kupewa jibu makini katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake. Asiwepo mtu awaye yote anayewageuzia wasichana na wanawake hawa kisogo au kunawa mikono kama ilivyokuwa kwa Pilato, kwamba, hayamhusu hata kidogo. Hii ni damu ya watu wasiokuwa na hatia inayoendelea kumwagika kwenye barabara mbali mbali ulimwenguni anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa uchungu mkubwa!

Papa: Mateso Wanawake

 

 

 

30 July 2019, 14:06