Tafuta

Vatican News
Utume wa Sala Kimataifa ni mhimili mkuu wa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia! Ni Kielelezo cha umoja na mshikamano wa dhati! Utume wa Sala Kimataifa ni mhimili mkuu wa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia! Ni Kielelezo cha umoja na mshikamano wa dhati!  (Vatican Media)

Papa: Utume wa Sala ni mhimili wa maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu anawashukuru wote wanaojisadaka ili kuhakikisha kwamba, Utume wa Sala unakita mizizi yake hata katika ulimwengu wa kidigitali kama alivyofanya Padre Antonio kutoka Ureno. Mitandao ya kijamii, yawe ni majukwaa ya kutangaza na kushuhudia: wema, huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mitandao, ilete mvuto wa kumwendea Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 175 ya Utume wa Sala Kimataifa, Ijumaa, tarehe 28 Juni 2019, amewapongeza wanachama wake ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kulisindikiza Kanisa katika maisha na utume wake, kwa njia ya sala; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu, maisha ya watu ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu amewashukuru wale wote waliotoa shuhuda mbali mbali wakati wa tukio hili! Padre Mathew kutoka Taiwan, ambaye amesema kwa njia ya mtandao “Click to Pray" hata wao wanaungana na Kanisa zima kwa njia ya sala.

Baba Mtakatifu amewashukuru waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kwa umoja na mshikamano huu kwa njia ya sala, licha ya changamoto mbali mbali na magumu wanayokabiliana nayo! Utume wa sala ni muhimu sana kama ushuhuda wa Injili, unaokuza ari na moyo wa udugu katika Kristo ili kuvunjilia mbali kuta za utengano na hatimaye, kujenga madaraja yanayowakutanisha watu ili kuwa na matumaini makubwa zaidi kwa siku za usoni! Marie Dominique kutoka Ufaransa amesimulia shuhuda kuhusu utume wa Sala ulioanzishwa nchini Ufaransa miaka 175 iliyopita. Huu ni utume unaopyaisha mchakato wa uinjilishaji unaokita mizizi yake katika sakafu ya nyoyo za watu, kwa kujenga mtandao wa mshikamano wa upendo na sala kati ya wakleri, watawa na waamini walei; katika furaha na magumu ya maisha. Utume wa sala ni muhimu katika kukoleza moyo wa Injili ya matumaini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga na kudumisha utamaduni na maisha ya sala, kwa ajili ya mahitaji yao binafsi, jirani na watu sehemu mbali mbali za dunia. Anakaza kusema, majungu si mtaji, bali ni upanga unaofisha maisha ya watu na jamii katika ujumla wake! Watu waache majungu na badala yake, wakite maisha yao katika sala! Katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, waamini wajifunze huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili nao waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kama alivyokumbusha Bettina kutoka Argentina wakati wa ushuhuda wake.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi Takatifu, EYM., kama alivyoshuhudia Sr. Selam kutoka Ethiopia, kinaonesha umuhimu wa vijana kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, shule ya Neno la Mungu, chachu na ari ya maisha na utume wa kimisionari, tayari kujimega bila kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Injili ya upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anawataka wazazi na walezi kujibidisha kuwafundisha watoto wao sala muhimu katika maisha. Baba Mtakatifu amekazia pia umuhimu wa vijana kudumisha majadiliano na “vijana wa zamani”, ili kushirikishana uzoefu na mang’amuzi mbali mbali ya maisha. Watambue kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuwaombea waja wake, mbmele ya Baba yake wa mbinguni.

Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka ili kuhakikisha kwamba, Utume wa Sala unakita mizizi yake hata katika ulimwengu wa kidigitali kama alivyofanya Padre Antonio kutoka Ureno. Mitandao ya kijamii, yawe ni majukwaa ya kutangaza na kushuhudia: wema, huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mitandao, ilete mvuto wa watu kumwendea Mwenyezi Mungu ili aweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao! Sala ni mhimili wa maisha na utume wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu, pasi na sala, Kanisa litanyauka na kupotea kama ndoto ya mchana!

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapongeza Wayesuit kwa kusaidia kueneza Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na Utume wa Sala Kimataifa katika kipindi cha Miaka 175 iliyopita. Wayesuit ni watu wa sala. Baba Mtakatifu pamoja na wajumbe wote waliohusika wamesali kwa pamoja nia za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Julai kwa kukazia unyenyekevu, mshikamano na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wamewaombea wale wote wanaotekeleza haki waweze kufanya kazi hii kwa ufasaha ili haki iweze kutawala ulimwengtuni kote!

Psapa: Utume wa Sala
28 June 2019, 18:41