Tafuta

Tarehe 20 Juni 2019 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani:Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji na Wakimbizi Duniani "Global Compact 2018. Tarehe 20 Juni 2019 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani:Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji na Wakimbizi Duniani "Global Compact 2018. 

Siku ya Wakimbizi Duniani 2019: Usalama wa wakimbizi na wahamiaji

Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani 2019 ni mwaliko wa tafakari kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018, yaani “Global Compact 2018”. Mkataba huu unapania: Kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio chao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Kimataifa kwa Mwaka 2019, Alhamisi, tarehe 20 Juni 2019 Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, wakati wa hija yake ya kichungaji, Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche, nchini Italia, amewakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji katika shida na mahangaiko yao. Ametumia fursa hii kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha moyo wa mshikamano na upendo wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anasema, hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Jumuiya za kikanisa na kiraia, zijitahidi kuonesha ukaribu wao, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Maadhimisho ya Mwaka huu 2019 ni tafakari kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018, yaani “Global Compact 2018”.  

Mkataba huu unapania: Kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Mkataba unakazia umuhimu wa jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao. Pamoja na mambo mengine unapania kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na wakimbizi kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa. Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao; pamoja na kuangalia uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi.

 

Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji” unapania kutokomeza ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Katibu  mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres  katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2019 anasema, kuna zaidi ya watu milioni 70 ambao ni wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi. Idadi hii imeongezeka maradufu, ikilinganishwa na idadi ya wakimbizi na wahamiaji miaka 20 iliyopita. Nchi zinazozalisha wimbi kubwa la wakimbizi duniani ni pamoja na: Siria, Afghanistan, Sudan ya Kusini, Myanmar na Somalia. Umoja wa Mataifa unazishukuru nchi zote ambazo zinaendelea kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji, changamoto na mwaliko wa kuwekeza zaidi katika huduma kwa wakimbizi pamoja na kuwahakikishia ulinzi, usalama, haki na amani endelevu!

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, watu wengi duniani wanalazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, dhuluma, vitendo vya kigaidi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, umaskini, baa la njaa na ukosefu wa fursa za ajira. Asilimia 86% ya wakimbizi na wahamiaji duniani wanahudumiwa katika Nchi zinazoendelea. Kambi ya Dadaab iliyoko nchini Kenya ni kambi kubwa ya wakimbizi duniani, inayotoa hifadhi kwa wakimbizi zaidi ya 329, 000. Siku ya Wakimbizi Duniani ilianzishwa kunako mwaka 2000 na kuaanza kusherehekewa kunako mwaka 2001 kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mkataba wa Hali y Wakimbizi Duniani, uliopitiwa mkwaju! Siku ya Wakimbizi Duniani ni fursa ya kusali, kujifunza na kuadhimisha ujasiri, nguvu na uthubutu wa wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Papa: Wakimbizi 2019
19 June 2019, 13:35