Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Siku ya Maisha Kitaifa: Baba Mtakatifu Francisko akemea ukatili wa wanawake majumbani huko Uingereza, Wales, Scotland na Ireland! Ataka watu wakuze Injili ya familia! Maadhimisho ya Siku ya Maisha Kitaifa: Baba Mtakatifu Francisko akemea ukatili wa wanawake majumbani huko Uingereza, Wales, Scotland na Ireland! Ataka watu wakuze Injili ya familia!  (AFP or licensors)

Siku ya Maisha Kitaifa: Papa akemea ukatili wa wanawake majumbani

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, Wales, Scotland na Ireland, Jumapili, tarehe 16 Juni 2019 limeadhimisha Siku ya Maisha Kitaifa kwa kuangalia kashfa ya vipigo vya wanawake majumbani. Maaskofu wanasema, hili ni tatizo nyeti ambalo linaendelea kuzipekenyua familia nyingi, kiasi kwamba, madhara yake ni makubwa katika malezi, makuzi na ustawi wa familia zenyewe! No Kipigo!!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Unatoa mwelekeo wa Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Ni waraka unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka na kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa kwa kutambua haki msingi za wanawake na ushiriki wao katika maisha ya jamii, lakini katika baadhi ya nchi kuna mengi yanayopaswa kufanyika ili kukuza haki za wanawake pamoja na kutupilia mbali mila, desturi na tamaduni ambazo zimepitwa na wakati.

Mfumo dume, nyanyaso, utumwa na ukatili wa majumbani, ukeketaji; ukosefu wa haki na fursa sawa ni mambo ambayo yanasigina kwa kiasi kikubwa utu na heshima ya wanawake sehemu mbali mbali za dunia! Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, Wales, Scotland na Ireland, Jumapili iliyopita, tarehe 16 Juni 2019 limeadhimisha Siku ya Maisha Kitaifa kwa kuangalia kashfa ya vipigo vya wanawake majumbani. Maaskofu wanasema, hili ni tatizo nyeti ambalo linaendelea kuzipekenyua familia nyingi, kiasi kwamba, madhara yake ni makubwa katika malezi, makuzi na ustawi wa familia zenyewe. Kanisa linasema, hili ni tatizo linalopaswa kuvaliwa njuga ili kulinda na kudumisha tunu msingi za Injili ya familia, utu, heshima na haki msingi za wanawake!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, amewatakia heri na baraka waamini wote katika maadhimisho haya. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wataweza kufanikiwa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana, ili hatimaye, waweze kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafanikio ya watu wa Mungu. Watu wanapaswa kutambua na kushirikishana Habari Njema kwamba,  maisha ya binadamu ni matakatifu na ni mazuri sana! Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Maadhimisho ya Siku ya Maisha Kitaifa yanapania kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika masuala ya kimaadili, kijamii na kisiasa, kwa kuzingatia Mafundisho tanzu ya Kanisa, Biblia, Kanuni maadili na utu wema!

Papa: Siku ya Maisha
17 June 2019, 09:54