Jumatatu ya Pentekoste, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa: Nafasi ya kutafakari mchango wa Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa. Jumatatu ya Pentekoste, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa: Nafasi ya kutafakari mchango wa Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa. 

Bikira Maria Mama wa Kanisa: Utume na dhamana yake!

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko lao kuhusu Fumbo la Kanisa wanafafanua kuhusu nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu katika Fumbo la Kristo na la Kanisa: tangu Agano la Kale, Fumbo la Umwilisho; katika maisha ya hadharani na baada ya Kristo Yesu kupaa mbinguni. Bikira Maria kama mshiriki mwaminifu wa kazi ya ukombozi, mwombezi wa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Kanisa kuanzia mwaka 2018 inaadhimishwa Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste na mwaka huu ni tarehe 10 Juni 2019. Mabadiliko haya yanapaswa kuwa tayari yamekwisha kuingizwa kwenye Kalenda za maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na kufanyiwa kazi tangu sasa! Ibada hii kwa Bikira Maria, itawasaidia waamini kukumbuka kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika Fumbo la Msalaba linaloadhimishwa katika Ekaristi Takatifu, Kanisa linapomtolea pia sifa na heshima Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi!

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko lao kuhusu Fumbo la Kanisa wanafafanua kwa kina na mapana nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu katika Fumbo la Kristo na la Kanisa: tangu Agano la Kale, Fumbo la Umwilisho, Bikira Maria katika maisha ya hadharani ya Kristo Yesu, Bikira Maria baada ya Kristo Yesu kupaa mbinguni. Wanaendelea kufafanua dhamana na nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa kama mshiriki mwaminifu wa kazi ya ukombozi, mwombezi kwa ajili ya wokovu, Bikira Maria kama mfano wa utimilifu wa Kanisa katika maisha na utakatifu wake na kwamba, Bikira Maria ni ishara na matumaini thabiti na faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri huku Bondeni kwenye machozi!

Kwa hakika, Mapokeo ya maadhimisho ya Fumbo la maisha ya Kristo ambayo kamwe hayawezi kumtenga Bikira Maria, Mama wa Kristo na Kanisa. Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Wakristo ambao wamezaliwa kwake kwa njia ya fadhila ya upendo na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kama wanavyofundisha Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa pamoja na Mtakatifu Leo Mkuu. Umama wa Kristo na Kanisa ulidhihirishwa pale chini ya Msalaba, Bikira Maria alipopokea upendo wa dhati kutoka kwa Mwanaye mpendwa na Yohane kwa niaba ya wengine wote, wakawa ni wafuasi na mitume wa upendo kwa ajili ya Mama yake.

Bikira Maria aliendelea kuandamana na Kanisa katika sala wakati Mitume wakisubiria ujio wa Roho Mtakatifu. Kwa nyakati mbali mbali, waamini wamekuwa wakimheshimu na kumfanyia Ibada Bikira Maria kama: Mama wa Mitume, Mama wa waamini wa wale wote wanaozaliwa upya katika Kristo Yesu na Mama wa Kanisa kama wanavyofundisha Papa Benedikto XV pamoja na Papa Leo wa XIII. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 21 Novemba 1964, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipokuwa wanahitimisha Kikao cha tatu cha Mkutano huo, alitamka kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa; yaani: ni Mama wa Wakristo wote na wachungaji wanaomkimbilia kama Mama.

Kumbe, Bikira Maria, Mama wa Kanisa anapaswa kuheshimiwa na Wakristo wote. Katika maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho1975, kuliadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Litania ya Bikira Maria wa Loreto ikaongeza heshima hii katika Litania. Majimbo mbali mbali wakaona kwamba, inafaa na kuomba Kiti Kitakatifu kuruhusu maadhimisho haya yaingizwe katika kalenda ya majimbo yao! Kutokana na kukua na hatimaye, kukomaa kwa Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia tamko lililotolewa na Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa kwamba, kuanzia sasa Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Kanisa itakuwa inaadhimishwa Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste ya kila mwaka!

Maria: Mama wa Kanisa
10 June 2019, 15:32