Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema: Waamini ni nguzo thabiti zinalolisimamisha na kulitegemeza Kanisa kwa njia ya upendo wa kidugu! Papa Francisko asema: Waamini ni nguzo thabiti zinalolisimamisha na kulitegemeza Kanisa kwa njia ya upendo wa kidugu!  (AFP or licensors)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Umoja wa Kanisa

Kanisa linahitaji kuonja upendo kutoka kwa waamini wake anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hili ni Kanisa la waamini wote, kumbe, wanawajibika kulihudumia, kuliendeleza na kulidumisha. Mitume ni nguzo thabiti za Kanisa na waamini ni nguzo zinalolisimamisha na kulitegemeza Kanisa kwa njia ya upendo wa kidugu! Petro na Paulo walitofautiana kwa mengi, wakashibana kwa Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, amewakumbusha waamini kwamba, Mitume hawa wawili ni miamba ya Kanisa la Kristo. Hili ni Kanisa la Kristo, yaani waamini wote ni mali ya Kristo Yesu na anawapenda upeo! Kristo Yesu amelipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake kama mchumba wake hata waamini ni wachumba wa Kristo anasema Baba Mtakatifu. Yesu analiangalia Kanisa lake kwa huruma na mapendo; analipenda kwa uaminifu wote licha ya udhaifu, mapungufu ya kibinadamu na usaliti unaoliandama Kanisa wakati mwingine, lakini bado linaendelea kuwa ni Kanisa la Kristo.

Hili ni Kanisa la waamini wote linalofumbatwa katika upendo, kwa kuonesha ule uzuri wa ndugu kukaa pamoja kwa upendo kama anavyopenda Kristo mwenyewe. Kanisa linahitaji kuonja upendo kutoka kwa waamini wake anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hili ni Kanisa la waamini wote, kumbe, wanawajibika kulihudumia, kuliendeleza na kulidumisha. Mitume ni nguzo thabiti za Kanisa na waamini ni nguzo zinalolisimamisha na kulitegemeza Kanisa kwa njia ya upendo wa kidugu! Mitume Petro na Paulo walitofautiana sana kwa mambo mengi; Petro alikuwa ni mvuvi wa samaki, Paulo alikuwa ni Mfarisayo. Mitume pia walitofautiana kwa mtindo wa maisha na tabia; hata kuna wakati walikuwa wanasigana kwa mawazo, lakini wote wanaunganishwa na Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu wao.

Udugu katika Kristo unapata chanzo chake kutoka imani, inayowawezesha waamini kuwa na furaha kwa kutambuana kwamba, wao ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Waamini wawe wepesi kutambua karama na mapaji ya jirani zao badala ya kugubikwa na wivu usiokuwa na mashiko wala mvuto! Baba Mtakatifu anakaza kusema, wivu unasababisha machungu moyoni ni sawa na upanga unaopenyeza moyoni mwa mtu. Waamini wafurahie umoja unaobubujika kutoka katika imani, upendo na matumaini kwa Kristo Yesu. Huu ndio mwanga angavu wa Fumbo la Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Petro amekabidhiwa dhamana na utume wa kuwalisha Kondoo wa Kristo kwa huruma na upendo; mambo msingi yanayolijenga na kulidumisha Kanisa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kulipenda na kulitegemeza Kanisa; kwa kuwaona waamini wote kuwa ni ndugu zao katika Kristo Yesu; watu wanaopendana na kuheshimiana kama ambavyo Kristo Yesu anawapenda.

Iwe ni fursa ya kusali na kuwaombea wale wote wenye mtazamo tofauti wa uelewa wa Kanisa, hata wao waonje na kuguswa na huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini wajenge utamaduni wa kusali na kupenda; badala ya kurushiana maneno yasiyofaa pamoja na kutetana vibaya. Bikira Maria aliyekuwa chombo na kielelezo cha umoja miongoni mwa Mitume wa Yesu pamoja na kusali nao, kwa ulinzi na tunza yake ya kimama, aweze kuwalinda na kuwasimamia kama ndugu ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, amewatakia heri, baraka na neema waamini, mahujaji na wageni wote wanaoishi mjini Roma. Amewataka wasimame kidete kupambana na kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; wajifunge kibwebwe kukabiliana na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote.

Mwishoni, Baba Mtakatifu kwa mara nyingine tena, ametambua uwepo wa ujumbe wa  Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Amewawatambua pia waamini na mahujaji walioandamana na Maaskofu wao wakuu ili kupokea Pallio Takatifu. Wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, Kanisa limesali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko na Maaskofu wote, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwajalia Roho wake mwenye nguvu, walipende na kulihudumia Kanisa lake bila ya kuteteleka. Kanisa limewaombea viongozi wa Serikali mbali mbali, Majaji na Mahakimu, ili wanapotekeleza dhamana na utume wao, daima watafute ukweli, ili kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kanisa limesali na kuwakumbuka Wakristo wanaoteswa sehemu mbali mbali za dunia, ili katika mateso kama haya, waendelee kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo. Kanisa limewakumbuka na kuwaombea, wamisionari na makatekista ili waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote. Mwishoni, Mama Kanisa amesali pia kwa ajili maskini, wagonjwa, wanaoteseka na watu ambao wanahisi upweke katika maisha yao, ili wote hawa wapate faraja, furaha na upendo kutoka kwa Kristo Yesu! Ombi kwa lugha ya Kiswahili limetolewa na Pauline Mkondya wakati Sr. Editha Christopher Kaselekete wa Shirika la Masista wa Bikira Maria Malkia wa Afrika Sumbawanga, Tanzania, ameshiriki kupeleka vipaji wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu! Matendo makuu ya Mungu!

Papa: Maaskofu wakuu
29 June 2019, 16:25