Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume 2019: Maaskofu 31 Kupewa Pallio Takatifu watakazovishwa majimboni mwao kwa wakati muafaka! Papa Francisko: Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume 2019: Maaskofu 31 Kupewa Pallio Takatifu watakazovishwa majimboni mwao kwa wakati muafaka!  (Vatican Media)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Maaskofu Wakuu wapya 31

Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Papa pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema; Kristo Yesu aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, mitume na miamba wa imani, Jumamosi tarehe 29 Juni 2019, Majira ya saa 3:30 asubuhi kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Pallio Takatifu kwa Maaskofu wakuu wapya 31 walioteuliwa katika kipindi cha mwaka 2018- 2019 kati yao kuna Maaskofu wakuu 8 kutoka Barani Afrika. Hii pia ni siku maalum ambayo imetengwa na Kanisa ili kuonesha moyo wa umoja, upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kuchangia kwa hali na mali ili kusaidia kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ya huduma na upendo kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia!

Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema; Kristo Yesu aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu wakuu wapya wanavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha waamini wengi katika tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia!

Askofu mkuu Philip Arnold Subira Anyolo wa Jimbo kuu la Kisumu, Kenya alizaliwa tarehe 18 Mei 1956 huko Tongareni. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, hapo tarehe 15 Oktoba 1983 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 6 Desemba 1995 akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kericho na kuwekwa wakfu tarehe 3 Februari 1996. Papa Yohane Paulo II kunako tarehe 22 Machi 2003 akamteuwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Homa Bay na kusimikwa rasmi tarehe 23 Mei 2003. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Novemba 2018 akamteuwa kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo Katoliki la Kisumu, Kenya.

Askofu mkuu Zeferino Zeca Martins, S.V.D. wa Jimbo kuu la Huambo, Angola, alizaliwa tarehe 8 Machi 1966 huko Cacolo. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, akaweka nadhiri za daima tarehe Mosi, Oktoba 1994. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 6 Agosti 1995. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Luambo tarehe 19 Mei 2012 na kuwekwa wakfu tarehe 12 Agosti 2012. Tarehe Mosi Oktoba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akamteua kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Huambo, nchini Angola.

Askofu mkuu Fridolin Ambongo Besungu, O.F.M. Cap. wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC, alizaliwa kunako tarehe 24 Januari 1960. Baada ya masomo na majiundo yake kitawa, kunako mwaka 1987 akaweka nadhiri zake za daima kwenye Shirika la Ndugu Wadogo Wakapuchini na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1988. Baadaye aliendelea na masomo ya juu na hatimaye, kujipatia Shahada ya Uzamivu wa Taalimungu maadili kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Alfonsiana. Tangu wakati huo, alibahatika kuwa Paroko usu tangu mwaka 1988 hadi mwaka 1989.

Aliwahi kuwa Jaalim wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kinshasa; Mkuu wa Shirika na Makamu Mkuu wa Shirika nchini DRC. Amewahi pia kuwa Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Kitaifa nchini DRC, ASUMA na Mkuu wa Wakapuchini Barani Afrika, CONCAU. Akateuliwa na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Bokungu-Ikela tarehe 6 Machi 2005. Aliwahi pia kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Kole, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC. Aliwahi kuteuliwa kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo kuu la Mbandaka-Bikoro kabla ya kuteuliwa na Papa Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo hilo. Tangu mwezi Juni 2016 alikuwa ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO.

Askofu mkuu Antoine Kambanda wa Jimbo kuu la Kigali, Rwanda alizaliwa tarehe 10 Novemba 1958 katika Jimbo kuu la Kigali, Rwanda. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, alapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 8 Septemba 1990 na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa hija yake ya kitume nchini Rwanda mwaka huo. Katika maisha na utume wake, tangu mwaka 1990-1993 alikuwa ni mlezi na Gombera wa Seminari ndogo ya Ndera Kigali; 199-1999 aliendelea na Masomo yake katika Chuo cha Kipapa cha Alfonsianum.

Kuanzia mwaka 1999-2005 aliteuliwa kuwa ni Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Jimbo kuu la Kigali; Mkurugenzi wa Tume ya Haki na amani, Jaalimu wa Taalimungu Maadili katika Seminari kuu ya Nyakibanda na mwalimu wa kiroho wa Seminari Kuu ya Rutongo. Kuanzia Mwaka 2005-2006 aliteuliwa kuwa Gombera wa Seminari Kuu ya Falasafa huko Kibgayi na 2006 Gombera wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Caroli Borromeo huko Nyakibanda  katika Jimbo la Butare. Na tarehe 7 Mei 2013 alichaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Kibungo. Tarehe 19 Novemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akamteua Askofu Antoine Kambanda kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kigali.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga,  wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania, alizaliwa kunako tarehe 3 Novemba, 1966, Wilayani Bunda, Mkoani Mara. Baada ya masomo yake ya msingi na sekondari, huko Mbeya na Sumbawanga, kunako Mwaka 1989 alijiunga na Seminari kuu ya Kibosho, Moshi, kwa ajili ya masomo ya Falsafa na baadaye akaendelea na masomo ya Kitaalimungu huko Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam na hatimaye, kuwekewa mikono kama Shemasi, kunako mwaka 1995 baada ya kumaliza mwaka wa kichungaji, alioufanya katika Parokia ya Itaka, Jimbo Katoliki la Mbeya.

Tarehe 11 Julai, 1996 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo Katoliki la Mbeya na Hayati Askofu Yakobo Dominic Sangu. Historia inaonesha kwamba, huyu ndiye aliyekuwa Padre wa mwisho kuwekewa mikono na Hayati Askofu Sangu. Baada ya Upadrisho alifanya utume katika sehemu mbalimbali za Jimbo Katoliki Mbeya, kama Paroko usu huko Itumba na Mwalimu wa Seminari Ndogo ya Mbalizi. Kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2001 alijiendeleza kwa masomo ya juu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, ambako alijipatia shahada ya kwanza. Baada ya masomo yake, alirudi kuendelea na kazi yake kama Mkuu wa shule ya Sekondari ya Pandahill, kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2006.

Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2009 alijiendeleza kwa masomo ya juu zaidi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikojipatia Shahada ya uzamili katika masomo ya Sayansi Jamii. Kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2011 alikuwa ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, kilichoko Jijini Mwanza. Akiwa SAUT. Kunako Mwezi Agosti, 2010, alitumwa nchini Ujerumani kwa masomo ya juu zaidi, kama sehemu ya maandalizi ya kuwa ni Jaalimu wa Elimu hasa katika somo la Jiografia. Kabla ya kuhitimu masomo yake huko Ujerumani,  tarehe 9 Januari 2011 akapokea simu kutoka kwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania, ikimtaarifu kwamba, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amemteua kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Dodoma na hatimaye, kuwekwa wakfu kama Askofu, tarehe 19 Machi 2011.

Tarehe 17 Februari 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda na kusimikwa rasmi tarehe 4 Mei 2014. Tarehe 21 Desemba 2018 Baba Mtakatifu Francisko akaunda Jimbo kuu Jipya ya Mbeya nchini Tanzania linaloundwa na Jimbo Katoliki la Mbeya, Jimbo Katoliki la Iringa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu ametemua Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda.

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, alizaliwa kunako tarehe 12 Novemba, 1965, Parokia ya Sumve, Jimbo kuu la Mwanza. Alipata masomo yake ya sekondari, Seminari ya Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma na baadaye Nyegezi, Jimbo kuu la Mwanza. Kunako Mwaka 1987 alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, kwa ajili ya masomo ya Falsafa na baadaye mwaka 1989 aliendelea na masomo ya Taalimungu Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Alipadrishwa kunako tarehe 2 Julai 1995 akiwa ni Padre wa Jimbo kuu la Mwanza.

Tangu alipopadrishwa amefanya shughuli mbali mbali za kichungaji kama Paroko msaidizi, Gombera wa Seminari ndogo ya Nyegezi, Jimbo kuu la Mwanza na baadaye kunako mwaka 2002 hadi 2005 alikwenda Roma kwa masomo ya Sheria za Kanisa, kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbanian na hapo akajipatia shahada ya uzamili katika sheria, kanuni na taratibu za Kanisa. Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2011 aqlikuwa ni Mhazini mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza. Tangu mwaka 2008 hadi 2009 alikuwa ni Makamu wa Askofu, Jimbo kuu la Mwanza. Na baadaye mwaka 2009 aliteuliwa kuwa msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Mwanza kufuatia kifo cha Askofu mkuu Athony Mayala. 

Tarehe 27 Novemba 2010, akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bunda na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 20 Februari 2011 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, utume ambao ameutekeleza kwa muda wa miaka 7 kama Askofu na miaka 23 kama Padre. Jimbo kuu la Mwanza lilikuwa wazi, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumteua Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam hapo tarehe 21 Juni 2018. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 11 Februari 2019 akamteuwa Askofu Renatus Leonard Nkwande kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania.

Askofu mkuu John Bonaventure Kwofie wa Jimbo kuu la Accra, Ghana, alizaliwa tarehe 26 Aprili 1958 huko Powa, Jimbo Katoliki la Sekondi-Takoradi, Ghana. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, akapadrishwa kunako tarehe 23 Julai 1988, huko Kumasi, Ghana. Katika maisha na utume wake kama Padre, alipangiwa shughuli mbali mbali za kichungaji nchini Gambia na kati ya mwaka 1991 akapelekwa mjini Roma kwa ajili ya masomo ya juu katika Sayansi ya Maandiko Mtakatifu, maarufu kama Biblicum na huko akajipatia shahada ya uzamili.

Amewahi pia kuwa ni Makamu mkuu wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika kwa vipindi viwili; Padre mkuu wa Kanda ya Shirika, Afrika Magharibi, Mratibu wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika, utume alioufanya kazi ya mwaka 2003 hadi mwaka 2005. Kati ya Mwaka 2004 hadi mwaka 2012 alikuwa ni mshauri wa kwanza wa mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu ulimwenguni. Jimbo la Sekondi-Takoradi lilianzishwa kunako mwaka 1969 na liko chini ya Jimbo kuu la Cape Coast, Ghana. Tarehe 3 Julai 2014 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Sekondi-Takoradi, nchini Ghana. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 2 Januari 2019 akatemuwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Accra nchini Ghana.

Askofu mkuu Dabula Anton Mpako wa Jimbo kuu la Pretoria, Afrika ya Kusini, alizaliwa tarehe 6 Septemba 1959. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 28 Juni 1986 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo kama Padre akafanya utume sehemu mbali za Jimbo kuu la Pretoria kama Paroko-usu, Mlezi na Gombera. Kati ya mwaka 1991-1994 akatumwa na Jimbo kuu la Pretoria kwa masomo ya juu zaidi, Chuo Kikuu cha Loyola kilichoko nchini Marekani ili kujiendeleza katika Taalimungu ya shughuli za kichungaji.

Kati ya Mwaka 1994-1998 akateuliwa kuwa Gombera wa Seminari kuu ya Falsafa ya St. Peter, huko Garsfontein. Kati ya mwaka 1999-2004 akateuliwa kuwa Paroko na Dekano. Kati ya Mwaka 2005-2010 akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya St. Columba, na Mwaka 2010-2011, akahamishiwa kwenye Parokia ya Mt. Thomas Moore. Tarehe 6 Agosti 2011 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Queenstown. Askofu mkuu Dabula Anton Mpako ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 30 Aprili 2019 akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Pretoria, nchini Afrika ya Kusini.

Maaskofu Wakuu
28 June 2019, 17:44