Tafuta

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya Kuombea: Toba, Wongofu na Utakatifu wa Mapadre Duniani ili waweze kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya Kuombea: Toba, Wongofu na Utakatifu wa Mapadre Duniani ili waweze kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu. 

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Toba, Wongofu & Utakatifu!

Mtakatifu Yohane Paulo II mwaka 2002 akatenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni ukumbusho kwamba Yesu ni chemchemi ya huruma, upendo, msamaha na wokovu wa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama na chemchemi ya Sakramenti za Kanisa na wokovu wa binadamu. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Mt. Margareta Maria Alakoki akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002 akatenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 26 Juni 2019 amekazia kwamba, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni ukumbusho kwa waamini kwamba, Kristo Yesu anaishi “Christus vivit”; anawapenda waja wake anaendelea kujisadaka kama chemchemi ya huruma, upendo, msamaha na wokovu wa walimwengu. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia ili kuweza kupata: hifadhi, amani na utulivu wa ndani kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Waamini wajitahidi kwenda kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa Sakramenti ya Upatanisho. Kamwe waamini wasisite kujiaminisha chini ya Moyo Mtakatifu wa Yesu katika hija ya maisha yao hapa duniani!

Waamini wavutwe na hisia za upendo wa kweli unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Watumie siku hii kwa ajili ya kuombea toba, wongofu na utakatifu wa Mapadre na wanapofanya hivi, wamkumbuke hata yeye katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili maisha na utume wao wote, upate chapa ya upendo wa Mungu kwa wanadamu wote! Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre, lakini pia iwe ni siku ya kujenga na kudumisha umoja na udugu miongoni mwa wakleri. Mapadre wanapoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu wakumbuke kwamba, wanawabeba waamini waliokabidhiwa na kupigwa chapa katika sakafu ya nyoyo zao.

Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wakleri wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waonje huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wasikubali kumezwa na malimwengu, bali: utii, useja na ufukara, viwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakleri kuendelea kukesha kwa njia ya: Sala, Tafakari makini ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha wongofu wa shughuli za kichungaji. Kardinali Beniamino Stella anawaalika wakleri kujitaabisha kusoma na kutafakari ujumbe unaotolewa mara kwa mara na Baba Mtakatifu ili waweze kuboresha maisha na utume wao; katika uchovu na uchungu wa maisha na utume wa Kikasisi, waweze kupata faraja na matumaini yanayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu.

Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ni dalili kwamba wito na utume huu mtakatifu umehifadhiwa katika chombo cha udongo. Mapadre wanaopitia vipindi vigumu vya maisha na utume wao, wanapaswa kusindikizwa kwa huruma na upole; wasikilizwe kwa makini; wasaidiwe kufikia mang’amuzi na ukomavu katika maisha. Huu ni wajibu wa kwanza kwa Maaskofu mahalia lakini hata kwa Jumuiya nzima ya waamini pamoja na familia zao, ambazo mara nyingi zinabeba Msalaba mzito! Wakleri ni watu ambao wanapaswa pia kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha na utume wao! Kamwe Mapadre wasidhaniwe kuwa ni mashine za kutolea huduma ya mambo matakatifu!

Mapadre wapendwe katika ukweli na uwazi; wasaidiwe kupata mahitaji yao msingi. Waamini walei, wakishirikiana, wakisaidiana na kushauriana na Mapadre wao, maisha na utume wa Kanisa vitasonga mbele kwa ari kubwa zaidi! Pale Mapadre wanapoonekana kuchoka na kuanza kukata tamaa, waamini wawe mstari wa mbele kuwaenzi kwa sala na sadaka zao; kwa kutambua na kuthamini huduma zao pamoja na ushauri wa kidugu! Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre, iwe ni fursa ya kuwasindikiza Mapadre katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Katika majitoleo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mama Kanisa anawaalika watoto wake katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kushiriki Misa Takatifu, kupokea Ekaristi Takatifu na kutenda matendo ya huruma, kusali sala iliyoelekezwa na Mama Kanisa kama njia ya kulipia madhulumu dhidi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu yafanywayo na watu mbalimbali na hasa kwa kukosa heshima kwa Sakramenti Kuu, yaani Ekaristi Takatifu.

Matunda ya majitoleo hayo ni neema zibubujikazo toka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu! Ahadi zinazobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu: Nitawajalia neema zote watakazozihitaji katika hali yao ya maisha. Nitawajalia amani katika familia zao. Nitawafariji katika magumu yao yote. Nitakuwa kimbilio lao salama wakati wa maisha yao, na zaidi sana katika saa yao ya kufa. Nitawapa baraka tele katika shughuli zao zote. Wakosefu watapata katika Moyo wangu chanzo na bahari ya huruma isiyo na mwisho. Waamini walio vuguvugu watakuwa na bidii. Waamini wenye bidii watakwea kwa upesi katika ngazi za juu za ukamilifu.

Yesu anasema, nitabariki kila mahali ambapo picha au sanamu ya Moyo wangu Mtakatifu itawekwa na kuheshimiwa. Nitawajalia mapadre karama ya kuigusa mioyo migumu. Wale wote watakaoeneza Ibada hii kwa wengine majina yao yataandikwa ndani ya Moyo wangu na sitawasahau kamwe. Wale wote watakaopokea Sakramenti ya Ekaristi kila Ijumaa ya kwanza ya mwezi kwa miezi tisa mfululizo wakiwa katika hali ya neema ya utakaso, hawatakufa wakiwa na uadui nami, nitawapa neema ya kudumu katika uaminifu hadi mwisho na hawatakufa bila kupokea Sakramenti za mwisho.

Moyo Mtakatifu

 

27 June 2019, 17:12