Papa Francisko anawataka wahudumu Wakatoliki kwenye Viwanja wa Ndege wawe ni mashuhuda na vyombo vya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Papa Francisko anawataka wahudumu Wakatoliki kwenye Viwanja wa Ndege wawe ni mashuhuda na vyombo vya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. 

Papa Francisko: Iweni mashuhuda wa Neno & Sakramenti za Kanisa!

Wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo uwepo endelevu wa Yesu kati ya watu wake. Wawe ni watu waungwana, wanaoweza kuwashirikisha jirani zao Injili ya huruma, matumaini na amani ya ndani. Yote haya yanaweza kumwilishwa katika amani, kwa matendo, kwa maneno au tu, kwa tabasamu la kukata na shoka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wahudumu Wakatoliki wanaotoa huduma ya maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege wanao mchango mkubwa katika ukuaji wa maisha ya watu kiroho; wanao mchango pia katika mchakato wa kukuza na kudumisha maendeleo fungamani ya binadamu! Hii ni huduma makini inayotolewa hata wakati mwingine kwenye mazingira magumu na hatarishi. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, yanawawezesha watu wengi kusafiri. Hawa ni watu kutoka katika mataifa, tamaduni, dini na lugha mbali mbali, wanaokutana kila siku ya maisha. Hawa kila mtu ana historia ambayo inafahamika tu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Ni watu wenye furaha, lakini, kuna wengine wenye machungu moyoni; watu wenye matumaini pamoja na wasi wasi na hofu kuu nyoyoni mwao! Katika hali na mazingira kama haya, wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo  uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya watu wake. Wawe ni watu waungwana, wanaoweza kuwashirikisha jirani zao Injili ya huruma, matumaini na amani ya ndani. Yote haya yanaweza kumwilishwa katika amani, kwa matendo, kwa maneno au tu, kwa tabasamu la kukata na shoka! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 10 Juni 2019 alipokutana na kuzungumza na washiriki wa Semina ya Kimataifa kuhusu Wahudumu wa Wakatoliki wanaotoa huduma za maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege.

Utamaduni wa viwanja vya ndege unafumbatwa katika sera za kula na kulipa na wala hakuna cha bure! Kwani mzee bure alikwisha kufariki dunia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, lakini, wahudumu hawa kwa sadaka na majitoleo yao wanawafungulia watu wa malango ya Mungu, ili kuwaonjesha leo ya Mungu, kwa njia ya ukarimu, ukaribu na upendo! Ushuhuda wao ni ujumbe makini unaotolewa kwa wakati huo; ujumbe ambao unaweza kuacha alama ya kudumu katika akili na nyoyo za watu, na hii ndiyo nguvu ya majitoleo pasi na kujibakiza! Hawa ni watu wanaowasaidia wasafari kujipatia tena nguvu ili kusonga mbele na safari yao kama ilivyo kwa Computer mpakato, ambayo baada ya kutumika sana inahitaji kuongezewa nguvu. Ushuhuda wa wahudumu hawa umewasaidia wasafiri kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Injili na Sakramenti zake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maendeleo fungamani ya binadamu yanapaswa kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wao, kwa kumjali na kumheshimu mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni mwaliko wa kuzingatia shughuli zao, tamaduni, maisha ya kifamilia, dini na imani zao; uchumi na maelekeo yao ya kisiasa. Huduma hii itolewe kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu, kwa kuwaangalia watu wanaopita machoni mwao, wakiwa na “miwani ya Kristo Yesu”, ili kila mmoja wao, aweze kuonja uwepo wa Mungu karibu sana na maisha yake. Watambue kwamba, wao ni milango na madaraja ya kuwakutanisha watoto wa Mungu.

Huduma yao inaweza kuwasaidia hata wale Kondoo waliopotea, kurejea tena zizini na hivyo kuanza mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya ndani kutokana na sababu mbali mbali. Kwa wafanyakazi na wahudumu wa ndege, si rahisi sana kujenga nao mahusiano ya karibu, lakini hata hivyo, wahudumu hawa wamekuwa ni msaada mkubwa kwa familia zao. Katika viwanja vya ndege, kuna nafasi ya kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala na Sakramenti za Kanisa na kwamba, ndoto kubwa ni kujenga Jumuiya ya waamini wanaoweza kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu katika hali na mazingira haya!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ambao wakati mwingine wanazuiliwa kwenye Viwanja wa Ndege! Watu kama hawa waonje wema, huruma na ukarimu wa Makanisa mahalia; kwa kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki zao msingi. Huduma ya Injili ya upendo ni kielelezo makini cha uwepo wa karibu wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Kwa wakleri wanaohudumia katika viwanja vya ndege, wanakabiliana na changamoto kubwa ambazo wakati mwingine zinaweza kuwasababishia uchovu, hali ya kukata tamaa na hata wakati mwingine, kushindwa kuona mafanikio kwa macho ya kibinadamu!

Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, kwa kushauriana na Maaskofu mahalia, waangalie jinsi ambavyo wanaweza kuanza kuwaandaa watu wengine, wanaoweza kushiriki maisha na utume wao, katika raha na shida kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waamini walei watambue kwamba, wao ni wasimisionari wenye haki, dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa. Ubora wa utume wanaotekeleza unakwenda sanjari na ubora wa maisha yao ya kiroho, kumbe, wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya utume wa Mama Kanisa katika ujumla wake. Ari na mwamko wa kimisionari ni muhimu sana katika huduma hii! Bikira Maria, Mama wa Kanisa awalinde na kuwahifadhi kwa ulinzi na tunza yake ya kimama!

Papa: Wahudumu
11 June 2019, 09:06