Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewapatia Mabalozi na Wawakilishi wa Vatican mwongozo wa maisha na utume wao sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu Francisko amewapatia Mabalozi na Wawakilishi wa Vatican mwongozo wa maisha na utume wao sehemu mbali mbali za dunia! 

Papa Francisko: Ujumbe kwa Mabalozi & Wawakilishi wa Vatican!

Mwongozo wa maisha na utume wa Mabalozi na wawakilishi wa Vatican unawakumbusha kwamba, wao: Ni watu wa Mungu na Kanisa wenye ari na mwamko wa kitume. Ni wapatanishi na wawakilishi wa Papa; ni watu wanaochakarika kwa ajili ya maendeleo ya watu; maisha yao yanasimikwa katika utii, sala, huduma ya upendo na unyenyekevu wa maisha, kama wafuasi wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Jumatano tarehe 12 Juni 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Mabalozi wa Vatican kutoka katika nchi 103; kati yao kuna Mabalozi 98 na wengine 5 ni Wawakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huu ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa malengo ya Baba Mtakatifu Francisko anayetaka kuimarisha umoja na mafungamano miongoni mwa wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia! Kama sehemu ya maadhimisho ya mkutano huu, Baba Mtakatifu Francisko Alhamis, tarehe 13 Juni 2019 amekutana na kuzungumza nao.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwakumbusha Kanuni 10 wanazopaswa kuzingatia katika maisha na utume wao kama Mabalozi na Wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia! Mosi, watambue kwamba, wao ni watu wa Mungu, wanaopaswa kuheshimu na kutekeleza Amri za Mungu na kuishi kadiri anavyotaka Mungu, kiasi hata cha kukubali kupokea mateso, shida na changamoto mbali mbali za kiimani. Anasema, Balozi wa Vatican ni mtu anayeongozwa kwa Neno la Mungu, ili kuweza kufikiri, kuamua na kutenda; daima akijikabidhi na kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mungu. Ni mtu asiyekubali kiurahisi kumezwa na malimwengu.Sifa za mtu wa Mungu ni pamoja na: haki, upendo, huruma, ibada na msamaha! Pale wanaposhindwa kujitambua kwamba, ni watu wa Mungu wanakuwa ni chanzo cha kuanguka kwao wenyewe pamoja na kusababisha madhara kwa watu wengine.

Pili, Balozi wa Vatican ni mtu wa Kanisa kwani anamwakilisha Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa. Anapaswa kuwaheshimu, kuwalinda na kuwaendeleza wale wote anaokutana nao katika maisha na utume wake, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni kwa ajili ya huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu. Ni watu wanaopaswa kushuhudia fadhila za kibaba na kichungaji. Makatibu na Washauri wa Balozi za Vatican ni viongozi ambao wako kwenye mafunzo, ili kwamba, siku moja waweze hata wao kuwa ni Mabalozi kadiri ya mpango wa Mungu. Mabalozi wa Vatican wawe ni watu wa kiasi, wakazie mambo msingi kwa kutambua kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa wote!

Wawe wanyenyekevu wanapotambulisha Uso wa Kanisa, Mafundisho na Msimamo wa Kanisa kwa kuweka mambo binafsi kando, tayari kulinda na kulitetea Kanisa dhidi ya maadui wa ndani na wa nje! Mabalozi wajenge na kudumisha uhusiano na mafungamano na Maaskofu mahalia, Wakleri, Watawa na Waamini walei kwa kuwasindikiza katika utekelezaji wa maisha na utume wa Kanisa mahalia, yote haya yawe ni kwa ajili ya wokovu wa roho za watu! Sherehe kuu za Kanisa yaani: Noeli na Pasaka ni nyakati za kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na watu wa Mungu wanaounda familia yake.

Tatu, Balozi wa Vatican ni mtu mwenye ari na mwamko wa kitume, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa mwanga wa Kristo Mfufuka. Ni kiongozi anayepandikiza mbegu ya imani, matumaini na mapendo na matunda yake ni sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu aliyemkomboa binadamu kwa kumwaga Damu yake azizi pale Msalabani! Wajivunie kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, bila woga wala makunyanzi. Ari na mwamko wa kitume, unawalinda viongozi wa Kanisa ili wasitumbukie kwenye saratani ya mawazo ya udanganyifu.

Nne, Balozi wa Vatican ni mpatanishi, ni mjenzi wa umoja, chachu ya majadiliano na maridhiano kati ya watu; ni mtu asiyekuwa na upendeleo na anayesimamia malengo, mwamuzi mwenye haki, mkweli na muwazi anayepania kudumisha misingi ya haki na amani bila ya kuruhusu kutumiwa kinyume chake. Ni chombo cha mawasiliano na huduma kwa Maaskofu mahalia na watu wa Mungu katika ujumla wake. Ni kiongozi mwenye madaraka yanayolenga kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu na ushauri. Balozi wa Vatican anapaswa kujenga utamaduni wa kukutana na watu, ili kuimarisha umoja na maridhiano, kama mwakilishi wa sura ya Kanisa la Kiulimwengu mbele ya Makanisa mahalia na Serikali zao!

Tano, Balozi wa Vatican ni mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na anatenda kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na anatekeleza malengo yake kwa ajili Kanisa na viongozi wa Serikali. Ni mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, Ubalozi wa Vatican unapaswa kueleweka kuwa ni “Nyumba ya Papa”. Ni watu ambao wanapaswa kuondokana na unafiki kwani wao ni madaraja yanayomuunganisha Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na wanawanchi wanaowahudumia, kumbe ni mwakilishi wa Papa. Dhamana na utume huu unahitaji: uwepo, uwezo wa kusoma alama za nyakati, unyenyekevu, weledi pamoja na uwezo wa kuwasiliana na kujadiliana na kwamba wao daima ni wasafiri.

Balozi awe na uhusiano wa karibu na familia ya Mungu anayoihudumia, bila kusahau kujenga mahusiano mema pia na wanadiplomasia pamoja na viongozi wa Serikali. Awe na ari, bidii na moyo wa kutembelea Jumuiya zile ambazo hazitapata hata siku moja nafasi ya kutembelewa na Papa, kama kielelezo cha uwepo wa karibu wa Kristo na Kanisa lake. Wawe na ujasiri wa kwenda pembezoni mwa vipaumbele vya mwanadamu. Wawe ni mashuhuda wa Kristo katika maisha yao kwa kukazia ukweli na neema ya kushiriki amana na utajiri unaobubujika kutoka kwa Kristo. Mabalozi wa Vatican wanapaswa kujiendeleza na kujipyaisha kila wakati pamoja na kutoa taarifa kwa Papa kuhusu yale yanayoendelea kujiri katika uwakilishi wao. Wawe na ufahamu mkubwa wa tamaduni, mila, desturi na lugha ya watu mahalia; kwa kuwa wazi kwa wote. Wajiepushe kujiunga na makundi ya mitandao inayoonesha kinzani na ukakasi kwa Sekretarieti kuu na Kanisa la Roma.

Sita, Balozi wa Vatican ni mtu anayechakarika usiku na mchana ili kufanikisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila “kuzenguliwa” na ugumu wa mawazo, kiroho na kiutu wala kutekeleza mambo yake kwa “mwendo wa kinyonga”. Huyu ni kiongozi anayehamasishwa kutafuta mafao ya wengi, daima akiwa mwaminifu kwa dhamana na utume wake. Ni mtu anayeweza kusoma alama za nyakati, tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika hali ya utulivu na amani ya ndani. Watambue kwamba, wao ni Maaskofu na wachungaji, licha ya kuishi hapa duniani, lakini wakumbuke kwamba wao si wa ulimwengu huu, wawe na hekima kama nyoka na wapole kama njiwa. Kama wafuasi waaminifu wa Kristo Yesu, wajitahidi kuiga mifano ya Mitume na wafuasi wa kwanza wa Yesu, waliovutwa na hatimaye kuambatana na Kristo Yesu katika maisha yao!

Saba, Balozi wa Vatican ni mtii anayetekeleza dhamana hii kwa uhuru wa ndani na kwamba, utii kwa Injili ni utimilifu wa utii wote. Utii wa kwanza unafumbatwa katika wito unaomwajibisha mtu kumfuasa Kristo Yesu, kwa kumtii Mungu zaidi, Kanisa na viongozi wake wakuu, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Utii ni dira katika mchakato wa kufikiri, kuamua na kutenda kwa hekima na unyenyekevu mkuu. Utii unakita mizizi yake katika: busara na upendo kwa Mungu na jirani. Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utii wa Kristo Yesu kwa Baba yake wa mbinguni. Mabalozi wa Vatican wawe mstari wa mbele kuonesha ushuhuda wa utii “Medice, cura te ipsum”.

Nane, Balozi wa Vatican ni mtu wa sala anayetoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Kristo Yesu kama amana na utajiri anao paswa kuutangaza, kuushuhudia na kuuwakilisha. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo kamwe hawezi kumtupa mtu anayemkimbilia na kumwambata. Wajenge utamaduni na mazoea ya kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu kwa njia ya sala, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni wahudumu waaminifu wa Neno la Mungu.

Tisa, Balozi wa Vatican ni mtu mwenye upendo tendaji unaomwilisha sala katika matendo ya huruma! Ni mtu anayethubutu kugeuza Fumbo la Ekaristi Takatifu na kuwa ni chemchemi ya Injili ya upendo kwa maskini, kama kielelezo cha imani tendaji. Ni kiongozi anayepaswa kujihusisha kikamilifu na shida pamoja na mahangaiko ya watu hususan katika masuala: ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya binadamu: kiroho na kimwili. Balozi wa Vatican atoe kipaumbele cha pekee kwa huduma ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama kielelezo makini cha utume na uwepo wake kama Baba na Mchungaji. Huu ni upendo unaomwilishwa katika sadaka na majitoleo; ili kusimamia haki na amani. Wawe makini ili wasipokee zawadi zitakazokwamisha uhuru wao na kuwatumbukiza katika utumwa.

Kumi, Baba Mtakatifu anasema, Balozi wa Vatican anapaswa kuwa mnyenyekevu na mpole wa moyo kama alivyo Kristo Yesu. Kamwe asitake kupendwa, kutukuzwa, kuheshimiwa, kushangiliwa na kupewa upendeleo. Lakini badala yake, wakubali wanaponyenyekeshwa, wanapodharauliwa, wanaposhitakiwa na kutuhumiwa kwa uwongo na zaidi wanaposahauliwa, ili Kristo Yesu aweze kupewa sifa na utukufu zaidi!

Papa: Mabalozi
13 June 2019, 16:50