Tafuta

Vatican News
Papa Francisko Ujumbe kwa Jumuiya ya "Nuovi Orizzonti: Kumbu kumbu na Matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi! Papa Francisko Ujumbe kwa Jumuiya ya "Nuovi Orizzonti: Kumbu kumbu na Matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi! 

Jumuiya ya Nuovi Orizzonti: Jubilei ya Miaka 25: Kumbu kumbu & Matumaini

Papa Francisko: Anaitaka Jumuiya ya "Nuovi Orizzonti" kuendeleza kumbu kumbu ya huruma na wema wa Mungu katika maisha yao, kama fursa ya kukutana na Mungu. Huyu ndiye Mungu ambaye amewasindikiza, akawawezesha kukua na kukomaa. Mwenyezi Mungu amewakuta katika jangwa tupu litishalo, akawazunguka na kuwatunza na kuwahifadhi kama mboni ya jicho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti” iliyoanzishwa na Chiara Amirante, katika Sherehe ya Pentekoste, imeadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Hii imekuwa ni historia yenye matatizo, changamoto na fursa za kuweza kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo! Jumuiya hii imekuwa ni chemchemi ya matumaini mapya kwa wasichana wanaojikuta wametumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Jumuiya hii tayari imekwisha eneza utume wake nchini Uingereza, Brazil, Uswiss na Argentina. Jumuiya hii imeanzishwa ili kusikiliza na kujibu kilio cha wanawake wanaoteseka na kunyanyaswa katika mifumo ya utumwa mamboleo. Hadi sasa kuna jumla ya wanachama 700 wanaosaidia kutoa huduma kwa wasichana wanaotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo. Si rahisi sana kuweza kuonja magumu wanayokabiliana nayo wanawake na wasichana wanaoishi katika hali na mazingira haya anasema Chiara Amirante, muasisi wa Jumuiya hii. Jubilei ya Miaka 25 ya Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti” ni muda wa kumshukuru Mungu kwa neema, baraka na tunza yake na kuomba tena nguvu ya kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa wanajumuiya wa “Nuovi Orizzonti” anasema, alitamani sana kuwa kati yao wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hii, lakini kutokana na majukumu mengine ya kichungaji, ameamua kuwatumia ujumbe huu. Ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa wema ambao ameitendea Jumuiya hii na katika maisha ya kila mmoja wao. Baba Mtakatifu anawataka kuendeleza kumbu kumbu ya huruma na wema wa Mungu katika maisha yao, kama fursa ya kukutana na Mungu. Huyu ndiye Mungu ambaye amewasindikiza, akawawezesha kukua na kukomaa. Mwenyezi Mungu amewakuta katika jangwa tupu litishalo, akawazunguka na kuwatunza na kuwahifadhi kama mboni ya jicho!

Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hata kama katika maisha, hawataweza tena kuolewa na kupata uzao, lakini wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha kwa jirani zao. Mambo makuu mawili wanapaswa kuyazingatia: Kumbu kumbu na matumaini yanayofumbatwa katika furaha. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume, huku akiwataka waendelee pia kuwa wacheshi katika maisha!

Papa: Ujumbe
11 June 2019, 08:50