Tafuta

Papa Francisko wakati wa Katekesi yake 19 Juni 2019 Papa Francisko wakati wa Katekesi yake 19 Juni 2019 

Papa Francisko:Sala ndiyo pafu la kupumulia mitume wa nyakati zote!

Roho Mtakatifu ni msanii wa umoja,anafanya Kanisa likue hata katikati ya vizingiti vya kibinadamu na kila kashfa.Zawadi ya Roho ya kinabii haikukabidhiwa kwa baadhi tu,bali kwa wote wanaoomba kwa Jina la Bwana.Hayo yamekumbushwa na Papa Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano 19 Juni 2019 katika uwanja wa Mtakatifu Petro,Vatican,akitafakari juu ya Pentekoste kama mwendelezo wa katekesi yake kuhusu kitabu cha Matendo ya Mitume.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kabla ya tafakari ya Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Juni 2019 katika uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa waamini na mahujaji kutoka pande za dunia, imesomwa somo kutoka Matendo ya mitume isemayo “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizo gawanyika, kama ndimi za moto zilizo kaa juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajalia kutamka.Kutokana na hiyo Baba Mtakatifu Francisko ameanza kusema kuwa:Siku hamsini baada ya Pasaka, wakati wakiwa katika nyumba ya karamu kuu na ambayo sasa ilikuwa ni nyumba yao na mahali ambapo uwepo wa Maria Mama wa Bwana ulikuwa ni jambo msingi kwa mitume waliokuwa wanaishi tukio ambalo lilikuwa linashinda matarajio yao.

Baada ya upepo ukafika moto unaokumbusha moto usiounguza kichaka na mlima Sinai

Na walikuwa wameungana katika sala. Sala ndiyo pafu la kupumua mitume wa nyakati zote, bila sala haiwezekani kuwa mitume wa Yesu; sala ni hewa, ni pumzi ya maisha ya kikristo, bila sala sisi hatuwezi kuwa wakristo! Ndipo wakashutukizwa na moto wa Mungu. Ni moto ambao hauwezi kuvumilia kufungwa. Unafungua milango kwa njia ya nguvu za upepo ambao unakumbushwa ruah,mvumo wa mchana kutwa na kutimiza ahadi ya nguvu aliyoitoa Mfufuka kabla ya kuwaaga kwenda mbinguni ( taz Mdo 1,8). Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi (Mdo 2,2). Baba Mtakatifu Francisko amesema, baada ya upepo huo ukafika moto ambao unakumbusha ule moto wa kichaka na Mlimani Sinai katika zawadi ya amri kumi  (Kut 19,16-19).

Katika utamaduni wa kibblia, moto unasindikiza maonyesho ya Mungu. Katika ishara ya moto wa Mungu anakabidhi neno hai na lenye nguvu (Eb 4,12), ambalo linafungua wakati ujao; moto unafafanua ishara ya kazi ya kupasha, ya kuangaza na kuonja ndani ya mioyo; utunzaji wake katika kuimarisha uhai wa kazi ya binadamu, ya kuitakasa na kuipyaisha. Wakati mlimani Sinai ilisikika sauti ya Mungu, Baba Mtakatifu anathibitisha, na huko Yerusalme wakati wa Pentekoste aliyezungumza ni Petro, mwamba ambao Yesu Kristo aliuchagua ili kuimarisha Kanisa lake. Neno lake, udhaifu na uwezo wake hadi wa kumkana Bwana, lakini kwa kupitiwa na Roho, anapata nguvu, anageuka kuwa na uwezo kuchoma mioyo na kuwafanya wengine wakimbilie uongofu. Mungu kwa hakika alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu (1Kor 1,27).

Kanisa linazaliwa kwa njia ya mooto na upendo.

Baba Mtakatifu akiendelea na katekesi yake amefafanua kwamba, Kanisa kwa dhati linazaliwa kwa njia ya moto wa upendo, kutokana na  moto unaowaka wa Pentekoste na ambao unajionesha kwa nguvu ya Neno la Mfufuka ndani ya Roho Mtakatifu. Upatanisho mpya na wa mwisho unaundwa si, tu juu ya sheria iliyoandikwa juu ya ubao wa mawe bali kwa njia ya matendo ya Roho Mtakatifu wa Mungu ambaye anafanya mambo yote kuwa mapya na kukita ndani ya mioyo ya mwili. Neno la Mitume linapenya kwa njia ya Roho ya Mfufuka na kugeuka neno jipya, lenye kuwa na tofauti, lakini ambalo linaweza kueleweka na karibia kufafanuliwa kwa lugha zote. Hiyo ni kwa sababu “kila mmoja alisikika akinena kwa lugha yake mwenyewe” (At 2,6). Hii ni lugha ya ukweli na ya upendo, ambayo ni lugha ya ulimwengu kwa maana hata wasio jua kusoma na kuandika wanaweza kuitambua lugha hiyo, amesisitiza Baba Mtakatifu Francisko. Lugha ya ukweli na upendo inajulikana kwa wote. Ni lugha ambayo inaeleweka kwa wote. Iwapo wewe unakwenda na ukweli,katika moyo wako, kuwa na uwazi na kwenda na upendo, wote watatambua kuwa wewe ni mkweli na mwenye upendo hata kama huwezi kuzungumza vizuri.

Roho inasaidia Kanisa kwenda mbele zaidi ya vizingiti vya kibinadamu, vya dhambi na kila aina ya kashfa!

Baba Mtakatifu aidha anafafanua juu ya kazi ya Roho kwamba, Roho Mtakatifu hajioneshi tu wakati wa maelewano ya milio ya sauti inayounganika pamoja na kutengeneza sauti zilizo tofauti, bali inajiwakilisha kama  Kiongozi wa Kikundi cha kupiga vyombo na noti zake za kusifu kwa ajili ya “matendo makuu ya Mungu”.  Roho Mtakatifu ni mkuu wa muungano na msanii wa mapatano yanayofanya kuondoa vizingiti kati ya wayahudi na wagiriki, kati ya watumwa na walio huru, kwa kuwafanya kuwa mwili mmoja. Yeye anajenga jumuiya ya waamini na kuleta umoja wa mwili na wajumbe wengi. Yeye anafanya kukua kwa Kanisa na kulisaidia kwenda mbele zaidi ya vizingiti vya kibinadamu, vya dhambi na kila aina ya kashfa! Maajabu ni mengi na kila mmoja anajiuliza kama wale watu walikuwa wamelewa. Kwa njia hiyo Petro anasimama na kutangaza kwa niaba ya Mitume wote na kwa kusoma tukio hilo katika mwanga wa Joeli 3, mahali ambapo alitangaza uvuvio wa Roho Mtakatifu. Wafuasi wa Yesu hawakuwa wamelewa, bali wanaishi  kama anavyoeleza Mtakatifu Ambrosi kwamba “ulevi wa Roho” ambao unavuvia katikati ya watu wa Mungu ule unabii kwa njia ya ndoto na maono. Hata hivyo zawadi hiyo ya kinabii haikukabidhiwa kwa baadhi tu, bali kwa wale wote wanaoomba kwa njia ya Jina la Bwana.

Tangu sasa na kuendelea Roho wa Mungu anakita ndani ya mioyo

Baba Mtakatifu Francisko amesema tangu sasa na kuendelea Roho wa Mungu anaendelea kukita ndani ya mioyo na kupokelewa wokovu unaopitia kwa njia ya Mtu mmoja Yesu Kristo, Yule mbaye aliwambwa kwa misumari juu ya Msalaba na ambaye Mungu alimfufua, akamwondolea uchungu wa mauti (Mdo 2,24). Ni yeye aliyevuvia Roho na ambaye ni kama kikundi cha vyombo vya nyimbo za kusifu, ambaye wote  wanaweza kusikiliza. Ni kama  alivyosema Papa Mstaafu  Benedikto XVI, “Pentekoste ndiyo hii, Yesu na wakati huo huo ni Mungu mwenyewe, alikuja kwetu na anatuvutia kwake” (Mahubiri tarehe 3 Juni 2006). Roho anafanya kazi ya kuwa kivutio cha Mungu. Mungu anatuvutia kwa upendo wake na hivyo kutuhusisha ili kusogeza historia na kuanza michakato kupitia njia mpya ambazo zinakita ndani ya uhai mpya. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu tu, mwenye uwezo wa kuleta ubinadamu mpya na kuupyaisha udugu kwa kila  mantiki, kuanzia na wale wote wanaokaribisha roho hiyo. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha katekesi yake akiomba Bwana ili tuweze kufanya uzoefu wa Pentekoste mpya, ambayo inapanua mioyo yetu na kuleta maelewano ya hisia zetu na zile za Kristo na ili tuweze kutangaza  Neno lake bila aibu, lenye uwezo wa kuleta mapinduzi; na  tushuhudie nguvu ya upendo ambao unatualika katika maisha yote ambayo tunakutana nayo.

19 June 2019, 13:40