Papa Francisko asema, kuenea kwa Injili sehemu mbali mbali za dunia ni matunda ya Fumbo la Ufufuko, chemchemi ya maisha mapya! Papa Francisko asema, kuenea kwa Injili sehemu mbali mbali za dunia ni matunda ya Fumbo la Ufufuko, chemchemi ya maisha mapya! 

Papa Francisko: Safari ya Injili Ulimwenguni: Ufufuko wa Yesu!

Injili kuenea sehemu mbali mbali za dunia ni matunda ya Fumbo la Ufufuko, chemchemi ya maisha mapya. Mitume waliendelea kuwa watiifu, wakawa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali pamoja nao wanawake, na Mariam Mama yake Yesu. Walikuwa wanajiandaa kupokea zawadi na nguvu ya Mungu kutoka juu, ili kuimarisha umoja na mshikamano kati yao, Jumuiya ya kwanza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 12 Juni 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameendeleza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume. Hii ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji: Wahusika wakuu katika mchakato huu ni Neno la Mungu na Roho Mtakatifu sanjari na Ushuhuda wa Mitume! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kuenea kwa Injili sehemu mbali mbali za dunia ni matunda ya Fumbo la Ufufuko, chemchemi ya maisha mapya.

Mitume waliendelea kuwa watiifu, wakawa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali pamoja nao wanawake, na Mariam Mama yake Yesu. Walikuwa wanajiandaa kupokea zawadi na nguvu ya Mungu kutoka juu, ili kuimarisha umoja na mshikamano kati yao. Hii ndiyo Jumuiya ya kwanza ya waamini iliyokuwa inaundwa na watu takribani 120, ndani mwake wakiwemo Mitume 12, kielelezo cha makabila 12 ya Israeli. Baada ya mateso na kifo cha Kristo, Yuda Iskarioti, baada ya kumsaliti Kristo Yesu na hatimaye kujinyonga, idadi ya Mitume ilibakia 11. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yuda Iskarioti alianza kujitenga na Mitume wengine kidogo kidogo; akawa anakwapua fedha iliyotolewa kwa ajili ya huduma kwa maskini, kiasi hata cha kupoteza dira na mwelekeo wa sadaka na majitoleo yake! Akatafunwa na kupekenywa kwa virusi vya jeuri na kiburi!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ule moyo wa urafiki uliokuwa umejengwa ndani mwake, ukageuka kuwa ni uadui na kiongozi wa wale watu waliokwenda kumkamata Kristo Yesu. Yuda Iskarioti alikuwa amehesabiwa pamoja na Mitume wengine na akapata sehemu ya huduma hii. Katika safari ya maisha yake, akajikuta akiwa anataka “kujiokoa mwenyewe” na hatimaye, akaanza pole pole kutoka katika Jumuiya ya Mitume. Akakoma kuwa ni sehemu ya Mitume wa Yesu kutoka katika undani wa moyo wake, akajikweza na kuwa juu ya Mwalimu wake! Basi kama yasemavyo Maandiko Matakatifu, mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka. Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akadelma, maana yake Konde la damu!

Yuda Iskarioti akachagua kufumbata utamaduni wa kifo, badala ya kuenzi Injili ya uhai; Mitume 11 wakaamua kufuata njia ya baraka, wakawajibika katika historia na hatimaye, kuzaa matunda kizazi baada ya kizazi kutoka katika taifa la Israeli hadi kuanzishwa kwa Kanisa! Usaliti na hatimaye, kifo cha Yuda Iskarioti kilisababisha donda kubwa katika maisha na utume wa Jumuiya ya kwanza! Petro akatoa ushauri wa mtu ambaye angeweza kuziba nafasi ya Yuda Iskarioti kwamba, awe ni mfuasi wa Kristo tangu Yesu alipobatizwa Mtoni Yordani hadi alipopaa kwenda zake mbinguni. Haya ndiyo mang’amuzi ya Kijumuiya yanayopania kuangalia ukweli wa mambo kwa jicho la Kimungu, Umoja na Ushirikiano.

Yusufu aitwaye Barsaba pamoja na Mathiya, wakaombewa na hatimaye kupigiwa kura na kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na Mitume kumi na mmoja! Huu ni ushuhuda wa umoja wa Mitume unaovunjilia mbali: kinzani, utengano, haki binafsi na kwamba, umoja na mshikamano ni ushuhuda wa kwanza unaotolewa na Mitume wa Yesu, kielelezo kwamba, kwa hakika wao wamekuwa ni wafuasi amini wa Yesu kwa kupendana wao kwa wao!  Mitume wa Yesu wanashuhudia mtindo wa maisha ya Kristo na wanakuwa kweli ni mashuhuda wa kazi ya ukombozi, kwa njia ya umoja na maisha mapya kati ya watu wa Mungu.

Na kwa njia hii, wanashuhudia pia uwepo endelevu wa Kristo Mfufuka kati yao na kama kielelezo cha sadaka na majitoleo yao! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kugundua tena ule uzuri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka; kwa kuondokana na tabia ya kutaka kujitafuta wenyewe na kukataa kupokea zawadi ya Mungu na hatimaye, kuangukia katika ubinafsi. Umoja na uhuru kamili ni vinasaba vinavyowaunganisha Mitume wa Yesu; kwa kuondokana na tabia ya kutaka kumezwa na malimwengu na hatimaye, kuwa kweli ni “martyres” yaani mashuhuda amini wa Mungu aliye hai anaendelea kutenda kazi katika historia!

Papa: Katekesi
12 June 2019, 15:00