Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema: Michezo daima inalenga kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu! Papa Francisko anasema: Michezo daima inalenga kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu! 

Papa Francisko: Michezo ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tunu msingi za kuheshimiana, ujasiri, tabia ya kuwajali wengine, uwiano, nidhamu na udhibiti binafsi wanazojifunza wana michezo ni muhimu sana katika maandalizi ya mashindano katika maisha. Michezo daima inalenga kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu. Vijana washirikishwe zaidi katika michezo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 13 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kimataifa la Umoja wa Mchezo wa Kuteleza Kwenye Barafu “International Skating Union”. Baraza hili linapania pamoja na mambo mengine kuendeleza mchezo wa kuteleza kwenye barafu sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwawezesha watu wengi zaidi kuona uzuri wa mchezo huu, kama chemchemi ya furaha, kwa kukutana na wengine, kwa kuwa hai pamoja na kuendelea kufurahia karama na mapaji mbali mbali kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayowakirimia katika maisha na hususan katika mchezo kuteleza kwenye barafu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mchezo huu unachota nguvu yake kutoka katika: uhalisia wa maisha, uhuru wa mtu kutembea, kwa njia ya mazoezi na nidhamu, kazi ya timu pamoja na ushiriki na mchango wa mtu binafsi. Kimsingi, mchezo huu umekuwa ni mchezo jumuishi unaovunjilia kuta za utengano wa kijamii na hivyo kutoa nafasi kwa watu wa marika mbali mbali kushiriki kikamilifu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatia shime wajumbe wa Baraza la Kimataifa la Umoja wa Mchezo wa Kutekeleza Kwenye Barafu ili uweze kuwa ni kati ya michezo inayowaletea watu furaha katika kiwango cha juu kimataifa.

Baba Mtakatifu anawataka kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha vijana zaidi katika mchezo, ili kwa malezi na maongozi yao, waweze kukua na kukomaa zaidi katika michezo na kama wazalishaji. Mwishoni Baba Mtakatifu anasema, tunu msingi za kuheshimiana, ujasiri, tabia ya kuwajali wengine, uwiano, nidhamu na udhibiti binafsi wanazojifunza wana michezo ni muhimu sana katika maandalizi ya mashindano katika maisha. Michezo daima inalenga kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu.

Papa: Michezo
13 June 2019, 16:31