Tafuta

Papa Francisko: Utambulisho endelevu wa Jumuiya ya Kikristo: Mafundisho ya Mitume; Ushirika katika kuumega mkate na katika sala! Papa Francisko: Utambulisho endelevu wa Jumuiya ya Kikristo: Mafundisho ya Mitume; Ushirika katika kuumega mkate na katika sala! 

Papa: Msingi wa Jumuiya ya Kikristo: Mafundisho, Umoja, Kuumega Mkate & Sala

Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilidumu katika mafundisho ya Mitume, katika ushirika, katika kuumega mkate na katika sala. Haya ni matunda ya Roho Mtakatifu alipoishukua Jumuiya ya kwanza ya Wakristo, watu wengi wakasikia ndani mwao wakiwa wanachomwa na mafundisho ya Mitume, wakaamua wenyewe kujiunga na Kanisa na kubatizwa na hatimaye, wakashukiwa na Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mzunguko wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume anaendelea kupembua: mchango wa Neno la Mungu na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu kiroho na kimwili. Wahusika wakuu katika mchakato huu ni Neno la Mungu na Roho Mtakatifu sanjari na shuhuda wa Mitume! Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilidumu katika mafundisho ya Mitume, katika ushirika, katika kuumega mkate na katika sala. Haya ni matunda ya Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipoishukua Jumuiya ya kwanza ya Wakristo, watu wengi wakasikia ndani mwao wakiwa wanachomwa na mafundisho ya Mitume, wakaamua kwa “raha zao” wenyewe kujiunga na Kanisa na kubatizwa katika jina la Yesu na hatimaye, wakashukiwa na Roho Mtakatifu.

Watu zaidi ya elfu tatu wakaongezeka katika Jumuiya ya kwanza ya Wakristo na kujenga udugu katika Kristo, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ushuhuda wa imani thabiti ya Wakristo wa Kanisa la mwanzo ilikuwa ni kazi ya Mwenyezi Mungu, aliyetenda miujiza kwa njia ya Mitume wa Yesu, huu ukawa ni ushuhuda wa ufunuo wa Kristo katika uhalisia wa maisha ya watu! Mwinjili Luka analionesha Kanisa la Yerusalemu kama kielelezo makini cha Jumuiya ya Kikristo inayosimikwa katika udugu wenye mvuto na mashiko. Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 26 Juni 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Hii ni Katekesi ya mwisho kwa mwezi Juni, kabla ya kuanza likizo ya kipindi cha kiangazi, ambapo katekesi zote za Jumatano zitasitishwa na zitarejea tena mwezi Agosti, 2019. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kitabu cha Matendo ya Mitume, kinawawezesha kuangalia maisha na utume wa familia ya Mungu, iliyokuwa inajengeka katika msingi wa “koinonia” yaani “umoja” wa udugu katika Kristo Yesu. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilidumu katika mafundisho ya Mitume, katika ushirika, katika kuumega mkate kama kumbu kumbu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kwa maneno mengine walikuwa wanaadhimisha Fumbo la Ekaristi na katika sala.

Huu ndio utambulisho wa Jumuiya ya kwanza ya Wakristo, mfano bora wa kuigwa hata kwa Wakristo katika ulimwengu mamboleo. Hawa ni waamini waliojipambanua kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe ubinafsi na uchoyo hauwa na nafasi katika utume wao. Ni jumuiya iliyokita mizizi yake katika umoja na mshikamano; ikataabikiana na kusaidiana kwa hali na mali kama kielelezo cha ujirani mwema. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, neema ya Ubatizo, iliwawezesha Wakristo wa mwanzo kuuza mali na vitu vyao na kuwagawia watu wote kadiri ya mahitaji yao. Kwa hakika, ilikuwa ni Jumuiya iliyopambwa kwa ukarimu, sadaka, majitoleo kwa wahitaji zaidi; kwa kuwatembelea na kuwasaidia wagonjwa; kwa kuwafariji wenye shida na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Huu ni ushuhuda wa udugu na umoja kama kielelezo cha Jumuiya ya kwanza ya Wakristo.

Mwinjili Luka anaendelea kufafanua kwamba,  siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Mwenyezi Mungu akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale watu waliokuwa wakiokolewa. Kumbe, kukua na kupanuka kwa Kanisa ni neema na kazi ya Mungu ambaye ameendelea kuimarisha Agano lake na watu wake. Hii ni nguvu yenye mvuto inayowashangaza wengi na kanuni ambayo Jumuiya ya waamini wa nyakati zote inajitahidi kuimwilishwa katika maisha na utume wake!

Mwishoni, mwa katekesi yake, Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Roho Mtakatifu aendelee kupyaisha maisha ya waamini, kwa kukazia umoja na mshikamano. Waamini watambue kwamba,  maadhimisho mbali mbali ya Liturujia ni nafasi ya kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha, ili kuendeleza umoja na mshikamano. Kanisa liwe ni mahali penye milango wazi kwa ajili ya kuingia kwenye Yerusalemu ya mbinguni.

Papa: Jumuiya ya Kikristo

 

26 June 2019, 14:33